Sunday, January 28, 2018

BWANA, TUFUNDISHE SISI KUSALI (Luka 11:1)


SALA / MAOMBI
Hili ni tendo ambalo watu wanaoamini humwendea Mungu wakimwabudu, wakifanya toba, wakimshukuru na kumwomba mambo mbali mbali. Sala / Maombi ni mawasiliano ya moja kwa moja kati ya mtu anayeamini na Mungu. Unamweleza Mungu kile kilichomo ndani yako (hatuombi kwa kukariri bali tunasema kile kilichomo ndani yetu); yanaweza kuwa ni sala / maombi binafsi au maombezi kwa ajili ya wengine.

Tunaposoma Biblia katika Injili ya Luka 11:1, mwanafunzi wa Yesu anamwambia Bwana wake kwamba:

“…Bwana, tufundishe sisi kusali…” – Luka 11:1

Kuna jambo la kuzingatia hapa: Kabla ya kuingia katika maombi, ni muhimu sana kutambua kwanini tunaomba, ni nani tunapaswa kumwomba, na kwanini tumwombe yeye; baada ya kufahamu hivyo, hapo ndipo tuingie katika maombi.

1. Tunaomba kwa sababu sisi ni dhaifu, hatujitoshelezi pasipo msaada wa kiroho. Tunahitaji dira, mwongozo na usimamizi ili tuweze kutenda vema. Pia tunasali kwa ajili ya kurudisha shukrani kwa Yeye atutimiziaye haja zetu.

2. Tunapaswa kumwomba Mungu ambaye ndiye muweza wa yote. Sala / Maombi yetu yote yanamwelekea Mungu.  Yeye anaweza kutujibu kwa namna mbalimbali: mf. kupitia watu, viumbe wa kiroho, na hata kupitia mazingira;  hivyo sisi hatutazami ni kwa njia gani tumepokea bali tunatazama ni wapi kimetoka. Kwa hiyo tunamwomba Yeye (Mungu) aliye chanzo cha baraka zetu.

3. Tunamwomba Mungu kwa sababu Yeye ndiye muweza wa yote; vitu vyote vimetoka Kwake na hata sisi ni Wake. Katika Zaburi 33 Biblia inasema,

“…Nchi imejaa fadhili za BWANA. Kwa neno la BWANA mbingu zilifanyika, Na jeshi Lake lote kwa pumzi ya kinywa Chake. – Zab 33:5-6

Hivyo, ni Mungu ndiye aliye chanzo cha baraka zote; sala / maombi yetu yote tunayaelekeza kwake Yeye pekee.

Sasa basi; katika Injili ya Luka11:1 tumeona mwanafunzi wa Yesu akimwomba awafundishe kusali; hebu tazama jinsi Yesu anavyowaambia: “…ninyi salini hivi…” (Mt 6:9), “…Msalipo semeni…” (Lk 11:2), “…Baba yetu uliye mbinguni…” (Mt 6:9; Lk 11:2). Yesu anawaambia sala zao wazielekeze / wazipeleke kwa “…Baba yetu…” (Mungu) aliye mbinguni, na wala si mwingine. Na vile vile Yesu anazidi kutufafanulia kwamba:

“Nanyi mkiomba lo lote kwa jina Langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana.” - Yn 14:13

Tunapaswa kumwomba Mungu kupitia Yesu Kristo (kwa jina la Yesu). Hapo anayetenda ni Yesu ndio maana amesema: “…hilo nitalifanya…” lakini anayetukuzwa ni Mungu Baba. Hapo zingatia point hii: Hatumwombi Yesu ila tunamwomba Mungu Baba kwa jina la Yesu (yaani kupitia Yesu kunapokea kutoka kwa Mungu Baba).
Ndio maana katika Wakolosai 3:17 Biblia inasema:

“Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa Yeye.” - Kol 3:17

Kwa jina la Yesu vipofu wanaona, viwete wanatembea, wafu wanafufuliwa, viziwi wanasikia, na wokovu tumeupata: Lakini shukrani zetu tunazipeleka kwa Mungu Baba kwa majibu ya sala zetu anayotupatia kupitia Yesu Kristo. Nadhani hadi hapo imeeleweka vema.
Hebu sasa tujifunze; ni kwa nini maombi yako yanaweza yasijibiwe?

Kuna mambo matatu yanayofanya maombi yako yasijibiwe:

1. Dhambi (maisha ya dhambi).
2. Kuomba vibaya.
3. Kutokuwa na imani.

1. DHAMBI (MAISHA YA DHAMBI).
Dhambi ndiyo inawatafuna wengi sana kuliko hivyo vingine viwili nilivyovitaja hapo juu. Biblia inasema kwamba:

“Kila atendaye dhambi, afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi.” – 1 Yn 3:4

Tukisoma 2 Kor 6:14 Biblia inasema hakuna urafiki kati ya haki na uasi. Ikiwa kama Mungu anatuambia sisi tusifungamane na waovu kwa namna isiyo sawa sawa; je, si zaidi ya hivyo kwa Mungu? Huwezi kupokea majibu ya maombi yako bila kufanya toba. Kabla ya kuingia kwenye maombi ni lazima kwanza wewe ujitakase (fanya toba ya kweli); na ili Mungu akusamehe nawe pia unapaswa kuwasamehe waliokukosea. Biblia inasema,

Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi.” – Kol 3:12-13

tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.” – Efe 4:32

“Jilindeni; kama ndugu yako akikosa, mwonye; akitubu msamehe. Na kama akikukosa mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba, akisema, Nimetubu, msamehe.” – Lk 17:3,4

“Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu. Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu. Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.” – Mk 11:24-26

Kuna umuhimu mkubwa sana kusamehe na kufanya toba ndipo uingie katika maombi; Ndio maana katika Waebrania 12:14, Biblia inasema:

“Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao.” – Ebr 12:14

Utakatifu unatangulia ndipo utapokea haja ya moyo wako. Hata uwe na imani kubwa namna gani, usipojitakasa hayo maombi yako ni sawa na kuupaka rangi upepo. Fanya toba; jinyeyekeze mbele za Mungu kwa toba ya kweli. Usijihesabie haki maana inawezekana umemkosea Mungu bila kujua. Kutenda dhambi sio lazima kuzini tu! Sin means to miss the mark! (kutofanya kwa kiwango ulichopaswa kutenda), na huo ndio uasi kwa maana haujatenda kama jinsi unavyopaswa kutenda.

2. KUOMBA VIBAYA.
Hapa kuna shida kubwa sana; watu hawa naona wapo katika makundi mawili:

i. Wanaoomba kwa tamaa zao na anasa (sio kwa utukufu wa Mungu). Biblia inasema kwamba:

Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu.”  - Yakobo 4:3

ii. Wasiojua nani wamwombe (wanaomba ovyo ovyo tu).
Hapo awali tumejifunza Yesu anasema tumuombe "Baba" katika jina Lake Yesu, hilo atafanya (Yohana 14:13); kwa maana nyepesi ni kwamba usipomwomba Mungu Baba kwa jina la Yesu hilo halifanyi, unakuwa unapoteza muda tu, na hata ukijibiwa unapokea kutoka kwa Shetani. Kuna watu wamefundishwa vibaya; utona wapo watu wanamwomba Mungu kupitia Maria, Yosefu n.k. hayo mapokeo yakijinga inabidi watu wajiepushe nayo. Tunapaswa kumwomba Mungu Baba kwa jina la Yesu, sio namna nyingine yoyote ile.

3. KUTOKUWA NA IMANI.
Unapoomba amini tayari umepokea hata kama unaona katika ulimwengu wa mwili hali bado haijabadilika. Biblia inasema,

“…imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana.” – Ebr 11:1

Kuamini hakusubiri matokeo mwilini; bali katika roho tayari umepokea alafu matokeo ya mwilini yatafuata. Bwana Yesu anasema,

“…Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.” – Mk 11:24

Napenda kuhitimisha somo hili kwa mfano ufuatao, Biblia inasema kwamba:

“Hata asubuhi yake walipotoka Bethania aliona njaa. Akaona kwa mbali mtini wenye majani, akaenda ili labda aone kitu juu yake; na alipoufikilia hakuona kitu ila majani; maana si wakati wa tini. Akajibu, akauambia, Tangu leo hata milele mtu asile matunda kwako. Wanafunzi wake wakasikia…
Na asubuhi walipokuwa wakipita, waliuona ule mtini umenyauka toka shinani. Petro akakumbuka habari yake, akamwambia, Rabi, tazama, mtini ulioulaani umenyauka. Yesu akajibu, akamwambia, Mwaminini Mungu. Amin, nawaambia, Ye yote atakayeuambia mlima huu, Ng'oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake. Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.”  - Mk 11:12-14,20-24

Kuna mambo ya muhimu sana kujifunza katika habari hiyo: 1. Yesu aliona njaa. 2. Wakati huo haukuwa msimu wa tini lakini Yesu alitaka apate tini kutoka kwenye huo mtini. Mambo hayo mawili ni mfano halisia wa maisha yetu: Wapo watu wenye njaa (shida / uhitaji), na katika maisha yao wapo katika wakati ambao dunia dunia nzima inasema hali ni ngumu, uchumi ni mgumu, ugonjwa huo hauna tiba; wanajaribu namna mbalimbali ya kujinasua lakini hawaoni matokeo. Hali hiyo ni sawa na jinsi Yesu alivyokuwa na njaa lakini alitaka ale tini wakati ambao sio msimu wa matunda hayo. Sijui kama hapo umenielewa vema.
Yesu aliulaani mtini kisha akaondoka zake, siku ya pili yake waliporudi walikuta ule mtini umekauka. Kuna jambo la kujifunza hapa: mti ule ulikauka pale punde tu alipotamka japokuwa kwa macho ya nyama ulionesha bado haujakauka! Matokeo huanzia katika ulimwengu wa roho alafu ndipo jibu linadhihirika katika ulimwengu wa mwili. Hivyo ndivyo tunapaswa kuwa na imani. Mtu wa haki ukitamka tu tayari papo hapo imetimia, usipoteze muda kusubiri matokeo katika ulimwengu wa mwili.

Bila shaka somo hili limefanyika baraka kwako. Nakutakia baraka tele, Mungu Mwenyezi akubariki katika jina la Yesu Kristo. Amen.

