Wednesday, May 29, 2013

UTAVUNA ULICHOPANDA !

"Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna. Maana yeye apandaye kwa mwili wake, katika mwili wake atavuna uharibifu; bali yeye apandaye katika Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele." - WAGALATIA 6:7-9

APANDACHO MTU NDICHO ATAKACHOVUNA.

Je! Injili ya KINAFIKI itahubiriwa hata lini? Je! Wewe utashika mafundisho ya KUPOTOSHA hata lini? Je! Mungu anasemaje kuhusu ufalme Wake?

Maswali hayo ni ya muhimu sana kujiuliza, kuyatafakari, na kuyafanyia kazi kwa maana ni ya muhimu sana kwa kila mtu anayetaka heri katika uzima wa milele.
Katika dunia hii wapo watu wa imani mbali mbali; Wapo watu wasioamini uwepo wa Mungu; wapo watu walio na mashaka juu ya imani zao kutokana na kutoyaona matunda ya kuamini kwao; na pia tupo watu tunaoamini uwepo na utendaji wa Mungu bila mashaka yo yote. Yawezekana hao wasioamini na walio na mashaka wamekuwa hivyo kutokana na mafundisho waliyoyapokea katika jamii au katika elimu ya dunia hii. Nakumbuka nimewahi kufundishwa shuleni kuwa: "Mwanadamu alitokana na nyani"; tena nikafundishwa: "Mwanadamu alitokana na mabadiliko ya nchi." Hao wote wafundishao hivyo ndio dunia inawaita kuwa ni WATU WENYE HESHIMA na wanathaminiwa kwa kupewa tuzo nyingi za heshima. Hebu tujiulize:

Je! Hayo wasemayo na kufundisha ni ya kweli? Je! Kizazi chetu tunakipeleka wapi?

