Neno La UZIMA

sparkle effect
Neno la Mungu linasema kwamba;

"...enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, ...na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi..." (Mathayo 28:19-20)

Neno La UZIMA

Huduma hii haipo chini ya Kanisa lo lote, na wala dhehebu lolote lile, bali hii ni huduma ya kuhubiri neno la Mungu pasipo kubagua dini wala imani ya mtu.
Huduma hii ni utekelezaji wa agizo la Bwana Yesu Kristo Mungu wetu ambaye ametuamuru sisi tulio wafuasi Wake tutekeleze agizo la kuhubiri injili kwa mataifa yote. Lengo kuu la huduma hii ni kufundisha "kweli" ya neno la Mungu pasipo kuongeza neno wala kupunguza neno katika neno la Mungu.
Biblia Takatifu inasema;

"Namshuhudia kila mtu ayasikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mtu ye yote akiyaongeza, Mungu atamwongezea hayo mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki." (Ufunuo 22:18)

Duniani leo kumeibuka na kuzuka watu wengi walio watumishi wa Shetani wanaoipotosha kweli ya neno la Mungu na kuwadanganya watu wa Mungu walio wachanga katika imani.
Biblia Takatifu inasema kwamba;

"...wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya Kristo. Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyo wahubiri, na alaaniwe." (Wagalatia 1:7-8)

Mpendwa msomaji; natumai huduma hii itawafungua watu wengi waliofungwa kwenye vifungo mbalimbali vya imani potofu na mapokeo ya kishetani. Yawezekana nawe ukawa ni mmojawapo kati ya wale waliopokea mafundisho potofu kutoka kwa wazazi ama viongozi wako wa kidini; tafadhali usikwazike pindi usomapo na kujifunza masomo mbalimbali yaliyomo ndani ya tovuti hii.
Japokuwa umejifunza mengi kwenye dhehebu / dini yako: lakini fahamu kuwa dini ni mpango wa wanadamu kumtafuta Mungu, bali wokovu ni mpango wa Mungu kumtafuta mwanadamu aliyepotea. Kwa hiyo dini / dhehebu laweza kumpoteza mtu, bali uzima wa mtu upo kwa Mwenyezi Mungu ambaye neno Lake ndilo kweli na uzima. Hebu sasa mkabidhi Mungu kazi ya kukufundisha. Mwambie Mwenyezi Mungu kwamba;

 "Ee Mwenyezi Mungu uliye Bwana wa vyote, najua wanisikia, najua wajua nimepokea mafundisho mbalimbali kutoka kwa watu mbalimbali, na pia ni Wewe pekee ujuaye kama kile nilichofundishwa ni sahihi au nilipotoshwa. Ee Bwana Mungu, ninakukabidhi mwili, roho, na nafsi (akili) yangu, nakuomba uniongoze na kunifundisha kweli yote ya neno Lako takatifu ili nipate kuyatimiza mapenzi Yako; kwa ajili ya sifa na utukufu Wako. Nakuomba unifanye mimi niwe vile utakavyo mimi niwe. Asante Mwenyezi Mungu kwa maana umenisikia, amina." (kama wewe wamwamini Yesu Kristo, waweza kumalizia kwa kusema; "katika jina la Yesu Kristo, amin")

Ni kweli kwamba watu wengi wamepokea mafundisho potofu na kuyaamini pasipo kujitambua kama wao wanapotea, ukizingatia hao viongozi wao wa dini ni watu wanaoonekana kuheshimika sana kwenye jamii waishiyo. Haijalishi ni nani amekuongoza kwenye imani hiyo, na haijalishi mnaheshimiana kwa namna gani. Biblia Takatifu inasema kwamba;
 "Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu." (Mdo 5:29).

Huduma hii haipo kwa ajili ya kujipatia maslihi binafsi, bali ni kwa ajili ya kulihubiri neno la Mungu. Mafundisho haya yote yaliyomo ndani ya huduma hii ninayatoa bure kwa watu wote pasipo kutoza gharama yoyote ile kwa msomaji. Hii ni zawadi kwenu nyote mnaotaka kujifunza neno la Mungu. Najua zipo mbinu nyingi za kunipatia kipato kupitia huduma hii lakini Roho Mtakatifu kaniongoza kutoa mafundisho haya bure kwa kila mtu apendae kujifunza na kuijua kweli kuhusu neno la Mungu.
Ili upate kunufaika na huduma hii pamoja na kulijua neno la Mungu kwa ufasaha; hebu kwanza ng'oa mizizi yote ya Shetani kwenye ufahamu wako. Fahamu kwamba Shetani hapendi uijue na kuifahamu kweli ya neno la Mungu ili uangamie. Je, wazijua tabia za Shetani?

Þ         Shetani umfanya mtu kukataa kusikia na kujifunza kitu tofauti na kile alichofundishwa.