Thursday, January 11, 2018

JIONESHE KUWA MWANAMUME


 JIONESHE KUWA MWANAMUME (1 Wafalme 2:1)

Bwana Yesu Kristo apewe sifa. Ninamshukuru Mungu kwa neema Yake kuu amenipatia kibali cha kulihudumia kanisa Lake hata sasa. Leo ninao ujumbe wenye baraka kwako uliobeba kichwa kinachoitwa: JIONESHE KUWA MWANAMUME. Huu ni mwanzoni mwa mwaka 2018, watu wengi wanatazamia baraka nyingi ziambatane nao; hivyo basi, Roho wa Mungu amenipa ujumbe huu kwa ajili yako: “JIONESHE KUWA MWANAMUME”.
Hebu tufungue Biblia zetu tusome 1 Wafalme 2:1-2, Biblia Takatifu inasema:

Basi siku ya kufa kwake Daudi ikakaribia, akamwusia Sulemani mwanawe, akasema, Mimi naenda njia ya ulimwengu wote (yaani, naenda kufa); basi uwe hodari, ujioneshe kuwa mwanamume…” ~ 1 Wafalme 2:1-2

Mfalme Daudi anamwambia Sulemani mwanawe: “…ujioneshe kuwa mwanamume…” (“…show thyself a man…” - KJV)

Je, nini basi maana ya “…kuwa mwanamume…”? Mwanamue ni mtu asiye ogopa, mtu jasiri mwenye kufanya mambo magumu na shujaa. Kuwa mwanamume sio kijinsia bali ni kuwa jasiri na hodari. Mfalme Daudi alitambua dhahili shujaa ndiye anayetawala wala si mtu mlegevu; hapo alimtaka Sulemani mwanawe awe mtu hodari na jasiri ili aweze kuhimili misukosuko ya utawala unaomkabili. Mfalme Daudi sio tu alimtaka Sulemani mwanawe awe hodari, bali pia AJIONESHE YEYE NI HODARI; yaani watu wamwone na wamtambue yeye ni hodari. Hivyo ndivyo Mungu anavyotaka sisi tuwe hadi ulimwengu utambue uwepo wetu (Luka 10:19).

Watu wengi huwa wanatamani sana kuinuliwa, lakini je umejiandaa kuzikabili changamoto zinazoambatana na baraka hizo? Mara zote unapobarikiwa na kuinuliwa kwa viwango vya juu kunaambatana na kundi la maadui linalokupinga kimwili na kiroho; mf. kuna majambazi, pepo wachafu, wachawi, wasengenyaji na wengine watakuchukia tu kwa sababu wewe umeinuliwa juu kuliko wao. Ndio maana neno la kwanza tumeona Sulemani ameambiwa “…uwe hodari…” (1 Fal 2:2; 1 Nya 28:10, 20) Mtu hodani ni yule mwenye uwezo wa kufanya jambo lililowashinda wengine, mtu mahiri na stadi; anayewaongoza watu kwenda pale wanapopaswa kwenda wala si pale wanapotaka kwenda.

Ukitaka kuvifikia viwango vya juu vya Baraka ni lazima uchague kufanya mambo magumu kwa wengine, usichague mambo mepesi mepesi; bali yafanye mambo magumu kwa umahiri na ustadi mkubwa. Uwe hodari katika kila ufanyalo; iwe katika biashara yako, masomo yako, familia yako, ndoa yako, kazi zako na katika kila utendalo.

Sasa hivi tumeshaingia katika mwaka mpya ambao wengi wanatazamia kuinuliwa zaidi ya mwaka uliopita; Lakini tambua kuwa mwaka mpya ni badiliko la kalenda tu, bali kutamalaki hakupo kwa watu walegevu wala wavivu, ila ni kwa watu walio hodari. Lazima ujioneshe kuwa mwanamume.
Biblia inasema:

Atendaye mambo kwa mkono mlegevu huwa maskini; Bali mkono wake aliye na bidii hutajirisha.– Mithali 10:4

Utofauti kati ya fukara na tajiri upo katika namna yake ya kufikiri na jinsi anavyotenda mambo; ni hivyo tu. Utajiri / kufanikiwa ni uchaguzi wako, hata ufukara / kushindwa pia ni uchaguzi wako pia. Huwezi kukwea ngazi ya kamba iliyoning’inia huku ukiwa umeweka mikono mfukoni mwa suluali yako! Ni lazima ushikilie vizuri ndipo utaweza kuikwea.

Hata mafanikio ya mtu hayaji kizembe, ni lazima uchague kufanya mambo magumu, makubwa yanayowashinda wavivu. Uwe na ndoto kubwa, heshimu malengo yako, uwe jasiri, thubutu kutenda bila woga, fanya kile chenye faida, tunza wakati, epuka marafiki wabaya, uwe na nidhamu ya pesa, weka akiba katika vitu vinavyoongezeka thamani na umtangulize Mungu katika kila ufanyalo. Wakati sahihi wa kufanikiwa ni sasa; anza na hicho ulichonacho: kama ni wazo basi washirikishe watu sahihi, na kama ni mtaji kidogo anza nao uo huo huku ukiwa na mipango ya kufika juu zaidi.

Vile vile tambua kwamba, hauwezi kufanikiwa kwa akili zako mwenyewe tu; ndio maana mfalme Daudi anaendelea kumwambia Sulemani mwanawe, kwamba:

“…uyashike mausia ya BWANA, Mungu wako, uende katika njia Zake, uzishike sheria Zake, na amri Zake, na hukumu Zake, na shuhuda Zake …upate kufanikiwa katika kila ufanyalo, na kila utazamako.” 1 Wafalme 2:3-4

Mweke Mungu mbele ya kila jambo; Ndio maana sisi tunaambiwa: “Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa Yeye. “ – (Wakolosai 3:17). Ukimtumainia Mungu katika yote, hapo ndipo kila utazamako (unachokihitaji) kinakuwa chako. Katika kuomba kwako usiombe kwa tamaa zako, bali kwa ajili ya utukufu wa Mungu (Yakobo 4:3). Lazima Mungu awe na sehemu katika mipango yako, na zingatia kumtolea Mungu sadaka ya shukurani katika mapato yako; si kwa kulazimishwa, bali kwa moyo mkunjufu wa shukurani sawa sawa na jinsi Mungu alivyokubariki. Endapo kama umemuwekea Mungu nadhiri, hakikisha unakuwa mwaminifu katika kuitimiza kwa uhaminifu wote (Hesabu 30:2; Kumb 23:21).
Uwe hodari katika kila lililo jema wala si katika uovu (Zaburi 64:5), ndio maana Biblia inasema:

“…Heri mtu yule amchaye BWANA, Apendezwaye sana na maagizo Yake. Wazao wake watakuwa hodari duniani; Kizazi cha wenye adili kitabarikiwa.” – Zaburi 112:1-2

Hapo zingatia neno hili: “Kizazi cha wenye adili kitabarikiwa.” Hicho ni kizazi kinachomtii Mungu ndicho kinachobarikiwa. Baraka za mcha Mungu hodari zitaambatana naye pamoja na kizazi chake. Sisi Wakristo, tayari Mungu ametubariki wala hakuna laana yoyote ile inayotuandama (1 Petro 2:9). Japokuwa tayari Mungu amekubariki, kama jinsi tunavyosoma katika Kumb 28:2-6

…baraka hizi zote zitakujilia na kukupata usikiapo sauti ya BWANA, Mungu wako. Utabarikiwa mjini, utabarikiwa na mashambani. Utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, na uzao wa wanyama wako wa mifugo, maongeo ya ng'ombe wako, na wadogo wa kondoo zako. Litabarikiwa kapu lako, na chombo chako cha kukandia unga. Utabarikiwa uingiapo, utabarikiwa na utokapo. – Kumb 28:2-6

Lakini baraka hizi utazipata pale USIPOKATA TAMAA. Hakuna mafanikio mepesi, ni lazima kuwa hodari kweli kweli; lazima ujioneshe kuwa mwanamume kweli kweli. Hebu tusome habari hii itakusaidia kukufungua ufahamu wako; katika Mwanzo 26:17-22 Biblia inasema:

Basi Isaka akatoka huko akapiga kambi katika Bonde la Gerari, akakaa huko. Isaka akarudi akavichimbua vile visima vya maji walivyovichimba siku za Abrahamu babaye, maana wale Wafilisti walikuwa wamevifukia baada ya kufa kwake Abrahamu. Naye akaviita majina kufuata majina alivyoviita babaye. Pia watumishi wa Isaka wakachimba katika lile bonde, nao wakapata kisima cha maji yanayobubujika.
Bali wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka, wakisema, “Maji haya ni yetu.” Ndipo akakiita jina la kile kisima Eseki, kwa sababu waligombana naye. Nao wakachimba kisima kingine, wakagombania na hicho tena. Basi akakiita jina lake Sitna. Akaondoka huko na akachimba kisima kingine, wala hicho hawakukigombania. Basi akakiita jina lake Rehobothi, kwa maana alisema, “Kwa kuwa sasa BWANA ametufanyia nafasi, nasi tutazidi katika nchi.” – Mwanzo 26:17-22

Hapo tumejifunza Isaka hakupoteza muda kung’ang’ania kushindana na adui zake, bali yeye alitazama fursa kwingine na kuitumia. Siku zote ukitaka kufika viwango vya juu vya baraka, usipoteze muda kushindana na mtu mpumbavu, bali tazama fursa zilizopo mbele yako alafu piga hatua kuzifuata. Usifanye jambo lisilo na faida kwako, usiupoteze bure wakati wako. Usiishie kulaumu tu, bali tazama fursa zilipo na ujichanganye huko. Baraka za Mungu zinaambata na mtu yule aliyechukua hatua kuzifuata; wala sio kwa kusali tu, wala kwa kufunga na kuomba tu: bali kwa matendo pia. Huwezi kuzifikia baraka zako kwa kuishia kusema “amina” kanisani wala kwa kupewa mafuta ya upako; bali unapaswa utambue tayari Mungu amekwisha kubariki ila kilichobaki ni wewe kuzifuata hizo baraka zako. Hapo ni sawa na mzazi aliyekuwekea chakula ndani, ila wewe umebakiza jukumu lako la kuinuka na kukila pindi unapokihitaji. Tazama wapi fursa zilipo, nawe nenda huko kazifuate ndipo utaifikia baraka yako.

