Kumpokea
Yesu maana yake ni KUKIRI kwamba Yesu ni MWOKOZI, na pia hakuna mwingine
awezaye kuokoa isipokuwa Yesu pakee. Biblia Takatifu inatuambia kwamba:
“Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote,
kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.”
(Matendo 4:12)
Ni Yesu pekee anayetuokoa wala si mtu mwingine
ye yote yule. Wapo watu wengine wanaokiri kwamba Yesu ni Mwokozi lakini bado
wanasema kuwa wapo wanadamu wengine wanaoweza kuwaokoa badala ya Yesu; huko ni
sawa na wanajidanganya wao wenyewe na tena wanapotea japokuwa wanajiita
Wakristo. Kuwa mfuasi wa Yesu ni kushika “...YOTE...” na kuwafundisha watu
kushika “...YOTE...” ambayo Yesu ametuamuru sisi bila kuongeza neno wala
kupunguza neno (Mathayo 28:20). Hatuokolewi kwa jina la Mariamu mama wa Yesu
wala kwa jina la mtakatifu ye yote yule; bali hao tunawaheshimu kwa kutambua na
kuuthamini mchango wao katika huduma ya Mungu sawa sawa na jinsi ambavyo
tunavyowaheshimu watumishi wengine wote wa Mungu, lakini wokovu upo kwa Yesu
pekee. Hilo
ndilo neno la Mungu lisemavyo, na tena imeandikwa:
“...Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu.”
(Matendo 5:29)
Yesu ni Mwokozi kwa sababu wokovu wetu upo kwa
Yesu pekee. Wala HAKUNA mtu ye yote yule mwingine aliyeutoa uhai wake kwa ajili
ya msamaha wa dhambi zetu; bali ni Yesu pekee. Unapompokea Yesu unakuwa
umeokoka. Najua hapa unaweza ukahoji kuwa: “Je! Nawezaje kuokoka ningali hai
bado humu duniani?” Mpendwa; hayo mawazo uliyonayo ni akili za kibanadamu
lakini kwa Mungu wokovu upo sasa wala si baadae. Biblia Takatifu inatuambia
kwamba:
“...Tazama, wakati uliokubalika ndio sasa; tazama,
siku ya wokovu ndiyo sasa.” (2 Wakoritho 6:2)
Je! Nini basi maana ya WOKOVU?
Wokovu maana yake: ni kutoka katika mateso,
shida, dhiki, na taabu za kila aina; kisha unapatiwa ulinzi ambao utakuweka
salama. Unaweza ukashangaa na ukahoji; “Mbona basi Yesu ametuokoa alafu bado
tunaishi katika dunia hii yenye tabu na mateso mengi?”
Mateso na tabu hizi za duniani ni za muda
mfupi tu. Na pia Mungu ameruhusu sisi tuwemo humu duniani ili tufanye kazi ya
kuhubiri neno la Mungu kwa watu wale ambao bado hawajalipokea ili nao wapate
kuokoka (Yohana 17:15-17). Wakati huu ni wa muda mfupi tu, na baada ya hapa
tutapewa maisha ya uzima wa milele yasiyokuwa na shida, tabu, wala mateso ya
namna yo yote ile. Biblia Takatifu inatuambia kuwa Mungu:
“...atafuta kila chozi katika macho yao , wala mauti
haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo
tena...” (Ufunuo 21:4)
Dhiki hizi za duniani ni matokeo ya vita dhidi
yetu na Shetani. Vile vile Yesu hajatutelekeza hapa duniani bali ametuachia
ulinzi wa Mungu unaotuwezesha sisi kuishi salama japokuwa tupo katika dunia
yenye majaribu. Bwana Yesu ametuambia kwamba:
“...mpate kuwa na amani ndani Yangu. Ulimwenguni
mnayo dhiki; lakini jipeni moyo, Mimi nimeushinda ulimwengu.” (Yohana 16:33)
Wokovu huu
tulionao unamaana ya kwamba:
Þ
Wokovu ni msamaha wa dhambi ambao Yesu ametupatia baada ya kufa msalabani
kwa ajili ya ondoleo la dhambi zetu. Msamaha huu wa dhambi tunaupokea bure kwa
njia ya imani na neema tu kwa kumkiri Yesu kuwa Yeye ni Bwana na Mwokozi wa
maisha yetu. Biblia Takatifu inatuambia kwamba:
“Kwa maana
mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu,
ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu.”
(Waefeso 2:8,9)
Biblia
imesema: “...MMEOKOLEWA...” maana yake ni tayari huo wokovu tunao hivi sasa.