Ukweli ni kwamba kila kiumbe kimetokana kwa kazi ya Mungu. Kila mwanadamu aliye hai ni lazima afahamu kuwa:
Þ          Mungu Yupo.
Þ          Shetani yupo.
Þ           Mbingu ipo.
Þ           Jehanum ipo.
Þ          Umilele upo.
Mambo hayo ni muhimu kuyafahamu kwa maana ndiyo yanayokupatia mwelekeo wa hapa ulipo sasa na kule uendako baada ya maisha ya sasa. Kama jinsi kila nchi na taifa la dunia lilivyo na kanuni  / sheria na taratibu zake; vivyo hivyo baada ya maisha ya sasa duniani upo umelele ambao nao unazo taratibu / sheria na kanuni zake. Pia kama jinsi pesa impavyo utukufu na heshima mwanadamu hapa duniani; vivyo hivyo utakatifu ndio unaompa heshima mtu katika umilele wake. Sidhani kama kuna mtu mzima (aliye komaa akili) ambaye hajui kuhusu kifo. Kila mtu mzima anaamini kifo kipo kwa sababu huwa tunawapoteza na tunawazika watu mara kwa mara. Hebu tujiulize: Je! Kwa nini kifo kipo na nini maana ya neno kifo?
Kifo maana yake ni kutengwa. Kipo kifo cha roho; na pia kipo kifo cha mwili. Yawezekana jambo hili likawa jipya kwako, basi leo ni siku yako ya kuufahamu ukweli huu.
      i:          KIFO CHA KIROHO:
Kifo hiki hutokea kwa mwanadamu baada ya kutengwa na Mungu. Mtu huyo anaweza akawa anaonekana kwa macho ya damu ni mzima na tena anatembea lakini mahusiano yake yeye na Mungu yakawa hayapo kabisa. Kufa kiroho maana yake ni kutengwa na Mungu. Mfano mzuri wa kifo hiki ni huu hapa; Tusomapo Biblia Takatifu tunaona Mungu anamwambia Adamu kwamba:
...matunda ya ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.” – MWANZO 2:17
Tukisoma kwa makini agizo hilo la Mungu tunabaini kwamba Mungu amesema: “...SIKU UTAKAPOKULA matunda ya mti huo UTAKUFA HAKIKA.” Hapo Mungu anamaanisha kwamba; tendo hilo la kufa kwa Adamu litafanyika papo hapo mara baada tu ya kula hilo tunda alilokatazwa asile. Kifo hiki kinachozungumziwa hapa ni kifo cha roho ya Adamu kwa kutengwa na Mungu. Kifo hicho kilimpata Adamu papo hapo. Tukisoma Biblia ya King James tunaona hapo inasema: “...in the day that you eat of it you shall surely die.” – (Genesis 2:17) Kwa hiyo; siku hiyo hiyo ambayo Adamu alikula tunda ndiyo siku hiyo hiyo ambayo Mungu alivunja uhusiano nae, ndio maana tunaona baada ya hapo Adamu na mkewe walifukuzwa katika bustani ya Edeni (Mwanzo 3:23).
Kifo cha kiroho si kigeni kwa wasomaji wa neno la Mungu, na wala si kitu cha ajabu kusikia mtu akiwaita watenda dhambi kuwa ni wafu wanaotembea. Ndiyo maana ipo siku ambayo Yesu alimwambia mtu fulani kwamba:
...Nifuate; waache wafu wawazike wafu wao.” – MATHAYO 8:22
Si kwamba Yesu alitamka hivyo kimakosa au kwa bahati mbaya; La! Yesu alikuwa sahihi kabisa kwa maana mtu ye yote yule asiye na mahusiano ya kiroho na Mungu, mtu huyo ni mfu japokuwa anaonekana kwa macho ya damu kuwa anatembea na kuongea. Nami sitakosea kumwita mtu huyo ni maiti inayotembea kwa maana rohoni yeye ni mfu ila tu tunasubiri mwili wake nao ufe tukauzike. Je! Wewe ni mfu au mzima rohoni mwako? Je! Wewe nawe ni maiti inayotembea?
    ii:          KIFO CHA KIMWILI
Kifo hiki humpata mtu baada ya mwili na roho yake kutengana. Hiki si kigeni mbele ya watu wengi nacho huwapata watakatifu na wenye dhambi kwa maana ni lazima mwili na roho vitengane; ndiyo maana Biblia Takatifu inatuambia:
"Basi, dhambi isitawale ndani ya miili yenu ipatikanayo na mauti..." - WARUMI 6:12
Kwa watakatifu tunapatwa na umauti wa miili yetu kutengana na roho zetu lakini kamwe roho zetu hazitatengwa na Mungu milele yote. Siku zote dhanbi ndiyo imeleta kifo cha roho na mwili kwa mwanadamu. Mtu atendapo dhambi papo hapo anakuwa mfu katika roho yake japokuwa mwilini anaonekana anaishi; yaani anakuwa ni maiti inayotembea. Ukubali ama ukatae lakini ukweli ndio huo.
Sasa hebu tujifunze; Je! Nini kinafuata baada ya kifo cha mwili?
Hapo napo tunakuta wapo watu wanaelezea na kuwafundisha watu kama wao wapendevyo. Wapo wanaofundisha kuwa lipo tumaini la msamaha kwa wafu wenye dhambi; na wengine husema mtu akifa anapotea kabisa wala hakuna kitakacho fuata baada ya umauti wake. Tena watu hao utakuta wanajiita "Wakristo" na wanaitumia Biblia; endapo ukiwauliza mafundisho hayo yapo katika andiko gani ndani ya Biblia Takatifu; utawasikia wakikwambia wamefundishwa na mtakatifu fulani. Hapa napo pana shida kubwa tena zaidi ya ile ya upotoshaji wa wanasayansi tuliyoiona hapo juu kuhusu uumbaji wa mwanadamu.
Ukweli ni kwamba hakuna tumaini jema kwa wafu wenye dhambi. Biblia Takatifu inatuambia baada ya kifo hukumu inafuata (Ebr 9:27). Imeandikwa:
"Na kama vile watu walivyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu." - WAEBRANIA 9:27
 Mtu akifa kimwili hesabu ya matendo yake inakuwa imefungwa. Hakuna tumaini kwa watu waliokufa (kimwili) katika dhambi. Siku zote Shetani ni mdanganyifu, anapotosha watu ili waangamie pamoja naye. Kama jinsi Shetani alivyomdanganya Hawa kwamba:
"...Hakika hamtakufa, kwa maana mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya." - MWANZO 3:4-5
Kumbuka kuwa Mungu amesema siku ukila "...UTAKUFA HAKIKA. – (Mwanzo 2:17) Lakini tunaona Shetani naye anasema: "...HAKIKA HAMTAKUFA..." - (Mwazo 3:4) Vivyo hivyo ndivyo hata leo tunaona neno la Mungu linatuambia: "...BAADA YA KUFA HUKUMU." - (Waebrania 9:27); naye Shetani anasema: "...UKIFA KATIKA DHAMBI TUTAKUOMBEA NAWE UTASAMEHEWA."
Kama kweli wewe unazo akili timamu hebu jiulize: Je! Adamu na Hawa walipokaidi agizo la Mungu kwa kumtii Shetani, ni nini kiliwapata? Je! Walikufa au hawakufa?
Siku zote maneno ya Mungu hayana shuruti; wewe mwenyewe kwa ridhaa yako unao uhuru wa kitii au kukaidi agizo la Mungu, lakini Mungu atakuadhibu sawa sawa na jinsi neno Lake linavyosema. Mungu anatuambia kwamba:
"Nazishuhudia mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimeweka mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako; kumpenda BWANA, Mungu wako, kuitii sauti Yake, na kushikamana Naye; kwani hiyo ndiyo uzima wako..." - KUMBUKUMBU LA TORATI 30:19-20
Mungu anasema: "...CHAGUA UZIMA..." na uzima huu unapatikana katika "...kumpenda BWANA, Mungu wako, kuitii sauti Yake, na kushikamana Naye..." Uzima tunaupata kwa Mungu kwa maana Yeye ndiye uzima wa milele. Inakuwaje basi leo watu kwa makusudi kabisa na kwa jeuri kabisa wanakaidi kutii sauti ya Mungu kwa mapokeo ya wanadamu? Sasa umefika wakati ambao tunapaswa tuache INJILI YA KINAFIKI ya kuipaka mafuta dhambi kwa faraja za KINAFIKI. Kama jinsi Mungu alivyokwambia "...CHAGUA..." nami leo nakwambia "UCHAGUZI NI WAKO. UZIMA WAKO AU MAUTI YAKO UNAIANDAA SASA, WEWE MWENYEWE KWA UCHAGUZI WAKO."