Jambo la mwisho la kuzingatia ninalopenda kukwambia; Tenda mambo kwa busara bila kumdharau mtu awaye yote. Biblia Takatifu inatuambia kwamba:

 “Tazama, Mungu ni hodari, wala hamdharau mtu ye yote; Ana uweza katika nguvu za fahamu.” – Ayubu 36:5

Mungu Mwenyewe ni hodari (yaani, anatenda mambo yanayowashinda wengine) lakini hamdharau mtu ye yote. Hizi mali na utajiri tunaoupata vyote vinatoka Kwake, ni kwa neema Zake tu; hatukuja na kitu duniani na wala hatutaondoka na kitu duniani; hivyo basi tuwahehimu na kuwapenda watu wote, na hata kuwaombea watu walio adui zetu (Luka 6:35; Warumi 12:20).
Tukisoma katika Mithali 17:2 tunaona Biblia inasema:

“Mtumwa atendaye kwa busara atamtawala mwana atendaye mambo ya aibu; Tena atapata sehemu ya urithi kati ya ndugu.” – Mithali 17:2

Zingatia point hii: hapo (Mithali 17:2) imetumia neno "Mtumwa...", kwa kumaanisha "mtu mwovu" (yule asiyemtii wala kumwabudu Mungu wa kweli) akitenda mambo kwa busara ndipo atamtawala "...mwana..."  atendaye mambo ya aibu (mtu wa Mungu aliyekengeuka au afanyaye mambo kivivu).  Kwa hiyo; hapo neno "mtumwa" linamwakilisha "mtu mwovu", na neno "mwana" linamwakilisha "mtu wa Mungu". Hapa ndipo utaweza kuwaona baadhi watu waovu wanafanikiwa na kustawi maishani kuliko wacha Mungu walio wavivu; ndiyo maana hapo Biblia inamalizia kwa kusema kuhusu huyo mtumwa: "..Tena atapata sehemu ya urithi kati ya ndugu.” – (Mithali 17:2) Yaani atamiliki ile sehemu uliyopaswa wewe kuipokea.

Mafanikio au kushindwa vyote vipo katika uchaguzi wako; ikiwa unahitaji kufanikiwa, basi tenda mambo yote kwa busara, hekima na uwe hodari. Hakuna mafanikio yanayokuja kizembe; ni lazima ujioneshe kuwa mwanamume (sio kijinsia, ila katika “attitude” yako – namna yako ya kufikiri na kutenda kama mwana wa mfalme).


Jina langu naitwa Masanja Sabbi (masanjasabbi@gmail.com), nakutakia kheri na baraka tele katika kila utendalo. Malaika wa Mungu akutangulie na kukufanikisha katika jina la Yesu Kristo. Amen.

Wednesday, April 19, 2017

THAWABU YANGU NI NINI?


NAWAKUMBUSHA TU WATUMISHI WA MUNGU

"Basi thawabu yangu ni nini? Ni hii, ya kuwa nihubiripo, nitaitoa Injili bila gharama..." - 1 Kor 9:18

Inawezekana andiko hili huwa unalipita au haujawahi kulisoma; lakini leo napenda kukukumbusha mtu wa Mungu, kabla ya kuingia kwenye huduma, ni vema ukazingatia andiko hili.

Mbarikiwe sana watu wa Mungu.

Tuesday, April 18, 2017

UFUFUKO WA YESU


Je, Ufufuko wa Yesu ndio sikukuu ya Pasaka?
Je, Pasaka na “Easter” ni kitu kimoja?


Maswali hayo huwatatiza watu wengi sana, hivyo basi leo nimependa tujifunze ili tuondokane na utata huo; barikiwa sana na somo hili:

PASAKA
Sikukuu ya Pasaka ilikuwa mpango wa Mungu kwa Waisraeli ili washerehekee kuokolewa kwao kutoka utumwani Misri kwa njia ya miujiza (Kut 12:14,24).

Jina la sikukuu lilikumbusha tendo la malaika wa Mungu “kupita juu” ya nyumba za Waisraeli alipowauwa wazaliwa wa kwanza wa Wamisri (Kut 12:27). Lakini Mungu alihifadhi nyumba za Waisraeli wasipatwe na hukumu ile alipoona damu ya mnyama wa sadaka iliyopakwa kuzunguka mlango mkubwa wa mbele wa nyumba zao. Damu hiyo ilikuwa ishara kwamba uzima usiokuwa na hatia ulitolewa badala ya mtu aliekuwa chini ya hukumu (Kut 12:5,7,12-13,21-23).

Mwezi wa Pasaka uliwekwa kuwa mwezi wa kwanza wa mwaka wa kalenda ya Kiyahudi (Abibu / Nisani ambao ni mwezi March kwenda April katika kalenda ya Gregory).

Baada ya Pasaka, sikukuu ya siku saba ya Mkate Usiotiwa Chachu iliunganishwa na sherehe ya Pasaka; mambo hayo miwili hasa yalihesabiwa kama sikukuu moja (Kum 16:1-8; Mk 14:1). Baada ya kuondoa chachu kutoka nyumba zao kabla ya Pasaka, watu walitunza nyumba zao zisiwe na chachu yo yote kwa juma lingine baada ya Pasaka (Kut 12:14-20). Jambo hili liliwakumbusha kwamba, baada ya kuokolewa kwa njia ya Pasaka, walikimbia kutoka Misri kwa haraka, wakipika mikate isiyochachwa hapo waliposafiri (Kut 12:33-34,39).

Waisraeli walipofika Kanaani, walipaswa kuadhimisha sikukuu ya Pasaka katika mahali maalumu pa ibada tu. Mwanzoni mahali hapo palikuwa Hema la Kukutania, na baadaye palikuwa helalu (Kum 16:5-6; Yos 5:10-12; 2Nya 8:12-13; 30:1; 35:1; Lk 2:41; Yn 2:13; 11:55). Wanaume wote wa Israeli waliokuwa watu wazima walipaswa kuhudhuria sherehe ya Pasaka (Kut 23:14,17), na hata wageni waliweza kusherehekea, mradi tu walipata tohara na hivyo walikuwa sehemu ya watu wa Agano (Kut 12:43-49).

PASAKA KATIKA AGANO JIPYA
Wakati wa Bwana Yesu, sikukuu ya Pasaka ilikuwa kanuni maalumu pamoja na sherehe kadhaa zilizokuwa zimeongezeka. Ingawa watu walichinja mwana-kondoo hekaluni walikula karamu yake binafsi pamoja na marafiki na jamaa (Lk 22:8-13). Kati ya nyongeza zile za karamu kulikuwa na kikombe cha divai ambacho ni kwa ajili yake mkuu wa nyumba alisema sala ya shukrani (au ya baraka, 1 Kor 10:16), ambacho pia alikizungusha kwa wote walioshiriki, kabla ya kula mkate usiochachwa na baada yake pia (Mk 14:22-24; Lk 22:15-20).
Kuimba pia kulikuwa sehemu ya sherehe, washiriki wakiimba nyimbo mbalimbali za Zaburi zilizojulikana kwa “Zaburi za Hallel” (yaani za Haleluya - za kumsifu BWANA, ambazo ni Zaburi 113-118). Kwa kawaida waliimba Zaburi mbili za kwanza kabla ya kula mwana-kondoo na Zaburi nyingine baadaye (Mk 14:26).

Katika Pasaka ya mwisho ya Bwana Yesu, Yeye na wanafunzi Wake walikula karamu siku moja kabla ya wakati wake hasa, na labda pasipo mwana-kondoo (Lk 22:15; Yn 13:1). Inawezekana walifanya hivyo kwa kuwa Yesu alikwisha jua kwamba Yeye mwenyewe wakati huo alikuwa mwana-kondoo wa Pasaka; siku ya kesho yake angetoa maisha Yake wakati ule ule ambao wanyama wangechinjwa kwa maandalizi ya karamu iliyofuata usiku huo (Yn 18:28; 19:14,31,42).

Kifo cha Yesu msalabani kilikuwa tendo kuu la ukombozi ambalo Pasaka ya Waisraeli ilikuwa mfano wake mdogo tu (linganisha Kut 12:5 na 1 Pet 1:18-19, pia Kut 12:46 na Yn 19:36, pia Kut 12:21,27 na 1 Kor 5:7). Baada ya kufa kwake Yesu, Pasaka ya Wayahudi haikuwa na maana tena; iliondolewa na mahali pake sherehe mpya ya ukumbusho iliwekwa, yaani Chakula cha Bwana (Mt 26:17-30; 1 Kor 10:16; 11:23-26).
Hata hivyo, Agano Jipya linataja mahitaji ya Pasaka katika mafundisho ya Kikristo; kwa maana jinsi sikukuu ya Pasaka ilivyokuwa na maana kwamba Waisraeli walipaswa kutoa "chachu" katika nyumba zao, vivyo hivyo sadaka ya Yesu Kristo ina maana kwamba Wakristo wanapaswa kuondoa "dhambi" katika maisha yao (1 Kor 5:7-8).

Je, EASTER ndiyo PASAKA?
Neno “Easter” halipo katika Biblia yo yote ile (ya Kiebrania – Agano la Kale, wala ya Kiyunani – Agano Jipya). Katika maandiko yote ndani ya Biblia Takatifu hakuna sherehe ya “Easter” kwa watu wa Mungu. Tafasiri ya neno “Easter” tunaziona kwenye kamusi mbalimbali zikifafanua kuwa; ni sherehe za Kikristo kuadhimisha ufufuko wa Yesu.
Hebu tutazame nukuu zifuatazo:

"Easter
· n. the festival of the Christian Church celebrating the resurrection of Christ, held (in the Western Church) on the first Sunday after the first full moon following the northern spring equinox.
– ORIGIN OE Uastre, of Gmc origin and rel. to east; perh. from Éastre, the name of a goddess assoc. with spring." –
Oxford Dictionary 10th Edition;

"Easter, annual festival commemorating the Resurrection of Jesus Christ, and the principal feast of the Christian year... a Christian festival, embodies many pre-Christian traditions. The origin of its name is unknown. Scholars, however, accepting the derivation proposed by the 8th-century English scholar St Bede, believe it probably comes from “Ä’ostre”, the Anglo-Saxon name of a Teutonic goddess of spring and fertility, to whom was dedicated a month corresponding to April. Her festival was celebrated on the day of the vernal equinox; traditions associated with the festival survive in the Easter rabbit, a symbol of fertility, and in coloured Easter eggs, originally painted with bright colours to represent the sunlight of spring, and used in Easter-egg-rolling contests or given as gifts." -
Microsoft ® Encarta ® Encyclopedia 2005.