Laiti kama wokovu tungekuwa bado hatujaupata basi hapo pangeandikwa
“...MTAOKOLEWA...” Lakini kwa kuwa tayari wokovu huu tunao ndio maana hapo
pameandikwa: “...MMEOKOLEWA...” Wokovu huu ni BURE kwa njia ya IMANI na KUKIRI
kuwa Yesu ni Bwana na Mwokozi wa maisha yako (Matendo 16:31).
Þ
Wokovu huu ni ushindi ambao Yesu ametupatia na kutuwezesha kuharibu
kila kazi ya Shetani na kumshinda Shetani kutokana na Roho Mtakatifu akaaye
ndani yetu. Bwana Yesu ametuambia kwamba:
“Tazama,
nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala
hakuna kitu kitakachowadhuru.” (Luka 10:19)
Japokuwa
tunapita katika majaribu mbalimbali humu duniani lakini Yesu ametuwezesha
kumshinda Shetani. Shetani tayari amekwishashindwa, kilichabaki ni sisi tu
kumkemea Shetani naye lazima atatii; kwa maana imeandikwa: “...Mpingeni
Shetani, naye atawakimbia.” (Yakobo 4:7). Hivyo wokovu tulionao sasa umetupatia
nguvu ya Mungu itupatiayo ushindi juu ya dhambi, Shetani, na pepo wachafu
katika maisha yetu ya kila siku.
Þ
Pia, Wokovu huu tulionao ni hakikisho la uzima wa milele tuliopewa
tayari na Bwana Yesu baada ya ufufuko wake kwa kuyashinda mauti. Japokuwa miili
yetu itakufa lakini tunalo hakikisho la uzima wa milele kwa maana Biblia
Takatifu inatuambia kwamba:
“...sisi,
wenyeji wetu uko mbinguni, kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu
Kristo. Atakayeubadili mwili wetu wa unyonge upate kufanana na mwili Wake wa
utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote chini
Yake.” (Wafilipi 3:20,21)
Kwa hiyo
wokovu huu tulionao hivi sasa unatupatia uhakika wa uzima wa milele baada ya
uharibifu utakaotokea katika miili hii tuliyonayo hivi sasa. Hivyo ndivyo neno
la Mungu linavyosema kuwa “...WAKATI ULIOKUBALIKA NDIO SASA; TAZAMA, SIKU YA
WOKOVU NDIYO SASA.” (2 Wakorintho 6:2) Kama wewe unapingana na Biblia Takatifu;
basi, wewe mwenyewe utajibu mbele za Mungu kwa nini umepingana na neno Lake .
Dunia
tunayoishi imejawa na mafundisho mengi yanayopotosha ambayo yamesababisha
mgawanyiko mkubwa wa imani na njia za kumtafuta Mungu wa kweli, na watu wengi wanapotea
pasipo hata wao kujitambua kuwa wanapotea. Japokua duniani wapo wapotoshaji
wengi, lakini haimaanishi kwamba neno la kweli la Mungu halipo; La! Neno la
Mungu la kweli lipo na wala halijabadilika na tena lipo wazi wala
halijajificha. Jambo la muhimu linaloweza kukusaidia ni wewe kuwa tayari
kulipokea neno hilo la Mungu na pia ukalifanyia
kazi kwa kuishi kama jinsi neno la Mungu
lisemavyo.
Ni kweli
kwamba Shetani yupo vitani dhidi yetu sisi watakatifu na watu wa Mungu tuliopo
hapa duniani, lakini sisi hatuwezi kumshinda shetani kwa nguvu na uwezo wetu
bali ni kwa nguvu na uweza wa Mungu unaotuwezesha. Hakika tunahitaji msaada wa
Yesu maishani mwetu ili tupate uzima wa milele.
Inawezekana
kabisa wewe unayesoma ujumbe huu umeshitushwa na maandishi hayo yaliyopo juu ya
ukurasa wa somo hili yasemayo “Yesu ni Mungu.” Yawezekana haufahamu hivyo
kutokana na mafundisho uliyoyapokea hapo awali; lakini napenda nikuambie neno hili:
Kutokufahamu kwako na kukana kwako hakuwezi kuuvua Uungu wa Yesu. Yesu anabaki kuwa Mungu daima na milele yote. Nitakupa ushahidi wa baadhi ya
maandiko matakatifu yanayotuthibitishia kuwa Yesu ni Mungu.
