Tuesday, July 23, 2013

KANUNI YA KUMJUA MUNGU.

Kanuni ya kumjua Mungu ipo hivi:

Hauwezi kuja kwa Yesu bila kuitwa na YEHOVA ~ (YOHANA 6:44;65); hauwezi kumjua Roho Mtakatifu bila kufundishwa na Yesu ~ (YOHANA 15:26); hauwezi kumpokea Roho Mtakatifu bila kupewa na Yesu ~ (YOHANA 20:22); na hauwezi kwenda kwa YEHOVA bila kuongozwa na Yesu ~ (YOHANA 14:6).

Zingatia kwamba; Pasipo Yesu hauwezi kufanya lolote ~ (YOHANA 15:5); na pia kila mtu asiye na Roho Mtakatifu ndani yake huyo si mwanafunzi wa Yesu. ~ (WARUMI 8:9).

Ni lazima kwanza KUITWA NA YEHOVA, pili KUMPOKEA YESU, na ndipo utakapompata Roho Mtakatifu; Naye Roho Mtakatifu akaapo ndani yako daima ndipo unapata uzima wa milele. 

Inawezekana ukawa jambo hili usilielewa hata ukajiuliza;


NINI MAANA YA KUFUNDISHWA NA YESU? Au NITAWEZAJE KUFUNDISHWA NA YESU?


Maana ya kufundishwa na Yesu ni hivi; Tunaposoma Injili ya Mathayo sura ya 28 tunaona Bwana Yesu anawaambia wanafunzi Wake kwamba:
"...enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi... na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi..." ~ MATHAYO 28:19-20.
Hapo Yesu alikuwa anaongea ana kwa ana na wale wanafunzi ambao walimwona na waliyapokea mafundisho Yake moja kwa moja; lakini tunaona anawaambia waende kufanya mataifa (watu wasiomjua Yeye) ili wawe wanafunzi kwa kuwafundisha kuyashika YOTE ambayo Yesu amawapa amri kuyafanya. Si kwamba kila mmoja wao akafundishe jinsi atakavyo yeye, bali anafundisha kile alichoamriwa na Yesu. Kwa hiyo kwa maana nyepesi ni kwamba Yesu anasema nasi kupitia watu hao.
Hebu chukulia mfano huu mwepesi: Mf. Rais akimpa ujumbe Waziri akahutubie taifa, na Waziri huyo akahutubia kile tu alichoambiwa na Rais pasipo kuongeza neno wala kupunguza neno; je! Hapo si nisawa na Rais kazungumza na taifa kupitia Waziri? Japokuwa anayeongea ni Waziri lakini anasema ujumbe kutoka kwa Rais. Vivyo hivyo nasi tunafundishwa na Yesu kupitia vinywa vya watumishi Wake. Kuna jambo hili zuri najifunza kwa Mtume Paulo, anasema kwamba:
"Kwa maana mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa ninyi, ya kuwa Bwana Yesu usiku ule aliotolewa alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru akaumega, akisema, Huu ndio mwili Wangu ulio kwa ajili yenu..." ~ 1 WAKORINTHO 11:23-24.
Hapo Mtume Paulo anasema: "...mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa ninyi..." Umewahi kujiuliza swali hili;


Je! Mtume Paulo alikuwepo siku ile ambayo Yesu anaumega mkate? Kama hakuwepo; Inakuwaje aseme: "...mimi nalipokea kwa Bwana..."?


Mtume Paulo amepata ujasiri wa kusema “MIMI NALIPOKEA” kwa sababu yeye Paulo alifundishwa na Yesu kupitia watumishi wa Yesu; vivyo hivyo na sisi tu watumishi wa Yesu ambao Yesu Mwenyewe anasema nasi kupitia neno lile ambalo ametuagiza kulisema. Hivyo basi; ninaposema kuwa hauwezi kumjua Roho Mtakatifu bila kufundishwa na Yesu; hapo ninamaanisha kwamba: Yesu Kristo ndiye ametufunulia namna ya kumjua Mungu. Haiwezekani mtu akamkubali Roho Mtakatifu bila ya kwanza kuyakubali mafundisho ya Yesu, kwa maana wote wasiomkubali Yesu kamwe hawawezi kuukubali Utatu Mtakatifu wa Mungu. Bwana Yesu anasema:
"...maana pasipo Mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote." ~ YOHANA 15:5.
Pasipo Yesu haiwezekani kumjua Mungu, na wala haiwezekani kumshinda Shetani. Bwana Yesu ndiye atupaye akili ya kumjua Mungu pamoja na kutufanya sisi kuwa watu wa milki ya Mungu. Kuwa milki ya Mungu maana yake ni kwamba sisi ni mali ya Mungu kwa sababu Mungu yupo nasi na anakaa ndani yetu.