Neno “Easter” asili yake ni neno “Ä’ostre” ambalo ni jina la mungu “mke” wa mavuno na uzazi aliyekuwa akiabudiwa (amewekewa wakfu) majira ya kuchipua mimea hususani kipindi cha mwezi April, ambayo pia ndiyo mwezi Nisani kwa Wayahudi ambao waliadhimisha Pasaka.

Sherehe ya “Eostre / Easter” iliambatana na mambo ya kimila; walitoa sadaka ya sungura kama alama ya uzazi, na mayai yaliyopakwa rangi ya mng’ao ili kuwakilisha “jua” ambayo yalitumika katika mashindano ya kupondana mayai, au kutolewa tu kama zawadi.
Sherehe hizo zilitokana na dini ya kale ya Kigiriki, walikuwa na desturi ya kuadhimisha kurudi kwa Persephone binti wa Demeter / Ä’ostre “mungu wa mavuno” kutoka kuzimu kuja duniani kwenye mwanga wa mchana (return of Persephone, daughter of Demeter, goddess of the earth, from the underworld to the light of day); kurudi kwake “Persephone” kwa Wagiriki wa kale walitafasiri ni ufufuo wa maisha katika kuchipua mimea kipindi cha mwezi April baada ya kuharibiwa na majira ya baridi kali huko kwao. Watu hao waliamani kuwa “mungu” wao mwenye nguvu zote alikwenda kulala wakati wa msimu wa baridi, nao wakafanya sherehe na kucheza muziki katika majira ya kuchipua kwa mimea wakiamini “mungu” wao ameamka toka usingizini, amerudi toka kuzimu.

Lakini, katika Biblia ya lugha ya Kiingereza neno Pasaka limeandikwa: “Passover” likimaanisha “PITA-JUU” kama jinsi tulivyojifunza katika Kut 12:27, malaika wa Mungu alipoziacha nyumba za wana wa Israel kwa kupita juu na kuwaangamiza wazaliwa wa kwanza wa Wamisri.

Sherehe hizo za “Easter” zimeingia kwenye baadhi ya dini za Kikristo kutokana na mapokeo kutoka dini ya kipagani ya Wagiriki wa kale.

Tukirejea katika Biblia; hakuna sherehe za “Easter”, wala Pasaka sio “Easter”. Sherehe hizo za kipagani “Easter” ziliadhimishwa katika majira sambamba na sherehe za Pasaka ya Kiyahudi (mwezi Nisani / April) ambayo pia ndiyo majira Yesu alisulibiwa, kufa na kufufuka.

Mapokeo hayo ya “Easter” ndiyo yameingizwa hata leo katika sherehe za kidini ingawa kiukweli huo ni upagani uliofunikwa mwamvuli wa Ukristo.

Easter sio Ufufuko wa Yesu, wala Easter sio Pasaka ya Kiyahudi.

Ninaamini ujumbe huu umewafungua fahamu watu wengi; nami nakuombea uzidi kubarikiwa katika jina la Yesu Kristo, Amen.

Thursday, April 30, 2015

SIYO MAPENZI YA MUNGU WEWE UTESEKE!


Neno la Mungu linasema hivi:

"Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini Mimi sitakusahau wewe.
Tazama, nimekuchora katika vitanga vya mikono Yangu; kuta zako ziko mbele Zangu daima." - Isaya 49:15-16

Mwanadamu anaweza kukutenga, anaweza kukunyanyasa, anaweza kukufanyia mabaya; lakini USIKATE TAMAA. Haijarishi unapitia magumu kiasi gani: iwe katika ndoa yako, iwe katika biashara yako, iwe katika uchumba wako, iwe katika afya yako, iwe katika uchumi wako, iwe katika jamii yako, iwe katika masomo yako; USIKATE TAMAA, Jibu lipo, na ipo njia ya kutokea. Mwamini Yesu TAYARI amekushindia.

Hayo magumu unayapata ili imani yako izidi kukua hata Shetani apate kuaibika kwamba tayari ameshindwa tangu pale msalabani Yesu aliposema IMEKWISHA.

Pokea jibu la mahitaji yako sasa katika jina la Yesu Kristo. Amen.

Thursday, February 26, 2015

UNALINDWA NA NGUVU ZA MUNGU KWA NJIA YA IMANI; HAUNA SABABU YA KUMWOGOPA SHETANI WALA KAZI ZAKE ZOTE!

Biblia Takatifu inasema kwamba:

"Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu; tupate na urithi usioharibika, usio na uchafu, usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu. Nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani hata mpate wokovu ulio tayari kufunuliwa wakati wa mwisho." - 1 Petro 1:3-5

Wakati umefika Mkristo kuyatambua mamlaka uliyopewa na Mungu Baba. Biblia inasema: Mungu Baba (JEHOVA / YAHWEH) ametuzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye UZIMA kupitia ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Hapa zingatia sana: Tumaini hilo la UZIMA tunalipata kupitia UFUFUKO wa Yesu Kristo; hatulipati tu kupitia Yesu, bali tunalipata kupitia UFUFUKO wa Yesu Kristo. Lazima uelewe kuwa UFUFUKO wa Yesu Kristo ndio umekamilisha uzima wetu.

Hapa siongelei habari za udini, maana kuna watu wa dini ambao Yesu wao bado amekufa / yupo kaburini!
Hapa siongelei habari za Yesu wa kwenye Qur'an; Injili ni kulitangaza neno la Mungu bila unafiki wala kufichana: Issa bin Maryamu bado amekufa! Lakini Yesu Kristo Mwana wa YAHWEH yupo hai. Issa bin Maryamu alikuja kumtangaza ALLAH, lakini Yesu Kristo alikuja kutimiza mapenzi ya Baba Yake wa mbinguni anayeitwa YEHOVA. Wakristo mwe na akili; huo upuuzi wa kukubali Issa bin Maryamu unawafanya kuwaondolea mamlaka mliyowekewa na Mungu Baba ndani yenu.

Biblia inasema: KUFUFUKA kwa Yesu kunatupatia TUMAINI LA UZIMA. Sisi ni uzao mteule wa Mungu; sisi ni milki ya Mungu; YEHOVA ametuzaa mara ya pili na kutufanya sisi kuwa milki Yake. Hakuna pepo mchafu wala mchawi mwenye mamlaka juu yako ikiwa wewe umemkabidhi Yesu awe Bwana na Mwokozi wa maisha yako. WEWE UNALINDWA NA NGUVU ZA MUNGU KWA NJIA YA IMANI.

Hatulindwi na nguvu za Mungu kwa kuvaa rozari, wala hirizi! Huo ni utapeli tu wa kidini. Neno IMANI ni kutenda pasipo kutumia vielelezo. Nguvu za Mungu hazimo katika maji, wala vitambaa, wala sanamu, wala mafuta; bali nguvu hizo zimo ndani yetu kwa sababu sisi ni hekalu la Mungu, Roho Mtakatifu ameweka makao Yake ndani yetu, nasi tunashinda zaidi ya kushinda.

Mkristo anayejitambua haogopi wachawi wala hila za Shetani. Mkristo anayejitambua hutumia mamlaka ya jina la Yesu kwa kuharibu kila kazi za Shetani. Sisi tunaye Mungu ndani yetu; tunapokutana na upinzani wa Shetani huo huwa sio muda wa kuomba bali ni muda ya kukemea katika jina la Yesu Kristo. Mtu aliyeokoka anatambua yeye ni nani katika ulimwengu huu. SISI TUNALINDWA NA NGUVU ZA MUNGU KWA NJIA YA IMANI.

Neema hiyo ipo kwa wale tu waliomkabidhi Yesu awe Bwana na Mwokozi wa maisha yao. Kama wewe bado haujamkabidhi Yesu maisha yako; basi sali sala hii fupi:

"Mungu Baba, asante kwa wokovu ulionipatia kupitia Yesu Kristo. Ninakiri pasipo msaada wako mimi nimeangamia; sasa ninayakabidhi maisha yangu Kwako, nitakase dhambi zangu kwa damu ya Yesu Kristo; tawala maisha yangu tangu sasa, niongoze katika mapenzi Yako, nifanye niwe jinsi Wewe utakavyo niwe kwa ajili ya utukufu Wako. Ninaomba Roho Wako Mtakatifu aniongoze tangu sasa hata milele. Asante kwa kunifanya kiumbe kipya katika jina la Yesu Kristo. Amen"

Amini tayari umekuwa kiumbe kipya, amini tayari umesamehewe dhambi; lakini umebakiwa na kitu kimoja tu! Ambatana na watu (Kanisa) wanaohubiri Injili ya kweli (wokovu) ili uweze kukua katika imani.

Nakutakia baraka tele katika jina la Yesu Kristo. Amen.

Thursday, January 8, 2015

CHUKIA UMASIKINI, LAKINI WAPENDE MASIKINI. WAELIMISHE NA UWASAIDIE.

CHUKIA UMASIKINI, LAKINI WAPENDE MASIKINI. WAELIMISHE NA UWASAIDIE.

Kwa mujibu wa maono niliyonayo:

UMASIKINI maana yake ni hali ya kukosa maarifa pamoja na kuwa na fikra / mtazamo mbovu akilini mwako! (POVERTY simply means; Lack of knowledge and having bad attitude! The state of having negative mentality).

Umasikini sio hali ya mtu kuwa na kipato chini ya dola moja, wala sio hali ya mtu kukosa mahitaji aliyonayo. Hiyo ni tafasiri mbovu ambayo watu wengi wamefundishwa na kuiweka akilini mwao. Hayo ni matikeo ya umasikini lakini sio maana halisi ya umasikini. Narudia tena:

UMASIKINI ni hali ya kukosa maarifa pamoja na kuwa na fikra / mtazamo mbovu akilini mwako! (POVERTY simply means; Lack of knowledge and having bad attitude! The state of having negative mentality).