Biblia
Takatifu inatuambia kwamba:
“Twajua ya
kuwa sisi tu wa Mungu; na dunia yote pia hukaa katika yule mwovu. Nasi twajua
kwamba Mwana wa Mungu amekwisha kuja, naye ametupatia akili kwamba tumjue Yeye
aliye wa kweli, nasi tumo ndani yake Yeye aliye wa kweli, yaani, ndani ya Mwana
Wake Yesu Kristo. Huyu ndiye Mungu wa kweli, na uzima wa milele.” (1 Yohana
5:19,20)
Hapo
tunaona Biblia Takatifu inatuambia: “...Yesu Kristo. Huyu ndiye Mungu wa kweli,
na uzima wa milele.” (1 Yohana 5:20). Ukimpokea Yesu unakuwa “...NDANI...” ya Yesu
ambaye ndiye Mungu wa kweli, pia ni Mwokozi wetu na uzima wa milele. Pia Biblia Takatifu inatuambia
kwamba:
“Tukilitazamia
tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa Kristo Yesu, Mungu mkuu na
Mwokozi wetu, Ambaye alijitoa nafsi Yake kwa ajili yetu, ili atukomboe na maasi
yote na kujisafishia watu wawe milki Yake Mwenyewe, wale walio na juhudi katika
matendo mema.” (Tito 2:13,14)
“Inawezekanaje
Yesu awe Mungu wakati alizaliwa na kuishi kama
mwanadamu?”
Ni kweli
jambo hili pia nalo huwashinda watu wengi kulielewa; Wapo watu waonakiri kuwa
Yesu ni Bwana lakini wanakana kwa kusema Yesu si Mungu. Ukweli ni kwamba Yesu
ni Mungu. Je! Yesu ni Mungu kwa vigezo vipi?
Ni vema
kwanza kabisa ukafahamu kwamba jina Mungu ni “cheo” ambacho kinazo sifa za
kipekee zifuatazo:
i:
Mwenye hicho cheo cha "Mungu"
Yeye hakuumbwa bali alikuwepo na tena hana mwanzo wala mwisho.
ii:
Mwenye hicho cheo cha "Mungu"
Yeye ndiye ameumba mbingu, nchi, na vitu vyote. Yeye ndiye mwanzo wa uhai wote.
iii:
Mwenye hicho cheo cha "Mungu"
Yeye ndiye mwenye amri na mamlaka ya kusamehe dhambi, pasipo Yeye hakuna
ondoleo la dhambi.
iv:
Mwenye hicho cheo cha “Mungu” Yeye ndiye
anayo mamlaka ya kuhukumu ulimwengu.
Hizo ndizo
sifa za kipekee kabisa ambazo Mungu anazo. Hebu tujifunze; je! Yesu Kristo
anazo sifa hizo za Mungu?
Jibu ni
“NDIYO” kwa uthibitisho ufuatao:
A. Yesu Kristo hajaumbwa
bali alikuwepo tangu milele yote.
Ni kweli
kabisa kwamba Yesu alikuwepo tangu milele yote kabla ya kuumbwa kitu cho chote
kile. Bwana Yesu kwa kauli ya kinywa chake mwenyewe anasema kwamba:
“Na sasa,
Baba, unitukuze Mimi pamoja Nawe, kwa utukufu ule Mimi niliokuwa nao pamoja Nawe
kabla ya ulimwengu kuwako.” (Yohana 17:5)
Neno
“UTUKUFU” maana yake ni heshima, uweza, uzuri, umaarufu, nguvu, sifa na mamlaka.
Mambo hayo yote Yesu alikuwa nayo kabla hata ulimwengu haujaumbwa. Yesu Kristo
alikuwapo hata kabla ya kuzaliwa na Mariamu; jambo hili pia Yesu Kristo kwa
kinywa Chake Yeye mwenyewe ametuthibitishia alipokuwa akiwaambia Wayahudi
kwamba:
“Yeye aliye wa Mungu huyasikia maneno ya
Mungu; hivyo ninyi hamsikii kwa sababu ninyi si wa Mungu.
Wayahudi wakajibu, wakamwambia, Je! Sisi
hatusemi vema ya kwamba wewe u Msamaria, nawe una pepo?
Yesu akajibu, Mimi sina pepo; lakini Mimi
namheshimu Baba yangu, na ninyi mwanivunjia heshima Yangu. Wala mimi siutafuti
utukufu Wangu; Yuko mwenye kutafuta na kuhukumu. Amin, amin, nawaambia, Mtu
akilishika neno langu, hataona mauti milele. Basi Wayahudi wakamwambia, Sasa tumeng’amua ya
kuwa una pepo. Ibrahimu amekufa, na manabii wamekufa; nawe wasema, Mtu
akuilishika neno langu, hataonja mauti milele. Wewe u mkuu kuliko baba yetu
Ibrahimu, ambaye amekufa? Nao manabii wamekufa. Wajifanya u nani? Yesu akajibu, Nikijitukuza mwenyewe, utukufu
wangu si kitu; anitukuzaye ni Baba Yangu, ambaye ninyi mwanena kuwa ni Mungu
wenu. Wala ninyi hamkumjua; lakini mimi namjua. Nikisema ya kwamba simjui,
nitakuwa mwongo kama ninyi; lakini namjua, na neno lake nalishika .
