Kanuni ya kumjua Mungu ipo hivi:
Hauwezi kuja kwa
Yesu bila kuitwa na YEHOVA ~ (YOHANA
6:44;65); hauwezi kumjua
Roho Mtakatifu bila kufundishwa na Yesu ~ (YOHANA 15:26);
hauwezi kumpokea Roho Mtakatifu bila kupewa na Yesu ~ (YOHANA 20:22); na hauwezi kwenda kwa YEHOVA bila
kuongozwa na Yesu ~ (YOHANA
14:6).
Zingatia kwamba;
Pasipo Yesu hauwezi kufanya lolote ~ (YOHANA 15:5);
na pia kila mtu asiye na Roho Mtakatifu ndani yake huyo si mwanafunzi wa Yesu.
~ (WARUMI 8:9).
Ni lazima kwanza KUITWA NA YEHOVA, pili KUMPOKEA YESU, na ndipo utakapompata Roho Mtakatifu; Naye Roho Mtakatifu akaapo ndani yako
daima ndipo unapata uzima wa milele.
Inawezekana
ukawa jambo hili usilielewa hata ukajiuliza;
“NINI MAANA YA KUFUNDISHWA NA YESU? Au NITAWEZAJE
KUFUNDISHWA NA YESU?”
Maana ya kufundishwa na Yesu ni hivi;
Tunaposoma Injili ya Mathayo sura ya 28 tunaona Bwana Yesu anawaambia wanafunzi
Wake kwamba:
"...enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi... na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi..." ~ MATHAYO 28:19-20.
Hapo Yesu
alikuwa anaongea ana kwa ana na wale wanafunzi ambao walimwona na waliyapokea
mafundisho Yake moja kwa moja; lakini tunaona anawaambia waende kufanya mataifa
(watu wasiomjua Yeye) ili wawe wanafunzi kwa kuwafundisha kuyashika YOTE ambayo Yesu amawapa amri kuyafanya. Si kwamba kila mmoja wao
akafundishe jinsi atakavyo yeye, bali anafundisha kile alichoamriwa na Yesu.
Kwa hiyo kwa maana nyepesi ni kwamba Yesu anasema nasi kupitia watu hao.
Hebu chukulia
mfano huu mwepesi: Mf. Rais akimpa ujumbe Waziri akahutubie taifa, na Waziri
huyo akahutubia kile tu alichoambiwa na Rais pasipo kuongeza neno wala
kupunguza neno; je! Hapo si nisawa na Rais kazungumza na taifa kupitia Waziri?
Japokuwa anayeongea ni Waziri lakini anasema ujumbe kutoka kwa Rais. Vivyo
hivyo nasi tunafundishwa na Yesu kupitia vinywa vya watumishi Wake. Kuna jambo
hili zuri najifunza kwa Mtume Paulo, anasema kwamba:
"Kwa maana mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa ninyi, ya kuwa Bwana Yesu usiku
ule aliotolewa alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru akaumega, akisema, Huu
ndio mwili Wangu ulio kwa ajili yenu..." ~ 1 WAKORINTHO 11:23-24.
Hapo Mtume Paulo
anasema: "...mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa ninyi..." Umewahi
kujiuliza swali hili;
Je! Mtume Paulo alikuwepo siku ile
ambayo Yesu anaumega mkate? Kama hakuwepo; Inakuwaje aseme: "...mimi nalipokea kwa Bwana..."?
Mtume Paulo amepata ujasiri wa kusema “…MIMI NALIPOKEA…” kwa sababu yeye Paulo alifundishwa na
Yesu kupitia watumishi wa Yesu; vivyo hivyo na sisi tu watumishi wa Yesu ambao
Yesu Mwenyewe anasema nasi kupitia neno lile ambalo ametuagiza kulisema. Hivyo
basi; ninaposema kuwa hauwezi kumjua Roho Mtakatifu bila kufundishwa na Yesu;
hapo ninamaanisha kwamba: Yesu Kristo ndiye ametufunulia namna ya kumjua Mungu.
Haiwezekani mtu akamkubali Roho Mtakatifu bila ya kwanza kuyakubali mafundisho
ya Yesu, kwa maana wote wasiomkubali Yesu kamwe hawawezi kuukubali Utatu
Mtakatifu wa Mungu. Bwana Yesu anasema:
"...maana pasipo Mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote." ~ YOHANA 15:5.