Bwana Yesu anasema kwamba:

"Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu." ~ YOHANA 14:16-17.
Yesu anasema: "... ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui..."
Ulimwengu haumtambui ni kwa sababu ulimwengu umemkataa Yesu kuwa ni Bwana na Mwokozi wao. Ukimkataa Yesu maana yake ni kuyakataa mafundisho Yake; na mtu akiyakataa mafundisho YOTE ya Yesu maana yake mtu huyo anakuwa gizani kwa sababu ameikataa nuru. Ndio maana ulimwengu HAUMTAMBUI Roho Mtakatifu.
Pia Yesu anasema kwamba ulimwengu HAUMWONI Roho Mtakatifu kwa sababu Yeye hakai ndani yao. Kama Roho Mtakatifu hayumo ndani yako kamwe hauwezi kuuona utendaji Wake akikutumia katika maisha yako. Roho Mtakatifu ni Mungu atupatiaye NGUVU za kushinda vita vyote vya mwilini na rohoni. Kwa hiyo ulimwengu hauwezi kumpokea Roho Mtakatifu kwa sababu wenyewe umemkataa Yesu ambaye ndiye atuongozaye kumjua Mungu.
NAMNA YA KUMPOKEA ROHO MTAKATIFU.
Kumpokea Roho Mtakatifu kupo hivi:
Kumpokea Roho Mtakatifu huja tu baada ya mtu KUISIKIA INJILI, KUIAMINI INJILI, KUMKIRI YESU KWA KINYWA CHAKO WEWE MWENYEWE, KUTUBU DHAMBI, na KUMKABIDHI YESU ATAWALE MAISHA YAKO KAMA JINSI APENDAVYO YEYE.

Hiyo ndiyo kanuni ya kumpokea Roho Mtakatifu. Jambo hili halihitaji wewe kujitaabisha au kuanzisha maombi ya kufunga ili Roho Mtakatifu aje kwako. Si hivyo. Kumpokea Roho Mtakatifu huja AUTOMATICALLY kwa njia ya imani bila hata wewe kumbembeleza. Si lazima mtu aweke mikono kichwani mwako ili wewe ujazwe Roho Mtakatifu; wala si lazima mchungaji wako akuombee ili wewe ujazwe Roho Mtakatifu. Japokuwa wapo watu ambao walimpokea Roho Mtakatifu baada ya kuombewa na kuwekewa mikono juu ya vichwa vyao (Mdo 8:17) lakini hiyo SIO KANUNI ambayo ili mtu ampokee Roho Mtakatifu ni lazima afanyiwe hivyo. Huo ni ufunuo tu ambao walipewa kwa wakati huo, lakini sio kanuni ya kujazwa Roho Mtakatifu. Kamwe mafundisho ya Yesu hayatuambii kuwa kumpokea Roho Mtakatifu kunatokana na maombi ya kufunga kwa siku kadhaa. La hasha! Sivyo. Bali kumpokea Roho Mtakatifu huja kwa njia ya IMANI kwa mtu aliyeoshwa dhambi zake kwa damu ya Yesu Kristo. Ni lazima wewe uwe mtakatifu hapo ndipo Roho Mtakatifu atakaa ndani yako. Namna pekee ya kumpokea Roho Mtakatifu ni kumkiri Yesu awe Bwana na Mwokozi wako, pamoja na kuoshwa dhambi zako kwa damu ya Yesu.

Inawezekana hapa hujaelewa, hebu nikufafanulie hivi:

Je! Bwana Yesu aliwawekea mikono wanafunzi Wake ili wampokee Roho Mtakatifu? Je! Yesu alisemaje? Yesu alisema:

  "...Pokeeni Roho Mtakatifu." ~ YOHANA 20:22.
 Ni hivyo tu; na kweli wote walimpokea Roho Mtakatifu (MATENDO 2:4).