Ibrahimu baba yenu, alishangilia kwa vile atakavyoiona siku yangu; naye
akaiona, akafurahi.
Basi Wayahudi wakamwambia, Wewe haujapata bado
miaka hamsini, nawe umemona Ibrahimu? Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambia, Yeye
Ibrahimu asijakuwako, Mimi niko.” (Yohana 8:47-58)
Katika kisa
tulichokisoma katika maandiko hayo (Yohana 8:47-57) tunajifunza mambo kadhaa
hapo. Tumeona dhahiri jinsi ambavyo hata baadhi ya Wayahudi ilivyo wawia vigumu
sana kumwelewa
huyu Yesu ni nani; hata wakadiriki kusema kuwa Yesu anayo mapepo (mashetani).
Hawakumwelewa kwa sababu walimtazama Yesu kibinadamu kama
jinsi wao walivyo, lakini hawakujua kuwa Yesu ni alikuwepo hata kabla ya Yeye
kuzaliwa na Mariamu. Huyo Ibrahimu anayeongelewa hapo ni yule ambaye habari
zake tunazisoma katika kitabu cha MWANZO cha Biblia (Ibrahimu baba yake Isaka
na Ishmaili). Wayahudi walishangaa; Inawezekanaje huyu Yesu aseme alimwona
Ibrahimu aliyeishi na kufa miaka mingi tena zaidi ya elfu moja iliyopita,
wakati huyu Yesu tumemwona utotoni mwake na hata sasa bado hajatimiza umri wa miaka hamsini? Hayo yalikuwa ni
mawazo ya kibinadamu; tena inaezekana hata wewe ukawa ni miongoni mwa waliokuwa
wanawaza hivyo; lakini, Yesu mwenyewe anatuthibitishia kwa kinywa Chake kwa
kusema:
“...Amin,
amin, nawaambia, Yeye Ibrahimu asijakuwako, Mimi niko.” (Yohana 8:58)
Pia Yesu amewaambia Wayahudi kuwa huyo ambaye
wao wanamwita Mungu (YEHOVA), Yeye ndiye Baba wa Yesu; tena Yesu anamjua ingawa
hao Wayahudi hawamju (Yohana 8:54,55). Vile vile tusomapo kitabu cha MITHALI
tunaona habari zinazo mhusu huyu Yesu; imeandikwa kwamba:
“BWANA
alikuwa nami katika mwanzo wa njia yake. Kabla ya matendo Yake ya kale. Nalitukuka
tokea milele, tangu awali, Kabla haijawako dunia. Wakati visipokuwapo vilindi
nalijidhihirisha... (...I was brought forth... – NKJV)...” (Mithali 8:22-24)
Usomapo
Biblia ya Kiswahili; hapo nilipoandika “...Wakati visipokuwapo vilindi
NALIJIDHIHIRISHA...” utaona baadhi ya Biblia za Kiswahili zimeandika
“...NALIZALIWA...” lakini maana halisi hapo ni “...I was brought forth...”
ambayo tafsiri yake ni “...NALIJITOKEZA...” au “...NALIJIDHIHIRISHA...”
Kumbuka kuwa Wayahudi walimtambua Mungu kwa jina "YEHOVA" ambalo mara nyingi walitamka kwa kusema "BWANA." Hapo Biblia Takatifu inamtaja huyu Yesu likuwa pamoja na YEHOVA katika mwanzo wa njia za YEHOVA. Kabla ya YEHOVA kuumba cho chote (...matendo ya kale...) huyu Yesu alikuwepo. Hivyo basi; huyu Yesu alikuwapo “...tokea milele,
tangu awali, Kabla haijawako dunia.” (Mithali 8:23) Neno “MILELE” maana yake ni
wakati ambao hauna mwanzo wala mwisho; ni wakati usioweza kuhesabika.
Upo
ushahidi mwingi sana
ndani ya Biblia Takatifu unaotuthibitishia kuwa Yesu alikuwepo hata kabla ya
kuumbwa kitu cho chote kile; kwani nao manabii pia walitabiri ujio wa Yesu
ambaye alikuwepo tangu milele yote, na tena manabii hao walisema wazi wazi
kuwa huyu Yesu ni Mungu. Unabii huo ni kama
ifuatavyo:
ü Yesu atazaliwa katika
mji wa Bethlehemu.