Watu wengi ni masikini kwa sababu wanayo BIDII KUBWA katika kuwa masikini! Wanayachukia maarifa; hawapendi kushughulisha akili zao; wanapenda kuomba omba!
Kuna wajinga wengi wanaodhani kuwekewa mikono na mchungaji ndipo watakuwa matajiri; wajinga wengine wanaambiwa panda mbegu utapata dabo dabo! Baraka za Mungu hazipo namna hiyo; bali baraka za Mungu utazipata pale unapokuwa na afya akilini mwako. Kitu cha kwanza unachopaswa kuchughulika nacho ni akili yako; uwe na fikra / mtazamo mzuri akilini mwako. Sikukatazi kutoa changizo kanisani mwako; lakini unatakiwa kuelewa kuwa Mungu leo hanashida ya kukubariki kwa sababu tayari amekwisha kukubariki; Lakini leo Mungu anahitaji uponyaji ufanyike katika akili zako ili neno Lake likae kwa wingi ndani yako na ndipo uweze kuziona, kuzifata, na kuzitumia baraka ambazo tayari amekubariki.

Ninaongea kwa maneno mmakali lakini ninaamini yanaleta uponyaji katika akili yako. Hakuna utajiri utakaoupata endapo kama hautapata uponyaji katika akili yako; uponyaji huo ni kupata maarifa. Soma vitabu sahihi, jifunze katika mitandao sahihi, sikiliza nyimbo sahihi, tazama vitu sahihi, na ujifunze kwa watu waliofanikiwa; Badiri fikra zako.

Penda maarifa.
Watu wengi wanatamani mabadiriko lakini wao wenyewe hawataki kubadirika! Haiwezekani kukokotoa hesabu kwa kanuni iliyoshindwa! Vivyo hivyo hauwezi kupata matokeo tofauti kwa kutumia mbinu ile ile iliyoshindwa! Ukifanya hivyo utafanana na mtu mpumbavu.
Mafanikio ya mtu yamo katika fikra na mtazamo wa akili alionao mtu. Mafanikio ya mtu hayapimwi kutokana na vitu aliyonavyo, wala elimu aliyonayo; bali mafanikio ya mtu yanapimwa kutokana na uwezo wake wa kufikiri akilini mwake. Watu wengi akili zao zimekufa japokuwa miili yao inaishi! Wengi wanawaza kusoma sana ili wapate vyeti vitakavyowawezesha kuajiriwa. Ndio, hayo ni mawazo mazuri, lakini sio mawazo mazuri sana. Je, usipopata ajira umejiandaa kufanya nini? Umejiandaa kulaumu serikali au umejiandaa kuwa kibaka! Au umejiandaa kuwa omba omba!

Tumia akili yako vizuri.
Ni kweli wasomi ni wengi, ni kweli ajira ni adimu, ni kweli wengi hawana mitaji; lakini tumia akili yako vizuri. Kile unachoomba watu wakusaidie, ujue nao pia wamekitafuta. Jifunze kutafuta sio kuomba omba. Pesa inakuja pale unapoiwekea mtego, mtego mzuri unatokana na fikra pevu za mtegaji. Tambua kwamba: pesa sio thamani bali ni kipimo cha thamani!

Kuna mambo matatu ambayo ni muhimu kuyazingatia; kwa mtu mwanye fikra pevu hupenda kuwa na mambo yafuatayo:

1. Haki ya kuishi.

2. Haki ya kufanya maamuzi sahihi.

3. Afya bora. [Afya ni pamoja na mwili kutokushambuliwa na maradhi wala magonjwa; Akili kuwa na fikra nzuri; pamoja na uwezo wa kifedha!]

Yote hayo utayapata pale unapokuwa na maarifa. Soma vitabu vizuri, na ujifunze kwa waliofanikiwa. Hebu fikiri zaidi ya hapo awali; badili fikra zako. Usipende kuomba omba; jifunze kuwajibika kwenye maisha yako mwenyewe. Kila mtu anawajibika katika kuyabadili maisha yake yeye mwenyewe; iwe kiroho hata kimwili. Hakuna ajira itakayokufanya uwe tajiri, hakuna serikali itakayokufanya uwe tajiri; Hiyo yote ni mifumo tu! HAKUNA MFUMO ULIOTENGENEZWA ILI UKUFANYE WEWE UWE TAJIRI; kila mfumo umewekwa kumnufaisha zaidi yeye aliyeuweka! Kama wewe akili zako zote zinategemea ajira, au serikali ikuletee utajiri; basi elewa wazi umepata ziro katika mafanikio yako! Hata kama umeajiriwa, hebu waza kuwa na mambo yako mwenyewe. Hebu nikupe siri hii itakusaidia: Dunia ya sasa imetoka katika mfumo wa kuajiriwa, bali imeingia katika mfumo wa Network Marketing! Najua hapo wengi hawajaelewa, narudia tena: Dunia ya sasa imetoka katika mfumo wa kuajiriwa, bali imeingia katika mfumo wa Network Marketing! Narudia tena kwa mara ya tatu ili uelewe vizuri:

Dunia ya sasa imetoka katika mfumo wa kuajiriwa, bali imeingia katika mfumo wa Network Marketing!

Sio nia yangu hasa wakati huu kukufundisha what is Network Marketing or Direct Selling, or Personal Franchise, or Mult Level Marketing Business. Ukitaka kuyajua hayo nitafute kwa muda wako; lakini kama kweli unahitaji kufanikiwa; BADILI MTAZAMO NA FIKRA ZA AKILI YAKO.

Tunahitaji uhamsho katika kanisa; akili zilizokufa tunatakiwa tuzifufue. Hebu juilize; utakuwa omba omba mpaka lini? Nani kakwambia umasikini ni kutokana na elimu ndogo au kukosa mtaji! Ukweli ni kwamba; umasikini wa mtu umo katika fikra mbaya alizonazo.

Ongeza maarifa, acha kuomba omba, chukia umasikini lakini wapende masikini; wasaidie na uwaelimishe.

Jambo la mwisho ninalopenda kukwambia, ni hili: ONGOZWA NA ROHO MTAKATIFU. Pasipo Roho Mtakatifu hauwezi kumpendeza Mungu, na pasipo kumpokea Yesu hauwezi kuurithi uzima wa milele. Kila ufanyalo zingatia HAKI na KWELI.

Nimeongea mengi lakini kwa uchache sana; yatakuwa na msaada kwake yeye mwenye hekima na akili. Mungu tayari amekwisha kukubariki, tatizo limo tu kwenye akili yako! Kumbuka kwamba:

UMASIKINI maana yake ni hali ya kukosa maarifa pamoja na kuwa na fikra / mtazamo mbovu akilini mwako! (POVERTY simply means; Lack of knowledge and having bad attitude! The state of having negative mentality).

Nawatakia baraka tele katika jina la Yesu Kristo. Amen.

Sunday, December 28, 2014

KUTII NENO LA MUNGU NA UTAKATIFU KWANZA.

KAMPENI YA UZIMA WA MILELE: 

"KUTII NENO LA MUNGU NA UTAKATIFU KWANZA."

Ukristo sio dhehebu; bali Ukristo ni mahusiano bora na Mungu.

Watu wengi hudhani Ukristo ni dhehebu ambalo limeanzishwa ili kuleta ustaarabu fulani katika jamii. Wakristo wengi wanaishi maisha ya kuigiza kisa tu ni wafuasi wa kanisa fulani! Wengine wanayaacha maagizo ya Mungu na kuyaheshimu mapokeo potofu ya dhehebu fulani eti kisa tu na wao wanajiita wakristo! Wengi wanaishi maisha ya maigizo, wanatenda dhambi kwa siri huku wakijiita "wapendwa"! Ndugu yangu na rafiki yangu; hapo unajidanganya wewe mwenyewe. Hakuna dhambi unayoweza kumficha Mungu. Leo ninasema na roho yako! Yachunguze matendo yako, chunguza siri za nafsini mwako; umemtenda Mungu dhambi. Umekuwa mnafiki, umekuwa na majungu japo unajiita mkristo, umekuwa mwizi japo unaitwa mpendwa, umekuwa mwongo umezaa hata nje ya ndoa yako kwa siri ukidhani Mungu hakuoni, umekuwa mshirikina na umejaa hila nafsini mwako. Unatenda ukidhani hakuna akuonaye; kumbe hapo wajidanganya wewe mwenyewe.
Biblia Takatifu inatuambia kwamba:

"Pumzi ya mwanadamu ni taa ya BWANA; Hupeleleza yote yaliyomo ndani yake." ~ Mithali 20:27.

Hakuna jambo uwezalo kumficha Mungu. Yeye anayajua mawazo yako hata kabla hujatenda jambo. Mungu anajua kuwa leo umekusudia kufanya uzinzi japo kuwa unamficha mchungaji wako! Anajua kuwa leo umetoka kufanya uzinzi japo kuwa unasema "Bwana Yesu asifiwe"!
Ichunguze nafsi yako, tubu sasa kwa maana neema bado ingalipo kwako. Wokovu sio wa maigizo, bali wokovu ni maisha halisi. Najua umeanguka mara nyingi dhambini lakini leo unayo nafasi ya kurekebisha maisha yako; Tubu sasa, la sivyo jehanam ipo kwa ajili yako na inakungoja.

Narudia tena kwa msisitizo: Ukristo sio dhehebu; bali Ukristo ni mahusiano bora na Mungu. Ukristo unaonekana katika kunena kwako, kuvaa kwako, upendo wako kwa Mungu na kwa majirani zako. Huwezi kusema Mungu hatazami uvaaji bali anatazama tu roho yako! Hapo hakika haupo salama; hicho ni kiburi tu cha uzima kinachokusumbua. Biblia inasema kuwa sisi ni barua isomwayo na watu wote (2 Kor 3:2), je ni tabia ipi uioneshayo kwa watu wasiomjua Mungu? Huko ni kuutukana wokovu wako, na hakika utatoa hesabu ya matendo yako yote. Haijarishi kuwa wewe unajiita au unaitwa mtume au nabii, haijarishi wewe ni mwinjilisti au mchungaji, haijarishi kwamba wewe ni mwimbaji au ni mwalimu, na hata kama wewe ni muumini wa kawaida tu; lakini nakuambia usipotubu leo, hakika kesho yako itakuwa ni ya majuto; itakuwa ni kilio na kusaga meno milele yote.
Biblia inapotuambia tujitenge na uovu wa kila namna (Zaburi 107:42); ni kwa sababu dhambi iingiapo unaweza ukaiona kama ni kitu kidogo tu, lakini usipoitubu na kuikemea utajikuta umejenga mazoea ya kuiona ni kitu cha kawaida tu; na hapo ndipo uovu unaumbika ndani yako. Hata kama ukikemewa utakuwa na kiburi kwa maana hiyo roho ya kuizoelea dhambi inakuandama. Dhambi sio kitu cha kuzoelea hata kidogo, dhambi imekusudia kukutenga tena na Mungu; uwe makini sana mpendwa. Leo ninaongea nawe kwa upole, ninaonge na roho yako. Rekebisha matendo yako kwa maana neema bado ingalipo kwako.
Biblia Takatifu inasema:

"Wanyofu wa moyo wataona na kufurahi, Na uovu wa kila namna utajifumba kinywa.
Aliye na hekima na ayaangalie hayo; Na wazitafakari fadhili za Bwana.
" ~ Zaburi 107:42-43

Mtu MNYOFU ndiye atakayeufurahia uzima wa milele; lakini mwovu atakataliwa mbali kabisa na Mungu. Kila jambo linayo kanuni yake, hata uzima wa milele pia unayo kanuni yake. Biblia Takatifu inatuambia kwamba:

"Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;
mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo.
" ~ Waebrania 12:14-15

Tafuta kwa bidii amani kwa watu wote pamoja na huo UTAKATIFU. Tunapoelekea katika mwaka 2015, hebu kampeni yetu iwe ni "KUTII NENO LA MUNGU NA UTAKATIFU KWANZA" Tuyakemee na kujiepusha na mafundisho potofu.Tuzingatie hili:

"KUTII NENO LA MUNGU NA UTAKATIFU KWANZA"

Ukristo sio dhehebu; bali Ukristo ni mahusiano bora na Mungu. Nawatakia nyote baraka tele katika jina la Yesu Kristo, amen.