Nakumbuka kipindi kile nikiwa Mkatoliki (RC) nilipokea mafundisho mbali mbali; Nilifundishwa kusali sala maalumu kwa ajili ya kuwaombea wafu. Sala hizo zinaitwa "SALA 15 ZA MTAKATIFU BRIGITA WA SWEDEN." Sala hizo zinapatikana katika kitabu chao kiitwacho "MAWARIDI YA SALA" kuanzia ukurasa wa 22 hadi 26. Pia katika huo ukurasa wa 22 tunaona yapo maelezo yafuatayo:
Bila shaka maelezo hayo yanasomeka vizuri kabisa kama jinsi nilivyo ya nukuu kutoka katika kitabu hicho. Na si hivyo tu; bali pia sala hizo zinaendana na ahadi 21 kwa wale watakaozisali; ahadi hizo ndizo zifuatazo kama jinsi zilivyo kataka ukurasa wa 26 wa kitabu hicho:
Kama hauzioni vizuri unaweza kuikuza picha hiyo ili uzisome zote vizuri.
Hapo tumena ahadi ya kwanza wanasema  Yesu atatoa "...ROHO 15 ZA JAMAA ZAO." ambazo zipo TOHARANI. Wakatoliki wanaamini mtu mwenye dhambi akifa anakwenda sehemu inayoitwa TOHARANI kwa ajili ya utakaso wa dhambi zao kutokana na maombezi ya watu waliopo humu duniani. Hivyo wanajipa moyo kwamba hata wakifa katika dhambi zipo sala maalumu za kuwaombea ili wapate msamaha wa dhambi na kisha wakaingia mbinguni katika uzima wa milele.
Mimi sina vita na Wakatoliki wala mtu awaye yote yule; bali vita vyangu ni dhidi ya Shateni na jeshi lake. Mimi sijitafutii wafuasi bali namtangaza Yesu kuwa ndiye njia, kweli, na uzima wa milele. Hakuna wokovu wo wote ule kwa mwanadamu isipokuwa ni kwa kumpokea Yesu na kumkabidhi maisha yako ili akutawale. Mimi sihubiri dhehebu bali namhubiri Yesu. Hakuna dhehebu litakalomwokoa mtu; Wokovu wa mtu upo kwa Yesu pekee (Mdo 4:12).
Mungu amesema baada ya kifo kinachofuata ni hukumu; Je! Wewe ni nani unayetangua neno la Mungu kwa upotoshaji wako? Shetani huwanasa watu katika vitu ambavyo watu huviona vidogo vidogo hata wakavidharau na kuvipuuzia. Je! Umewahi kujiuliza ni dhambi ipi ambayo aliifanya Adamu na Hawa hata mauti ikatupata?
Hakuna dhambi nyingine waliyoifanya Adamu na Hawa isipokuwa ni dhambi ya kutotii neno (agizo) la Mungu. Baada ya ukaidi wao tunaona matokeo yake hata sasa; Je! Unadhani hukumu itakayokupata wewe unaekaidi neno la Mungu itakuwa ni hukumu kubwa na kali kiasi gani? Kama Adamu kwa kutokutii amesababisha kifo kitupate; je! Wewe uliye mwongo, mwizi, mzinzi, mfiraji, mla rushwa, mzulumaji, tapeli, jambazi, n.k. unapaswa hukumu kali kiasi gani? Tambua kuwa Mungu Yupo; Shetani yupo; mbingu zipo; na jehanum kupo. UCHAGUZI NI WAKO. 
Ndugu mpendwa uchaguzi ni wako; kutii sauti ya Mungu ama kutii mapokeo ya wanadamu. Shetani hana mbingu, wala hana nchi, yeye ni kiumbe tu, hata huko jehanum aendako napo Shetani hajapaumba yeye; Shetani hana lo lote la kukupa wewe zaidi ya kukupoteza. Kwa nini basi unakataa kumtii Mungu ambaye ndiye uzima wa milele.
UCHAGUZI NI WAKO WEWE MWENYEWE. Siku ya hukumu utahukumiwa sawa sawa na jinsi ulivyo chagua. Biblia Takatifu inatuambia:
"Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna. Maana yeye apandaye kwa mwili wake, katika mwili wake atavuna uharibifu; bali yeye apandaye katika Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele." - WAGALATIA 6:7-9
UKIPANDACHO SASA NDICHO UTAKACHO KIVUNA. TUBU SASA KWA MAANA NEEMA IPO KWAKO UNGALI BADO UPO HAI KATIKA MWILI. HAKUNA NEEMA BAADA YA KIFO; BAADA YA KIFO NI HUKUMU, NA BAADA YA HUKUMU NI MAISHA YA MILELE (yawezekana milele yako ikawa mbinguni; au pia yawezekana milele yako ikawa katika ziwa la mateso ya moto wa milele). UCHAGUZI NI WAKO. Mungu ni mwenye rehema sana kwa watu watiifu. Haijalishi umetenda dhambi kiasi gani; ukitubu, Mungu anakusamehe dhambi zako zote. Neno la Mungu linatuambia kwamba:
"...Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji..." - ISAYA 1:18
Pia Mungu anatuambia kwamba:
"Amin, amin, nawaambia, Ye yote alisikiaye neno Langu na kumwamini Yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele." - YOHANA 5:24
Mwamini Yesu. Mpe Yesu maisha yako sasa ili akusamehe dhambi zako zote, akuokoe na kukupatia uzima wa milele. Kama unayo nia ya dhati ya kutubu sasa na kumpa Yesu maisha yako sasa hebu sali sala hii kwa dhati kutoka moyoni mwako. Usiiache neema hii ya wokovu ikupite bure. Hujui kama kesho utakuwa hai au umekufa kimwili. Tubu sasa.
Tamka maneno yafuatayo:
"Bwana Yesu, naja kwako. Mimi ni mwenye dhambi. Bwana Yesu, ninaamini kwamba wewe pekee ndiwe Mwokozi. Nakuomba unisamehe dhambi zote nilizozitenda kwa kufahamu na kwa kutokufahamu.
Bwana Yesu, sasa hivi ninayakabidhi maisha yangu Kwako. Ninamkataa Shetani. Bwana Yesu, nakuomba unitakase kwa damu Yako takatifu. Nakuomba uyatawale maisha yangu tangu sasa hata milele. Nakukabidhi maisha yangu uwe Bwana na Mwokozi wangu. Nakuomba unifanye mimi niwe kama jinsi utakavyo mimi niwe; kwa ajili ya utukufu Wako. Amina."
Nami ninamwomba Roho Mtakatifu awe nawe tangu sasa katika jina kuu la Yesu Kristo. Amina.
Ni mimi Mtumishi wa Mungu,
                Mwijilisti Masanja Sabbi.


0 MAONI:

Post a Comment

TUMA KWA RAFIKI :

Twitter FacebookMore

 
Kuhusu Huduma Hii | Masharti Ya Utumiaji Wa Tovuti Hii | Wasiliana Nasi | Tangaza Kupitia Tovuti Hii