Biblia
Takatifu inasema kwamba:
“Bali wewe, Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni
mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika
Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele.”
(Mika 5:2)
Andiko hilo pia linamtaja Yesu
kuwa: “...matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele.” (Mika 5:2)
ü Yesu atazaliwa katika
kabila la Yuda.
Biblia
Takatifu inasema kwamba:
“Fimbo ya
enzi haitaondoka katika Yuda, Wala mfanya sheria kati ya miguu yake, Hata
atakapokuja Yeye, mwenye milki, ambaye mataifa watamtii.” (Mwanzo 49:10)
Hapo
tumeona panasema: “...Hata atakapokuja Yeye, mwenye milki...” ndio maana
tukisoma kitabu cha YOHANA 1:10,11 tunaona pameandikwa kwamba: “Alikuwako
ulimwenguni, hata kwa Yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu
haukumtambua. Alikuja Kwake, wala walio Wake hawakumpokea. Bali wote
waliompokea aliwapa uwezo kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina Lake .” Yesu ndiye mwenye milki ya ulimwengu huu
tunaouishi.
ü Manabii walisema Yesu
atazaliwa na bikira.
Biblia
Takatifu inasema kwamba:
“Kwa hiyo
Bwana mwenyewe atawapa ishara: Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa Mtoto
mwanamume, naye atamwita jina Lake
Imanueli .” (Isaya 7:14)
Jina
“IMANUELI” maana yake ni “Mungu pamoja na wanadamu.”
ü Pia manabii walisema Yesu
ni Mungu.
Biblia
Takatifu inasema kwamba:
“Maana kwa
ajili yetu Mtoto amezaliwa, Tumepewa Mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme
utakuwa begani Mwake; Naye ataitwa jina Lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye
nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani. Maongeo ya enzi yake na amani
hayatakuwa na mwisho kamwe...” (Isaya 9:6,7)
Upo
ushahidi mwingi sana
ndani ya Biblia Takatifu unaotuthibitishia Uungu wa Yesu pamoja na umilele wa
uwepo Wake wa tangu zamani hata baadae.
Sifa
nyingine ya cheo cha Mungu ni hii ifuatayo:
B. Yesu Kristo ameumba
mbingu, nchi, watu, na ulimwengu wote.
Biblia
Takatifu inatuambia kwamba:
“...tuliumbwa
katika Kristo Yesu...” (Waefeso 2:10)
Ni jambo lililo wazi kabisa kuwa sisi wanadamu
wote pamoja na viumbe vyote ni kazi ya mikono ya Yesu. Yesu ameumba vitu vyote;
tendo la mtu kuukana Uungu wa Yesu ni jambo la kumkosea heshima Mungu
aliyekuumba. Ndio maana Yesu aliwaambia Wayahudi kwamba: “...ninyi mwanivunjia
heshima Yangu...” (Yohana 8:49).
Tusomapo Biblia Takatifu katika kitabu cha
YOHANA sura ya kwanza, tunaona pameandikwa:
“Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu...
Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo Yeye hakikufanyika cho chote
kilichofanyika... Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona
utukufu Wake, utukufu kama wa Mwana pekee
atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.” (Yohana 1:1,3,14)
Huyo “Neno” anayetajwa hapo ndiye Yesu Kristo.
Mwandishi wa kitabu hicho cha YOHANA ametumia usemi wa: “...Neno alikuwako kwa
Mungu...” akiwa anawafahamisha hususani Wayahudi waliokuwa wanajua kuwa YEHOVA
ndiye Mungu wao. Kwa hiyo Yohana anasema “...Neno alikuako kwa Mungu...” kwa
maana ya kwamba; huyu “...Yesu alikuwako kwa YEHOVA...” ambaye wao Wayahudi
walimtambua kuwa ndiye Mungu wao.
Pia zaidi tunaona Yohana anafafanua kwa kusema
kuwa; huyu “...Yesu alikuwa Mungu...” Ufafanuzi zaidi tunauona katika YOHANA
1:14 ambapo Yohana amefafanua kwa kusema; “...Yesu alifanyika mwili; akakaa kwetu...”
Biblia Takatifu inamtaja kwa wazi kabisa kuwa Yesu ni Mungu na ameumba vitu
vyote “...Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo Yeye hakikufanyika cho chote
kilichofanyika...” (Yohana 1:3).
Sifa nyingine ituthibitishiayo kuwa Yesu ni
Mungu; ni hii ifuatayo:
C. Yesu Kristo anayo amri
na mamlaka ya kusamehe dhambi.