Thursday, December 25, 2014

UKWELI KUHUSU CHIMBUKO LA SIKU KUU YA CHRISTMAS.!

UKWELI KUHUSU CHIMBUKO LA SIKU KUU YA CHRISTMAS.!


Tusiwe wanafiki, tusiwe waongo! UONGO NI DHAMBI.

Mafundisho ya Yesu kazaliwa tarehe 25 Disemba yametoka wapi? Christmas sio sikukuu ya kusheherekea tarehe ambayo Yesu amezaliwa.
Tukitazama ushahidi wa Kibiblia hauoneshi Yesu alizaliwa mwezi gani wala tarehe gani; hata pia tukitazama ushahidi wa Kihistoria nao unatubainishia kuwa Yesu Kristo alizaliwa KATIKATI YA MWAKA 6 kwenda wa 5 b.C. Hivyo basi Yesu Kristo alizaliwa miezi ya KATIKATI YA MWAKA wala sio mwishoni mwa mwaka! Mambo haya ni muhimu sana kwako Mkristo uelewe, sio unakwenda tu kama kipofu.

Kwa ushuhuda wa kweli, katika Injili zote ndani ya Biblia Takatifu hakuna mahali po pote palipoandikwa kuwa Yesu Kristo alizaliwa majira yapi wala tarehe ipi; bali tunaona tu ushuhuda wa Yesu Kristo ambaye ni Mungu aliuvaa mwili kisha akazaliwa mfano wa mwanadamu! Kuzaliwa kwa Yesu Kristo kunaelezwa wazi wazi katika Injili ya Mathayo 2:1-16, na katika Injili ya Luka 2:1-7. Tangu kuzaliwa kwa Yesu, hata wakati wa utoto wa Yesu, hata wakati wa huduma ya Yesu hapa duniani, hata wakati wa mitume, hadi kufika mwaka wa 349 AD hapakuwa na sherehe ya kuzaliwa kwa Yesu mnamo tarehe 25 mwezi Disemba kila mwaka!

JE, DESTURI HII IMETOKEA WAPI?

Mara nyingi tunapoelekea mwishoni mwa kila mwaka, tangu mnamo mwaka 350 AD, watu wengi duniani husherehekea siku kuu maarufu sana ijulikanayo kwa jina Christmas. Siku kuu hiyo huadhimishwa kila tarehe 25 ya mwezi Disemba kila mwaka, na wengi huamini kuwa ndiyo tarehe ambayo Yesu Kristo alizaliwa! Je, ni kweli kuwa Yesu alizaliwa katika tarehe hiyo (tarehe 25 Disemba)?
Kusema ukweli, kabla ya mwaka 350 AD, sherehe ya Christmas haikuwepo kabisa, na wala hapakuwepo na maadhimisho ya Yesu kuzaliwa katika tarehe 25 Disemba hadi ulipofika mnamo mwaka 350 AD wakati ambao papa wa kanisa la RC aitwae jina lake Julius I alipotangaza rasmi kuwa tarehe 25 Disemba ndiyo itakuwa siku ya kusheherekea kuzaliwa kwa Yesu Kristo! Julius I alifanya hivyo kwa lengo la kuifuta na kuifidia siku ambayo wapagani walikuwa wakisherehekea kuzaliwa kwa “mungu” wao JUA na mwanzo wa majira ya “Spring” (kuchipuka kwa mimea).

Katika majira hayo ayo pia kulikuwa na sikukuu ya wapagani wa Kirumi inajulikana sana kwa jina la “Roman Saturnalia” ambayo pia Warumi walikuwa wanampa heshima “mungu” wao “Saturn” (sayari ya Satan), ambaye wao walikuwa wanamwabudu kuwa ndiye “mungu” wao wa mavuno! Warumi walikuwa wanaadhimisha sherehe hiyo kila mnamo tarehe 19 ya mwezi Disemba na ilikuwa inaadhimishwa kwa siku saba mfululizo hadi tarehe 25 ya mwezi huo wa Disemba ndipo maadhimisho ya siku kuu hiyo yalipositishwa.

Vivyo hivyo, katika Ulaya kaskazini, pia nao walikuwa wanaadhimisha sherehe ijulikanayo kwa jina la “Yule” ambayo pia waliifanya kwa heshima ya “mungu” wao kwa kuwa katika majira hayo ndipo wakati ambao majira ya baridi yalikuwa wanamalizika na jua lilianza kuchomoza.

Kimsingi na kiukweli maadhimisho ya siku ya Christmas HAYAMO ki Biblia, kwa sababu hayo ni mapokeo tu yaliyowekwa na wanadamu, na tena SIO TAHERE SAHIHI ambayo Yesu Kristo alizaliwa. Ndio maana yapo mataifa yanayoadhimisha kuzaliwa kwa Yesu mnamo mwezi Januari, na mengine wanaadhimisha miezi mingine kulingana na mtazamo wao; Bali hayo maadhimisho katika tarehe 25 Disemba yametokana na fundisho la Julius I wa kanisa la RC ambaye aliliweka kulingana na mitazamo yake yeye mwenyewe; japokuwa neno “Christmas” tukilinyambua tunapata jina “Christ - Mas” ambalo maana yake inakuwa “Christ” maana yake ni “Kristo”, na “Mas” huenda likawa na maana ya “Misa” japokuwa neno “Misa” lenyewe linakuwa linaandikwa “Mass” yenye double “ss” sio single “s”!

Huo ndio ukweli kuhusu chimbuko la sherehe ya Christmas katika tarehe 25 Disemba. Kwangu mimi binafsi Christmass ipo kila siku wala sio tu tarehe 25 Disemba kwa maana kila siku kwangu ni Ibada ya Kristo, pia ninajua kwamba Yesu HAKUZALIWA MWISHONI MWA MWAKA, bali Yesu Kristo ALIZALIWA KATIKATI YA MWAKA WA 6 kwenda MWAKA WA 5 b.C.

 Uthibitisho huo wa Yesu Kristo kuzaliwa mnamo KATI KATI ya mwaka wa 6 kwenda wa 5 b.C (k.K) pia unatibitishwa na Biblia ijulikanayo kwa jina la Life Application Study Bible, katika ule ukurasa wa "A20" kama jinsi picha hii inavyoonesha katika sehemu hiyo iliyozungushishwa duara jekundu.
Na kwa takwimu hizo, hata mwaka wa kwanza A.D (b.K) Yesu Kristo tayari alikuwa na umri wa miak mitatu unusu! Na hapo pia panapingana na ile dhana inayosemwa kuwa Yesu alipozaliwa ndipo miaka ikaanza kuhesabiwa kwa mfumo wa A.D.
Hilo fundisho la Yesu kuzaliwa tarehe 25 mwezi Disemba ni uongo tupu na ni lazima tulipinge kabisa, tena Kanisa la Kristo tunatakiwa kulipinga na kulipiga vita vikali kabisa.

Tuutafuteni wokovu sio kuitafuta tarehe ambayo Yesu alizaliwa; Kila siku tunapaswa kukumbuka kuzaliwa kwa Yesu na thamani ya wokovu huu; sio tu katika tarehe 25 Disemba, bali kila siku tuwe katika uwepo wa Kristo. Mimi binafsi, kila siku kwangu ni Christ mass, hata leo pia. Tarehe haiokoi, bali Yesu ndiye anaokoa.


Je, wewe unasherekeaje Christmass?

Tuesday, October 21, 2014

UMEPEWA TUMAINI MAHALI PASIPO NA TUMAINI ! ! ! ~ Fahamu ukweli huhusu Purgatory (toharani)

UMEPEWA TUMAINI MAHALI PASIPO NA TUMAINI ! ! !

SHETANI AMEKUPIGA NGWALA, NAWE UMEANGUKA CHINI PUU!!! POLE KWA MAANA HUJITAMBUI, FUMBUA AKILI SASA KABLA HUJALALA FOFOFO.

Biblia inatuambia kwamba; Shetani ni "mdanganyifu", tena kazi yake ni sawa na "mwizi" ambaye ni mwaribifu, tena Shetani ni "mjanja sana"; Tazama sasa amekupa tumaini mahali pasipo na tumaini!

Purgatory (toharani)

Kwa imani ya baadhi ya makanisa yanawaambia watu kwamba ipo sehemu ya kutakasa DHAMBI NDOGO baada ya wao kufa katika hizo waziitazo DHAMBI NDOGO.
Wao wanasema hivi:

Purgatory (toharani) ni nyumba iliyopo katikati ya Mbinguni na kuzimu. Ni mahali pa kutakasia ambapo roho itaona maumivu kwa muda kidogo kabla ya kufaa kupata kibali cha kuingia mbinguni. Kwa hiyo; wao wanasisitiza: Watu waliobaki hai duniani watakapofanya maombi, kuwasha mshumaa na kutoa fedha kwenye kanisa huweza kupunguza muda ambao roho inaweza kupata machungu ya mateso ya kutakaswa katika 'Purgatory’ (Toharani).

Je! Biblia inazungumziaje fundisho hilo?