Je! Mtume Petro aliweka mikono juu ya Kornelio na juu ya watu wa nyumbani mwake ili wampokee Roho Mtakatifu? Je! Mtume Petro aliwaombea watu hao ili Roho Mtakatifu awashukie?
HAPANA. Bali Biblia inasema kwamba:
"Petro alipokuwa akisema maneno hayo Roho Mtakatifu akawashukia wote waliolisikia lile neno." ~ MATENDO 10:44.
Yeye Mtume Petro alikuwa bize akihubiri, watu wale walipoamini na kuweka tayari mioyo yao kwa ajili ya kumpokea Yesu, ndipo Roho Mtakatifu akashuka na kuweka makao Yake ndani yao. Roho Mtakatifu huweka makao Yake mahali ambapo ndani yake kuna CHAPA YA YESU. Kamwe hakuna mchungaji wala mtumishi ye yote yule wa Mungu awezaye kukuombea ujazwe Roho Mtakatifu endapo kama wewe HAUJAMKIRI YESU AWE BWANA NA MWOKOZI WA MAISHA YAKO. Roho Mtakatifu haamrishwi na mtu kwamba INGIA KWA HUYO au YULE. Yeye Mwenyewe anaingia pale palipotakaswa kwa damu ya Yesu. Hauwezi kumlazimisha bali Yeye anaingia pale ambapo ni patakatifu tu. Kubatizwa au kutobatizwa si hoja Kwake, bali Yeye huutazama kwanza moyo wako kama Yesu ameshaweka makao Yake ndani yako, ndipo na Yeye Roho Mtakatifu huja na kuingia ndani yako. Wapo watu waliompokea Roho Mtakatifu kabla ya kubatizwa, na pia wapo watu waliompokea Roho Mtakatifu baada ya kubatizwa.

Kitu ambacho kinakuwa kizingiti kwa watu wasijazwe Roho Mtakatifu ni KUTOKUAMINI pamoja na DHAMBI kwa ujumla.


Je! Utajuaje kwamba umejazwa Roho Mtakatifu?

Utajua kwamba umejazwa Roho Mtakatifu kwa sababu maisha yako yatabadirika kimwili na kiroho pia.

KWANZA:
Utaona ipo nguvu ndani yako ambayo inakuamrisha ujitenge na dhambi. Kila kilicho dhambi utakatazwa usikifanye; utasikia sauti au nguvu kutoka ndani yako inayokushuhudia kwamba hicho si halali kwako kufanya.

PILI:
Utapata nguvu na hamu ya kujifunza neno la Mungu. Yawezekana hapo awali ulikuwa hauwezi kuomba kwa muda mrefu, au yawezekana ulikuwa haupendi kusikiliza mahubiri, au yawezekana ulikuwa haupendi uhudhulia ibada, au yawezekana ulikuwa haupendi kusoma na kujifunza neno la Mungu; lakini pindi tu Roho Mtakatifu awekapo makao ndani yako utajikuta automatically unampenda Mungu na kupenda kujifunza neno Lake.

TATU:
Utapata nguvu na ujasiri wa kulihubiri neno la Mungu. Katika kuhubiri ni lazima unawafundisha watu wawe wanafunzi wa Yesu; utakutana na changamoto nyingi lakini Roho Mtakatifu atakuwa anakufundisha namna ya kujibu, pia atakupa maarifa ya namna ya kuufikisha ujumbe wa Mungu mahali husika. Utajikuta hofu, woga, pamoja na aibu zinatoweka kabisa. Hauwezi kufanya kazi ya Mungu bila kuwa na Roho Mtakatifu; Ndio maana Yesu aliwaambia wanafunzi wake kwamba:
…nawaleteta juu yenu ahadi ya Baba Yangu; lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu.  LUKA 24:49.
Hapo Yesu anasema: “...KAENI humu mjini, hata MVIKWE UWEZO utokao juu.” Roho Mtakatifu ndiye atupaye UWEZO / NGUVU ya kuitenda kazi ya Mungu.

NNE:
Utaweza kushinda vita vyote dhidi ya Shetani na jeshi lake. Bwana Yesu ametupatia AMRI ya kuharibu kila kazi ya Shetani wala hakuna lo lote litakalotudhuru (Luka 10:19). Tunaziharibu kazi hizo za Shetani kwa kutumia NGUVU na UWEZO wa Roho Mtakatifu anayekaa ndani yetu.

Hivyo ndivyo namna ya kujua kwamba wewe unaye Roho Mtakatifu ndani yako. Nakutakia amani na Baraka tele.

Kila mwanafunzi wa Yesu ni lazima awe na Roho Mtakatifu  ~ (WARUMI 8:9).

Pokea Roho Mtakatifu katika jina la Yesu Kristo. Amina.


2 MAONI:

alamagroup said...

Mungu awabariki

M.S.O.T said...

Mungu aku jazie

Post a Comment

TUMA KWA RAFIKI :

Twitter FacebookMore

 
Kuhusu Huduma Hii | Masharti Ya Utumiaji Wa Tovuti Hii | Wasiliana Nasi | Tangaza Kupitia Tovuti Hii