Kuna jambo
lililowahi kutokea hadi likawashangaza watu; hebu fatilia kisa hiki. Biblia
Takatifu inasema kwamba:
“Wakaja watu wakimleta mtu mwenye kupooza,
anachukuliwa na watu wanne. Na walipokuwa hawawezi kumkaribia (Yesu) kwa sababu
ya makutano, waliitoboa dari pale alipokuwapo; na wakiisha kuivunja
wakalitelemsha godoro alilolilalia yule mwenye kupooza. Naye Yesu, alipoiona
imani yao ,
akamwambia yule mwenye kupooza, Mwanangu, umesamehewa dhambi zako. Na baadhi ya
waandishi waliokuwako huko, wameketi, wakifikiri mioyoni mwao,
Mbona huyu anasema hivi? Anakufuru. Ni nani awezaye
kusamehe dhambi isipokuwa mmoja, ndiye Mungu?
Mara Yesu akafahamu rohoni mwake kwamba
wanafikiri hivyo nafsini mwao, akawaambia, Mbona mnafikiri hivi mioyoni mwenu?
Vyepesi ni vipi, kumwambia mwenye kupooza, Umesamehewa dhambi zako, au kusema,
Ondoka, ujitwike godoro lako, uende?
Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu
anayo amri duniani ya kusamehe dhambi – Akamwambia yule mwenye kupooza,
Nakuambia, Ondoka, ujitwike godoro lako uende
nyumbani kwako.
Mara akaondoka, akajitwika godoro lake,
akatoka mbele yao
wote; hata wakastajabu wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, Namna hii hatujapata
kuiona kamwe.” (Marko 2:3-12)
Kwa
Wayahudi uponyaji haukuwa kitu kigeni kwao kwani hata manabii enzi za Agano la
Kale nao walitumia nguvu za Mungu kuponya wagonjwa; lakini, jambo lililoonekana
geni kwa Wayahudi ni kusikia Yesu amesema “...Umesamehewa dhambi zako...”
(Marko 2:5) Kauli hiyo ya Yesu iliwafanya waone kwamba Yesu AMEKUFURU kwa maana
mwenye mamlaka ya kusamehe dhambi ni Mungu pekee. Watu hao walidhani Yesu amekufuru
kwa sababu hawakujua kuwa Yesu ni Mungu ingawa alikuwa ameuvaa mwili wa
kibinadamu kama sisi.
Ukimpokea
Yesu; anakusamehe dhambi zako zote. Haijalishi umetenda dhambi nyingi
kiasi gani; haijalishi hali uliyonayo hivi sasa. Fahamu kwamba Yesu anakupenda.
Neno la Mungu linasema kwamba:
“...asema
BWANA. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana ,
zitakuwa nyeupe kama theluji...” (Isaya 1:18)
Yesu ni
Mungu, endapo ukimpokea atakusamehe dhambi zote ulizozitenda. Yesu anakupenda sana . Hebu leo mpe Yesu
maisha yako ayatawale; Yesu ataiondoa kiu hiyo ya kutenda dhambi ikufanyayo
ushindwe kujizuia kuwaka tamaa mbaya za mwili wako; Yesu atakupatia ulinzi
ambao utazuia pepo wachafu wasiingilie maisha yako; Yesu atakubariki na
kufungua tumbo lako lililokosa mtoto kwa muda mrefu wote huo unaotaabika hata
sasa; Yesu atawarejesha kwako watoto wako ambao wamekataa kukutii hata
wametoweka kwako; Yesu atakupatia uzima na kuyaondoa magonjwa yote hayo
yanayokutesa hata sasa; Yesu atakubariki na kukupatia uzima wa milele.
Kwa kweli
nashindwa kuuelezea kwa ufasaha zaidi upendo wa Yesu juu yako kwa maana wewe ni
wathamani kubwa sana
mbele za Mungu. Mimi nachoweza kukwambia ni kwamba: Yesu anakupenda tena hataki
upotee. Mpe Yesu maisha yako sasa ili ufurahie uzuri wa pendo Lake .
Jambo
jingine lituthibitishialo kuwa Yesu ni Mungu; ni hili lifuatalo:
D. Yesu Kristo Ndiye atanayekuja
kuuhukumu ulimwengu wote siku ya kiyama.