Utasikia sauti ndani yako ikikwambia ondoka, hacha kijufunza, wewe si wa imani hii (Tafadhali mtu asitafasiri vibaya pointi hii kwa maana natambua Shetani huongeza maana mbaya katika tafasiri, nazungumzia kujifunza neno la Mungu na si vinginevyo). Ndugu yangu; penda sana kujifunza kwani katika kujifunza utapata ufahamu mkubwa na kutambua iliyo kweli.
Unapojifunza ndipo unapoweza kujithibitisha kama imani uliyonayo ni sahihi au unapotea; Unapojifunza ndipo unapoweza kufanya maamuzi sahihi ya wewe uamini nini au umwabudu Mungu kwa namna ipi. Hebu tafakari hili: Je, mimi nisingejifunza ningewezaje kukufundisha wewe namna ya kutofautisha imani ya kweli na imani ya uongo?
Biblia Takatifu inasema kwamba;
 "...jaribuni mambo yote; lishikeni lililo jema; jitengeni na ubaya wa kila namna." (1 Wathesalonike 5:21-22)
Þ         Shetani humfanya mtu awe mshabiki wa dini / dhehebu.
Shetani humfanya mtu kuukataa ukweli hata kama mtu huyo anashuhudiwa ndani ya moyo wake kwamba kile anachoelezwa ni ukweli. Shetani humfanya mtu kupandwa hasira na kupata ghadhabu pale mtu huyo aambiwapo ukweli na kutambua hana vigezo vya kuupinga ukweli huo. Badala ya kukiri kwamba unahitaji kubadilika na kuufuata ukweli, lakini Shetani umfanya mtu huyo kushikwa hasira na ghadhabu, na wakati mwingine uleta chuki, uhasama na magomvi.
Þ         Shetani umfanya mtu kupuuzia na kudharau mambo ya msingi hususani yale yahusuyo neno la Mungu.
Shetani umfanya mtu  kumdharau mtumishi wa Mungu amfundishaye neno la Mungu. Yawezekana mtumishi huyo wa Mungu ni mdogo wako wa kuzaliwa au kiumri; yawezekana mlisoma pamoja au mlishirikiana pamoja kutenda mambo mbalimbali (dhambi) kabla mtumishi huyo hajampokea Yesu; yawezekana mtumishi huyo ni mwanao na unamtambua kwa kina madhaifu yale aliyokuwa nayo kabla ya kumpokea Yesu; yawezekana pia unamzidi kiuchumi na hali ya maisha ya kibinadamu.
Usimdharau mtumishi wa Mungu, kwa maana Yeye aliyemtuma ni mkuu kuliko vyote. Usiidharau huduma ya neno la Mungu kwa maana wewe haukuwepo wakati Mungu anamtuma. Na pia si makosa kukosoa endapo ukiona ameenda kinyume na neno la Mungu, ikibidi mkemee waziwazi kama jinsi mtume Paulo alivyomkemea mtume Petro. Nawa mtumishi wa Mungu unapokemewa unapaswa kutubu na kusimama imara kwenye imani ya kweli (hata mimi ukiniona nakengeuka tafadhali nikemee bila woga na kwa mamlaka yote ya jina la Yesu Kristo, kwa maana kwa kufanya hivyo utakuwa umenisaidia kujua kasoro zangu.) Je, ni mtu yupi ajuae sura yake ilivyo pasipo kujitazama kwenye kioo?;
Pia umwombee baraka mtumishi wa Mungu kwa Mwenyezi Mungu ili huduma aliyonayo ikuwe na watu wengi waipokee injili ya Kristo Yesu kama jinsi Yeye alivyotuamuru.
Þ         Shetani hutafuta mbinu za kupotezea muda ili apate sababu za kukuangamiza na ufe bila kutubu. Utasikia sauti ndani yako ikisema "subiri, ngoja kidogo, mbona mapema hebu nitengeneze maisha kwanza alafu nitamtumikia Mungu nikiwa tayari nimeyaweka vizuri maisha yangu". Kama sauti hiyo waisikia akilini mwako tambua hiyo ni sauti ya Shetani, anataka akuangamize na ufe bila kutubu. 
Þ         Shetani uleta uchovu, uvivu, na wakati mwingine usingizi wakati wa kujifunza neno la Mungu. Je! Umewahi kujiuliza ni kwa nini mambo hayo utokea wakati wa kujifunza neno la Mungu na si kwenye kujifunza mambo ya kidunia? Fahamu kwamba yapo majeshi ya pepo wachafu walio wafuhasi wa Shetani ambao hufanya kazi Muda wote ili kuhakikisha watu hawajifunzi neno la Mungu kwa namna yo yote ile. Ili uweze kuzishinda nguvu hizo za Shetani hakikisha kwamba unafanya maombi kwa jina la Yesu kabla ya kuanza kujifunza neno la Mungu.
Þ         Na pia; Shetani utumia watu na mazingira kuwakwaza watu wasijifunze neno la Mungu.
Unaweza kupanga ratiba kwamba ikifika muda fulani ujifunze neno la Mungu, lakini mara kabla ya muda huo kufika unaweza kuona wanakuja rafiki zako ambao wanataka mtoke mkatembee au wakaanzisha mazungumzo yatakayokupotezea lengo lako la kujifunza neno la Mungu. Wakati mwingine Shetani anaweza kutumia mazingira ambayo yatamfanya mtu achoshwe na kazi kiasi kwamba akitaka tu kujifunza neno la Mungu anashindwa na kupitiwa usingizi kutokana na uchovu.
Hizo ni baadhi ya mbinu za Shetani azitumiazo kuwaangamiza watu. Je! Wewe ulikuwa wazitambua mbinu hizo? Je! Wewe umesimama na kusonga mbele kuufikia uzima wa milele au umeanguka na kuachwa njiani? Je! Wazitambua dalili za kufa kiroho?
  1. Kupoteza hamu ya kusoma na kujifunza neno la Mungu (unatumia muda mwingi kuzungumza, kujifunza, na kusoma mambo ya kidunia yasiyoweza kukupatia uzima wa milele).
  2. Kukosa nafasi ya kuudhuria vipindi vya ibada kanisani na maeneo mbalimbali.
  3. Kuacha kushuhudia kweli ya neno la Mungu mbele ya watu wasiyoifahamu kweli (yawezekana unashindwa kwa kuona aibu, kwa kupuuzia, kwa kuwaogopa watu hao, bado unaishi maisha ya dhambi yakufanyayo ukose ujasiri wa kuhubiri neno la Mungu.) Mungu anataka watu jasiri na walio tayari katika wakati wote.
Tambua kwamba, vipo vikwazo vikuu vinne viwafanyao watu wengi wasizione baraka za Mungu maishani mwao, ambavyo ni;
  • Kikwazo cha kwanza ni Shetani na majeshi ya pepo wachafu.
  • Kikwazo cha pili ni wewe mwenyewe unapojidharau na kutotambua thamani yako mbele za Mungu, na unapomwekea Mungu mipaka kwa kuyakataa mabadiliko anayotaka uyafanye ili ufikie baraka Zake. Hebu jiulize; Je! Wewe ukitupwa jehanamu na kukosa uzima wa milele, Mungu atapata hasara kwa kutokuwepo kwako mbinguni au hasara hiyo ni juu yako wewe uliyeambulia mateso ya moto wa milele? 
  • Kikwazo cha tatu ni watu wanaokuzunguka. Watu wanaweza kukudhihaki, kukutenga, na hata kukudharau. Songa mbele na wala usifanye jambo ili usifiwe na wanadamu, bali fanya jambo linalokupatia uhusiano mzuri kati yako na Mwenyezi Mungu.
  • Kikwazo cha nne ni mazingira unayoishi na kufanyia kazi zako za kila siku. Yawezekana unafanya kazi ambayo wewe waona yakupatia faida kubwa kutokana na ufinyu wa fahamu zako. Unahisi ukiiacha kazi hiyo basi utapoteza kipato na kukufanya uyumbe kiuchumi. Hebu jiulize, je! Itakufaa nini uupate ulimwengu wote na kuipoteza roho yako katika mateso ya ziwa la moto?
Hakikisha jua halizami / siku haipiti pasipo kujifunza neno la Mungu. Biblia Takatifu inasema kwamba;

"Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu  katika hekima yote..." (WAKOLOSAI 3:16)

Huo ni utangulizi tu kati ya mengi utakayoweza kujifunza ndani ya tovuti hii na kupitia hiduma hii ya kujifunza neno la Mungu.
Nakutakia baraka tele pindi ujifunzapo neno la Mungu. Roho Mtakatifu akuongoze katika kujifunza kwako. Ahsante kwa kufungua ukurasa huu; ahsante kwa kufungua tovuti hii. Pia endelea kujifunza masomo mazuri yaliyomo ndani ya tovuti hii.
Kumbuka: Wajulishe ndugu, jamaa, na rafiki zako ili nao washiriki baraka hizi za kujifunza neno la Mungu kupitia huduma hii ya Neno La Uzima.

TAHADHARI:

Huduma hii (tovuti hii) hairushwi hewani kwa msaada wa fedha au mchango wa fedha utolewao kwa kuwaomba watu. Jihadhari kwa kuepukana na matapeli watakaosema wanahitaji mchango wa fedha kwa namna yo yote ile ili kuwezesha huduma hii. Endapo likitokea hitaji la namna hiyo; TUTATANGAZA RASMI NDANI YA TOVUTI HII.
Hatutahusika na udanganyifu wo wote ule utakaojitokeza, na pia hatutahusika kulipa fidia ya madai ya fedha zilizotapeliwa kwa namna hiyo.
Ni mimi mtumishi wa Mungu,

             Mwinjilisti Masanja Sabbi.
Mwenyezi Mungu akubariki katika jina la Yesu Kristo, amina.


TUMA KWA RAFIKI :

Twitter FacebookMore

 
Kuhusu Huduma Hii | Masharti Ya Utumiaji Wa Tovuti Hii | Wasiliana Nasi | Tangaza Kupitia Tovuti Hii