~ Biblia INAPINGA mafundisho hayo POTOFU. Tena HAKUNA DHAMBI KUWA WALA DHAMBI NDOGO "Atendaye dhambi ni wa Ibilisi..." - 1 Yoh 3:8. Tena hukumu yao ni kutupwa katika ziwa la moto wa mateo ya milele (UFUNUO 21:8)

Ukweli ni huu:

"Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu" ~ WAEBRANIA 9:27
SASA HIVI ndio muda pekee ambao Mungu amekupatia kutengeneza mazingira mazuri ya roho yako baada ya kufa. Lakini, pindi tu utakapo kata roho, hapo ndipo MWISHO wa hesabu ya matendo yako. Kinachokuwa kimebaki kwa wakati huo ni WEWE KUISUBIRI HUKUMU ambayo itakuwa sawa sawa na jinsi MATENDO yako yalivyo. KIFO KINAFATIWA NA HUKUMU. Wafu wote wamehifadhiwa kwa ajili ya HUKUMU ambayo kila mtu atahukumiwa SAWASAWA na MATENDO YAKE MWENYEWE (soma kitabu cha Ufunuo 20:13).

Usiufanye moyo wako mgumu katika dhambi; usisubiri KUOMBEWA baada ya kufa kwako! Fanya maamuzi sahihi wakati huu ambapo neema bado ingalipo kwako. Biblia Takatifu inatuambia:

"...tazama,wakati uliokubalika ndiyo sasa; tazama siku ya wokovu ni sasa." ~ 2 Kor 6:2.

Usiiache neema hii ikupite bure! Bwana Yesu anasema:

"Hakuna mtu awezaye kuja Kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka; nami nitamfufua siku ya mwisho." ~ YOHANA 6:44.

UJUMBE HUU UNAKUHUSU WEWE ULIYEGUSWA NA INJILI HII: HACHA KUPEWA TUMAINI MAHALI PASIPO NA TUMAINI ! ! !

HAKUNA NEEMA BAADA YA KIFO. SASA HIVI NDIO WAKATI WA KUTENGENEZA MAZINGIRA YA ROHO YAKO BAADA YA KUFA; NA HUU NDIO WAKATI MUAFAKA WA KUMPOKEA YESU ILI AKUPATIE WOKOVU.

"Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana..." ~ Kor 6:17

Saturday, October 4, 2014

UZIMA NA MAUTI VIPO MBELE YAKO, BARAKA NA LAANA ZIPO MBELE YAKO. UCHAGUZI NI WAKO ! ! !

SIRI YA KUANGAMIA IPO HIVI:

~ TENDA DHAMBI

~ KAIDI NENO LA MUNGU

~ SHIKA MAPOKEO YANAYOPINGANA NA NENO LA MUNGU
(Mfano; Neno la Mungu linapokwambia: "USIIBE" wewe iba; ukiambiwa "USIZINI" wewe zini; ukiambiwa "USISEME UONGO" wewe sema uongo; Ukiambiwa: "USIOMBE WAFU" wewe omba wafu; ukiambiwa: "YESU NI MUNGU" wewe kataa; ukiambiwa "USIABUDU SANAMU" wewe abudu; ukiambiwa: "USIUE" wewe ua!

Kweli nakuhakikishia kabisa ukifanya hivyo UTAANGAMIA; kwa sababu neno la Mungu linatuambia hivi:
 "Bali WAOGA, na WASIOAMINI, na WACHUKIZAO, na WAUAJI, na WAZINZI, na WACHAWI, na hao WAABUDUO SANAMU, na WAONGO WOTE, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti..." ~ UFUNUO 21:8
HIYO NDIO SIRI YA KUANGAMIA. ANGAMIA UKIWA UNAJITAMBUA KABISA UNAANGAMIA, NA MWISHO WAKO UTATUPWA KATIKA ZIWA LA MOTO WA MATESO YA MILELE.

ZINGATIA HILI: HAKUNA NEEMA BAADA YA KIFO; HAKUNA MAOMBI YA KUMWOKOA MTU ALIYEKUFA KATIKA DHAMBI; HAKUNA UTAKASO WA DHAMBI KWA MFU !

NAYO SIRI YA UZIMA WA MILELE IPO HIVI:


TUBU SASA!
UPOKEE WOKOVU MAANA NEEMA BADO INGALIPO, MKIRI YESU AWE BWANA NA MWOKOZI WAKO, BATIZWA NA USHIKE KILA NENO ALILOTUAMURU YESU TULIFANYE. UKIFANYA HIVYO UTAKUWA NA UZIMA TELE, TENA UZIMA WA MILELE.
UCHAGUZI NI WAKO, KWA MAANA NENO LA MUNGU LINATUAMBIA HIVI:
"Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako;
kumpenda BWANA, Mungu wako, kuitii sauti yake, na kushikamana naye; kwani hiyo ndiyo uzima wako..."
~ KUMB 30:19-20
UZIMA NA MAUTI VIPO MBELE YAKO, BARAKA NA LAANA ZIPO MBELE YAKO.

UCHAGUZI NI WAKO ! ! !

Monday, August 11, 2014

"Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote..." ~ WAKOLOSAI 3:16

"Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote..." ~ WAKOLOSAI 3:16

Kama jinsi mwili unavyoweza kudhoofika kwa kukosa chakula bora; vivyo hivyo na roho yako idhoofikavyo kwa kukosa neno la Mungu. Kama jinsi urafiki kati ya mtu na mtu unavyoweza kuvunjika kwa kukosa mawasiliano ya mara kwa mara; vivyo ndivyo kukosa sala na maombi kunaifanya roho yako ijitenge mbali na Mungu.

Watu wengi wapo bize (busy) katika shughuli zao hata wanamsahau Mungu; Je, wajua kwamba shughuli zote uzifanyazo ni ubatili, isipokuwa tu kumtumikia Mungu!

Elewa kwamba; mbinguni hautaingia kwa sifa ya udaktari, kwani huko hakuna wagonjwa; mbinguni hautaingia kwa sifa ya uinjinia (uhandisi) kwani huko mbinguni miji imeshawekwa tayari na barabara zake hazibomoki; wala uanasiasa wako hauna nafasi mbinguni, kwa maana Mungu peeke ndiye Mtawala wa huko; hata ujuzi wako katika sekta ya ulinzi, upelelezi na usalama hauhitajiki mbinguni! Mbinguni hakuna nafasi za kazi ya uhakimu, uanasheria, wala uwakili, kwa maana waovu hawatakuwepo huko. Sasa wewe wajuvunia nini! Je, ujuzi wako unafaida gani endapo usipomtumikia Mungu?

Ukristo sio dhehebu, bali Ukristo ni uhusiano kati ya mtu na Mungu. Wewe umeokolewa ili ufanyike chombo cha kuwahubiria hao watu wakuzungukao; pia umeajiriwa katika kitengo hicho ulichopo ili uwe chombo cha kulifikisha neno la Mungu mahali hapo. Upo hapo kwa ajili ya utukufu wa Mungu. Usiionee haya Injili, kaza mwendo, nawe utaipokea taji ya uzima kutoka kwa Bwana wetu Yesu.

Kumbuka; NENO LA KRISTO YESU LIKAE KWA WINGI NDANI YAKO. SALA NA MAOMBI NDIYO SILAHA YAKO KATIKA IMANI.

Nakutakia baraka tele.

Friday, March 21, 2014

Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo...!

"Moyo wa mwenye ufahamu hutafuta maarifa..." - Mithali 15:14.
Ujaze moyo wako kwa UFAHAMU; kwa maana Biblia Takatifu inasema: "Ufahamu ni chemchemi ya uzima kwake aliye nao..." (Mithali 16:22). Moyo wako ujaapo UFAHAMU ndipo utamtukuza Mungu kwa kila tendo na kila neno litokalo katika kinywa chako. Ndio maana Biblia inasema kwamba:
"Moyo wake mwenye hekima hufundisha kinywa chake; Huzidisha elimu ya midomo yake." - Mithali 16:23.
Moyo ndio ufundishao KINYWA cha mtu mwenye HEKIMA. Moyo ndio uongoza MIDOMO ya mtu mwenye HEKIMA; Tena Biblia inasema kwamba: "Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima." (Mithali 4:23).
Je! Nini maana ya MOYO kulingana na Maandiko hayo?
Tunapo zungumzia neno "MOYO" kwa Mujibu wa Biblia Takatifu; upo wakati neno "MOYO" limetumika kumaanisha "ROHO" (mf. Zab 51:10,17; Eze 36:26) ambao ndio undani wa mtu, au uzima wa mtu; Lakini pia kuna wakati neno "MOYO" limetumika kumaanisha "NAFSI au AKILI" ya mtu, ambayo ndiyo NIA ya mtu katika kutenda jambo fulani; na pia kuna wakati neno "MOYO" limetumika kumaanisha "MOYO" wenyewe (kiungo cha mwili).
Sasa basi; katika maandiko hayo tuliyoyasoma hapo awali (Mithali 4:23; 15:14; 16:22,23) neno "moyo" limetumika kumaanisha "NAFSI" au "AKILI" ya mtu. Je! Nini maana ya NAFSI?
Neno nafsi maana yake ni kituo cha maamuzi katika mwili wa binadamu, kinachofanya maamuzi kati ya roho na mwili wa mtu. Nafsi / akili ya mwanadamu ndiyo inayoongoza kile mtu afanyacho; nafsi / akili ya mtu ikijaa mambo yakumchukiza Mungu, ndipo mtu huyo utenda machukizo mbele za Mungu. Je! Wewe akili yako imejaa nini ndani yake?
Akili / nafsi ya mtu ndiyo inabeba NIA ya kila ufanyalo! Biblia inasema kwamba:

"Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu." - Warumi 12:2.
Hapo tunaona Biblia inasema: "...mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu..." Huko kufanywa UPYA katika NIA ni kufanya akili zetu kupokea mambo yampendezayo Mungu ili ufahamu wetu upate kujaa kila jema la kumpendeza Mungu. Akili yako ijaapo neno la Mungu ndipo kinywa na matendo yako yote yatampendeza Mungu. Mambo hayo yajazayo akili ya mtu, ndiyo hayo mtu huyo atayafanya. Haiwezekani kuyajua MAPENZI ya Mungu ikiwa NIA / AKILI / NAFSI yako imeharibika; nafsi / nia / akili ya mtu huweza kujengwa au kuharibiwa kwa kile UNACHOONA / UNACHOTAZAMA, UNACHOGUSA, pamoja na kile UNACHOSIKIA!!! Uwe makini sana katika UONACHO, UGUSACHO, na USIKIACHO.
Je! Ni neno lipi liwezalo kuzigeuza nia zetu? Biblia Takatifu inatuambia kwamba:
"Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu." - (Wakolosai 3:16).
Biblia Takatifu inatuambia: "Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu..." Si kwamba LISIMAME, bali LIKAE kwa wingi ndani yetu. Neno la Bwana Yesu LIKIKAA kwa WINGI NDANI yako ndipo ufahamu wako utajaa uzima na kila jema la kumtukuza Mungu. Nasisitiza tena; Hapa sisemi LISIMAME NDANI YAKO, bali ninasema NENO LA KRISTO LIKAE NDANI YAKO; wala si kukaa tu, bali LIKAE KWA WINGI ndani yako. Upo utofauti kati ya KUSIMAMA, na KUKAA. 
Sasa hebu ruhusu neno la Bwana Yesu Kristo LIKAE NDANI YAKO, ndipo akili / nafsi / nia yako itajaa hekima na chemchemi ya uzima ndani yako.