Jambo hili
si mzaha wala uzushi bali ni kweli; Yesu Kristo anakuja kuhukumu ulimwengu
wote. Yesu Kristo ametutamkia kwa kiywa Chake kwa kusema kwamba;
“Tena Baba
hamhukumu mtu ye yote, bali amempa Mwana hukumu yote; ili watu wote wamheshimu
Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba.” (Yohana
5:22,23)
Katika
hukumu siku ya kiyama hatutegemei kumwona YEHOVA akija kuhukumu ulimwengu,
bali, Yesu Kristo ndiye ajaye kuhukumu ulimwengu. Hii itakuwa hivyo ili WATU
WOTE WAMHESHIMU Yesu sawa sawa na jinsi ambavyo wanamheshimu YEHOVA. Hapo ndipo
viumbe vyote watathibitisha kuwa Yesu ni Mungu. Biblia Takatifu inasema kwamba:
“...kwa
jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya
chini ya nchi; kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA...” (Wafilipi
2:10,11)
Hakika Yesu
ni Mungu. Najua hapa huwachanganya baadhi ya watu hata wanaweza kuhoji;
Je! Wapo Miungu
wangapi? Kwa maana tunasikia habari za Mungu Baba, Mungu Mwana, na Mungu Roho
Mtakatifu? Inawezekanaje tuseme Yupo Mungu mmoja wakati hapo tunaona wapo
watatu?
Ni kweli Utatu Mtakatifu wa Mungu umekuwa
mgumu sana kueleweka kwa watu wengi kutokana na mafundisho
dhaifu waliyoyapokea kutoka kwa viongozi wao wa madhehebu yao na imani zao. Je! Utatu Mtakatifu wa Mungu ni
uzushi uliotungwa na wanadamu kwa lengo la kupotosha watu au Biblia Takatifu
inatuthibitishia wazi wazi kuhusu Utatu Mtakatifu wa Mungu? Hebu twende katika neno la
Mungu tuone jinsi lisemavyo.
Biblia Takatifu inatuambia kwamba:
“Kwa maana
wako watatu washuhudiao mbinguni: Baba, Neno, na Roho Mtakatifu; na watatu hawa
ni umoja.” (1 Yohana 5:8 / 1 John 5:7)
Andiko hilo katika Biblia ya New
King James Version inasema “...these three are one.” (1 John 5:7) kwa maana ya
kwamba “...WATATU HAWA NI MMOJA.” Hebu tujiulize; je! Huo umoja wao unaowafanya
watatu hao (YEHOVA, Yesu, na Roho Mtakatifu) hata wote wawe MMOJA ni upi?
Umoja wao upo katika Uungu. Wote watatu wanaungana
kuwa Mungu mmoja kwa maana ya kwamba uumbaji wa vitu vyote umefanywa kwa pamoja na hawa
watatu (yaani; YEHOVA, Yesu, pamoja na Roho Mtakatifu).
Tukirejea katika uumbaji; Neno la Mungu linasema
kwamba:
“Mungu
akasema, Na Tumfanye mtu kwa mfano Wetu, kwa sura Yetu...” (Mwanzo 1:26)
Pindi niliposoma
andiko hilo kwa
umakini nilijiuliza; Mbona Mungu hakusema;
"...Nimfanye
mtu kwa mfano Wangu, kwa sura Yangu..."?
Kwa nini Mungu ametumia maneno "...kwa mfano WETU, kwa sura
YETU..."? Maneno hayo "...WETU..." na "...YETU..." yanadhihirisha hapo kuna zaidi ya mmoja. Je, ni nani
mwingine aliye muumba mwanadamu zaidi ya Mungu?
Wakati nikiwa
ninajiuliza maswali mengi, ndipo Roho Mtakatifu akanifundisha kwamba neno
"Mungu" ni cheo, na sifa zake ndizo tulizojifunza hapo awali. Mungu hufanya kazi katika ushirika ambao
katika Umoja huo ndipo aliumba vitu vyote.
Yesu anakupenda, mpe maisha yako sasa ili
akuokoe. Ni jambo la imani tu, ukiamini ndani ya roho yako na kumkiri Yesu kwa
dhati kwa kinywa chako; hakika hapo hapo unakuwa umeokoka.
Kumpokea Yesu maishani mwako maana yake ni
kukiri kwamba Yesu ni Bwana, Yesu ni Mungu, pamoja na KUKIRI kwamba Yesu pekee ndiye uzima wa
milele wala hakuna kiumbe ye yote yule awezaye kuokoa isipokuwa Yesu pekee
ambaye ni Mungu wetu.
Inawezekana
kabisa ya kuwa wewe unayesoma ujumbe huu hujaokoka - yaani hujampokea Yesu
Kristo ndani ya roho yako kuwa Bwana na
Mwokozi wako; Lakini sasa umeona umuhimu wa kumpokea Yesu Kristo katika maisha
yako.
Naamini
Roho Mtakatifu ameweka fursa hii mikononi mwako kwa mpango maalumu wa Mungu ili
ufike mahali pa kutubu na kuokoka. Wokovu ni kwa ajili ya uponyaji wako ili uwe
na uzima wa milele; kamwe usimtazame huyo aliye pembeni mwako kwamba akisikia
umeokoka atachukia; wala usiisikilize hiyo sauti ikwambiayo ndani ya akili zako kwamba "subiri" Hiyo ni sauti itokayo kwa yule mwovu Shetani ambaye anataka wewe ufe katika dhambi zako. Fahamu kwamba uzima wako wa milele unauandaa sasa; pia
Biblia inasema hakuna neema baada ya kifo; kwa maana imeandikwa:
“Na kama vile watu walivyowekewa kufa mara moja, na baada ya
kufa hukumu.” (Waebrania 9:27)
Mtu akifa
kinachofuata ni hukumu. Asije akatokea mtu akakudanganya kwamba yapo maombi yanayoweza kuwaombea
wafu nao wakasamehewa dhambi zao (mwulize mtu huyo akwambiae hivyo; mwambie akuonyeshe andiko ndani ya Biblia Takatifu linalosema unaweza kumwombea mfu.) Huo ni uongo tena utokao kwa Shetani. Neno la Mungu linasema kwamba:
“Yeye si
Mungu wa wafu, bali wa walio hai. Hivyo mwapotea sana .” (Marko 12:27)
Nakushauri
usiiache neema hii ya wokovu iliyopo mbele yako sasa ikipite. Wakati huu ni wa thamani sana kwako kwa maana huijui kesho wala badae ikoje. Tafakari kwa kina kati
yako wewe na Mungu ni nani anahitaji msaada wa mwenzake. Tubu sasa.
Sikulazimishi ila fanya sawa na kile Mungu anachoshuhudia ndani ya roho yako.
Fahamu kuwa; haiwezekani kuona baraka za Damu ya Yesu bila ya wewe kuokoka.
“Ee
Mungu wangu ulie Mtakatifu. Ninakuja mbele zako. Mimi ni mwenye dhambi. Naomba
unisamehe dhambi zangu zote nilizokukosea katika maisha yangu yote. Ninatubu kwa dhati ya kweli kutoka rohoni mwangu.
Naomba damu ya Yesu Kristo iliyomwagika msalabani kwa ajili yangu initakase
sasa katika roho yangu na nafsi yangu na mwili wangu. Nimefungua moyo wangu.
Bwana Yesu Kristo nakukaribisha ndani yangu. Ingia kwa uwezo wa Roho Wako – Uwe
Bwana na Mwokozi wangu kuanzia sasa na siku zote. Nakuomba unifanye niwe vile
utakavyo mimi niwe. Ahsante kwa kunisamehe na kwa kuniokoa. Nimejitoa kwako
nikutumikie katika siku zote za maisha yangu. Shetani hana mamlaka tena juu
yangu katika jina la Yesu Kristo. Amina."
Ikiwa
umesoma sala hii kwa kukusudia kabisa na kwa imani, basi wewe umeokoka na
dhambi zako zote zimesamehewa kabisa. Damu ya Yesu iko juu yako sasa.
Baada ya kuokoka
Unapoanza
maisha haya mapya katika Yesu Kristo nakushauri mambo yafuatayo:
(a)
Zungumza na Mungu kwa maombi kila siku (Yohana 15:7).
(b)
Soma Neno la Mungu (Biblia) kila siku (Matendo ya Mitume 17:11).
(c)
Mruhusu Roho Mtakatifu akutawale (Wagalatia 5:16-25; Warumi
8:14-17).
(d)
Umtumaini Mungu kwa kila jambo katika maisha yako (1Petro 5:7;
Zekaria 4:6).
(e)
Usiache kukusanyika na kushirikiana na wengine waliompokea Yesu
Kristo kuwa Mwokozi wao ili uimarike zaidi (Waebrania 10:25).
(f)
Ikemee dhambi na ujitenge nayo. Ukiamini, kwa jina la Yesu unaweza
kuishi maisha matakatifu (Yakobo 4:7-8).
(g)
Jidhihirishe wazi kwa watu kwamba wewe umeokoka na pia shuhudia
kwa watu injili (Mathayo 10:32-33; Warumi 1:16).
Hongera kwa
kuokoka, tangu sasa umekuwa kiumbe kipya. Nakutakia baraka tele katika jina la
Yesu Kristo, amina.
Ni mimi mtumishi wa Mungu,
Mwinjilisti Masanja Sabbi.
Ni mimi mtumishi wa Mungu,
Mwinjilisti Masanja Sabbi.