"Linda AKILI / NIA / NAFSI yako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima."
Akili yako ikiharibika, mwili na roho yako nazo zitaharibikiwa na kupotea!
Nakutakia baraka tele katika jina la Yesu Kristo.


Sunday, October 27, 2013

JE ! WEWE UMEBARIKIWA?

JE ! WEWE UMEBARIKIWA?

Kubarikiwa ni kuwa na amani, furaha, na uzima wa milele. Kubarikiwa sio tu kuwa na wingi wa mali; bali ni kuwa na Yesu moyoni mwako. Kubarikiwa ni kujazwa Roho Mtakatifu, kutembea Naye, pamoja na kuishi maisha matakatifu. Kubarikiwa ni kuwa na uhakika wa kuwa hai milele katika roho yako.

JE ! WEWE UMEBARIKIWA?

Kubarikiwa ni kumpokea Yesu awe Bwana na Mwokozi wa maisha yako. BARAKA KAMILI IMO NDANI YA YESU KRISTO PEKEE. Mpokee Yesu sasa ili nawe akupe baraka kamili.

JE ! WEWE UMEBARIKIWA?

Kubarikiwa ni kupata uwezo wa kuishinda dhambi na kuacha kutenda dhambi. 

JE ! WEWE UMEBARIKIWA?

Kubarikiwa ni kupata neema ya kuwafanya watu wawe wanafunzi wa Yesu; Kubarikiwa ni kupata uwezo na ujasiri wa kuhubiri Injili bila woga na kuharibu kila kazi ya Shetani.

JE ! WEWE UMEBARIKIWA?

Shalooom wana wa Mungu. 

REACH OUT TO THE WORLD & PREACH THE GOSPEL OF JESUS.

Monday, September 16, 2013

Uchaguzi wako na uhamuzi wako ndio matokeo ya jinsi ambavyo wewe ulivyo.

Je! Wajua ? ? ?

"MTU ANAKUWA MASIKINI KWA SABABU YEYE MWENYEWE AMECHAGUA AU AMEKUBALI YEYE MWENYEWE KUWA HIVYO." Uchaguzi wako na uhamuzi wako ndio matokeo ya jinsi ambavyo wewe ulivyo.

Bibilia Takatifu inasema kwamba:
"Mtu mvivu hapiki mawindo yake; Bali mwenye bidii anazo mali za thamani." ~ MITHALI 12:27.
Siku zote watu wengi huwa masikini kwa sababu ya UVIVU walio nao. Upo uvivu wa namna tofauti, mfano: Uvivu wa kufikiri; na, Uvivu wa kufanya kazi. Watu wengi ni wavivu wa kufikiri namna ya kufanyia ufumbuzi changamoto mbali mbali wanazokutana nazo maishani; wamekuwa ni wepesi wa kukata tamaa. Wao wanataka kwanza warahisishiwe mambo ndipo wapate wepesi. Hawapendi kabisa kushughulisha akili zao; watu wa namna hiyo hawafanikiwi kwa sababu ya uvivu walio nao.

Tukija kwenye kundi la wavivu wa kufanya kazi; hapa napo wapo watu wengi sana. Watu hawa wamekaa wakisubiri kula kutoka katika kazi za wenzao; hawalimi lakini wao ni wa kwanza kuvuna hata ambavyo havijakomaa; hawapiki lakini wao ni wa kwanza kuuliza kama vimeiva jikoni; wanakataa kuajiriwa lakini wao ndio wa kwanza kuuliza kama mshahara umetoka; hawatafuti chakula lakini wao ndio wa kwanza kulalamika kuwa chakula hakitoshi mezani; na hawataki kujishughulisha lakini wao ndio wa kwanza kulalamika maisha ni magumu. Wanashinda vijiweni na wengine utawaona kutwa amekaa kwenye makochi sebureni akinyanyanyana remote control ya tv na watoto; wanajivunia mali za ndugu zao. Watu hao ni wapumbavu wanaokesha wakiomba ndugu zao wafe ili wao wapate mirathi. Na endapo wakiambiwa wajitegemee utasikia wakisema fulani ana roho mbaya, apendi kukaa na ndugu.
Biblia Takatifu inasema kwamba:
"Ataabishaye nyumba yake mwenyewe ataurithi upepo; Mpumbavu atakuwa mtumwa wa mtu mwenye moyo wa akili." ~ MITHALI 11:29
Kama na wewe ni miongoni mwao basi fahamu kuwa wewe ni MPUMBAVU na urithi wako unaokustahiri ni UPEPO. Kwa maana nyepesi ni kwamba wewe utakufa ukiwa hauna mali. Kwa nini ushinde sebureni kuwataabisha watoto kwa kunyanganyana nao remote ya tv? Kwa nini ushinde nyumbani kuwasumbua mawifi zako na mashemeji zako badala ya wewe kwenda kufanya kazi? Biblia inasema kwamba wewe ni mpumbavu na utakuwa mtumwa wa mtu mwenye moyo wa akili. Huo umasikini wako ulio nao ni matokeo kabisa ya uchanguzi ambao wewe mwenyewe umeuchagua. Mungu ajakuumba ili uishi kwa huzuni hapa duniani; wewe mwenyewe unaweza ukawa kichocheo cha furaha yako au huzuni yako uliyo nayo. Hebu badirika ufahamu wako sasa. Mtumainie Mungu huku ukiwa unafanya kazi.
Unajua kuna mambo ambayo watu huyakosea pasipo kujua; Zipo baraka za aina mbili ambazo Mungu anatupatia watu wake, ambazo ni: Baraka za mwilini, pamoja na baraka za rohoni. Baraka za rohoni huja kwa njia ya maombi; wakati baraka za mwilini huja kwa njia ya kufanya kazi huku ukimtumainia Mungu katika mambo yako yote. Umasikini ulionao unatokana na shida iliyomo ndani ya ufahamu wako. Usimsingizie shetani kabisa katika hilo. Uvivu wako ndio matokeo ya jinsi ulivyo. Biblia Takatifu inasema kwamba:
"Je! Wamwona mtu mwenye bidii katika kazi zake? Huyo atasimama mbele ya wafalme; Hatasimama mbele ya watu wasio na cheo." ~ MITHALI 22:29.
Hapo Biblia Takatifu inasema "...Wamwona mtu mwenye BIDII katika KAZI zake?..." Bidii hiyo inatakiwa iwepo katika KAZI sio katika KUOMBA OMBA. Hebu tazama hata mataifa yanayofanikiwa hapa duniani ni yale ambayo yameweka BIDII katika kufanya KAZI. Endapo akili yako ukiielekeza katika kuomba omba kamwe hautafanikiwa; kwa sababu Mungu anasema "..HERI KUTOA KULIKO KUPOKEA..." au kwa maana nyepesi ni kwamba "AMEBARIKIWA YEYE ANAYETOA KULIKO YULE ANAYEPOKEA." Usipende kuwa omba omba, bali fanya kazi zako kwa bidii huku ukimtumainia Mungu katika mambo yako yote.
Japokuwa hapa duniani tunapita, lakini Mungu anataka tufanikiwe miili yetu kama jinsi roho zetu zifanikiwavyo. Usiwe mvivu, fanya kazi nawe utaona baraka za Mungu zikimiminika maishani mwako. Pia kuwa mwaminifu kwa sababu Mungu huwapenda watu waaminifu; wawezeshe kwa kuwaonyesha njia wanaohitaji msaada wa kuinuliwa (usiwe mchoyo / saidia wengine). Mwisho kabisa napenda kusema kwamba fanya mambo yako kwa maarifa bila pupa, kwa maana imeandikwa:
"Kila aliye na busara hutenda kazi kwa maarifa; Bali wapumbavu hueneza upumbavu." ~ MITHALI 13:16.
Epukana na mambo yasiyofaa. Usiutangaze ubaya bali utangaze wema wa Mungu. Mungu anakupenda na hataki uishi maisha ya tabu hapa duniani. Usiwe mvivu; fanya kazi kwa bidii huku ukimtumainia Mungu na ukiwa mwaminifu Kwake ndipo utaona milango ya baraka ikikufungukia maishani mwako. Endapo ukiona umepata vipingamizi katika kazi hii, basi achana nayo na ufanye kazi nyingine yenye maslahi zaidi kwako. Usikate tamaa; mtumaini Yesu naye atakuwezesha katika mambo yako yote.
Biblia inasema kwamba:
"Mwenye haki hula akaishibisha nafsi yake; Bali tumbo la mtu mbaya litaona njaa." ~ MITHALI 13:16, 25.
Umasikini ulionao unatokana na shida iliyomo katoka ufahamu wako (akili zako), au umasikini unatokana na uvivu wako. Usimlaumu mtu kwa sababu wewe mwenyewe ndivyo umechaguwa kuwa hivyo. Ukitaka kuamini maneno haya; basi chukua hatua sasa nawe utathibitisha hiki nisemacho.

Wewe uliye fanyia kazi ujumbe huu; nakutakia baraka tele katika jina la Yesu Kristo. Amina.

TUMA KWA RAFIKI :

Twitter FacebookMore

 
Kuhusu Huduma Hii | Masharti Ya Utumiaji Wa Tovuti Hii | Wasiliana Nasi | Tangaza Kupitia Tovuti Hii