Pasipo Yesu
haiwezekani kumjua Mungu, na wala haiwezekani kumshinda Shetani. Bwana Yesu
ndiye atupaye akili ya kumjua Mungu pamoja na kutufanya sisi kuwa watu wa milki
ya Mungu. Kuwa milki ya Mungu maana yake ni kwamba sisi ni mali ya Mungu kwa
sababu Mungu yupo nasi na anakaa ndani yetu.
Bwana Yesu anasema kwamba:
"Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu." ~ YOHANA 14:16-17.
Yesu anasema: "... ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui..."
Ulimwengu haumtambui ni kwa sababu
ulimwengu umemkataa Yesu kuwa ni Bwana na Mwokozi wao. Ukimkataa Yesu maana
yake ni kuyakataa mafundisho Yake; na mtu akiyakataa mafundisho YOTE ya Yesu maana yake mtu huyo anakuwa gizani kwa sababu ameikataa
nuru. Ndio maana ulimwengu HAUMTAMBUI Roho Mtakatifu.
Pia Yesu anasema kwamba ulimwengu HAUMWONI Roho Mtakatifu kwa sababu Yeye hakai
ndani yao. Kama Roho Mtakatifu hayumo ndani yako kamwe hauwezi kuuona utendaji
Wake akikutumia katika maisha yako. Roho Mtakatifu ni Mungu atupatiaye NGUVU za kushinda vita vyote vya mwilini na
rohoni. Kwa hiyo ulimwengu hauwezi kumpokea Roho Mtakatifu kwa sababu wenyewe
umemkataa Yesu ambaye ndiye atuongozaye kumjua Mungu.
NAMNA YA KUMPOKEA ROHO MTAKATIFU.
Kumpokea Roho Mtakatifu kupo hivi:
Kumpokea Roho Mtakatifu huja tu baada ya
mtu KUISIKIA INJILI, KUIAMINI INJILI, KUMKIRI YESU KWA KINYWA CHAKO WEWE
MWENYEWE, KUTUBU DHAMBI,
na KUMKABIDHI YESU ATAWALE MAISHA YAKO KAMA JINSI APENDAVYO
YEYE.
Hiyo ndiyo kanuni ya kumpokea Roho
Mtakatifu. Jambo hili halihitaji wewe kujitaabisha au kuanzisha maombi ya
kufunga ili Roho Mtakatifu aje kwako. Si hivyo. Kumpokea Roho Mtakatifu huja AUTOMATICALLY kwa njia ya imani bila hata wewe
kumbembeleza. Si lazima mtu aweke mikono kichwani mwako ili wewe ujazwe Roho
Mtakatifu; wala si lazima mchungaji wako akuombee ili wewe ujazwe Roho
Mtakatifu. Japokuwa wapo watu ambao walimpokea Roho Mtakatifu baada ya kuombewa
na kuwekewa mikono juu ya vichwa vyao (Mdo 8:17)
lakini hiyo SIO KANUNI ambayo ili mtu ampokee Roho Mtakatifu ni
lazima afanyiwe hivyo. Huo ni ufunuo tu ambao walipewa kwa wakati huo, lakini
sio kanuni ya kujazwa Roho Mtakatifu. Kamwe mafundisho ya Yesu hayatuambii kuwa
kumpokea Roho Mtakatifu kunatokana na maombi ya kufunga kwa siku kadhaa. La
hasha! Sivyo. Bali kumpokea Roho Mtakatifu huja kwa njia ya IMANI kwa mtu aliyeoshwa dhambi zake kwa damu
ya Yesu Kristo. Ni lazima wewe uwe mtakatifu hapo ndipo Roho Mtakatifu atakaa ndani
yako. Namna
pekee ya kumpokea Roho Mtakatifu ni kumkiri Yesu awe Bwana na Mwokozi wako,
pamoja na kuoshwa dhambi zako kwa damu ya Yesu.
Inawezekana hapa hujaelewa, hebu
nikufafanulie hivi:
Je! Bwana Yesu aliwawekea mikono wanafunzi Wake ili wampokee Roho Mtakatifu? Je! Yesu alisemaje? Yesu alisema:
Je! Bwana Yesu aliwawekea mikono wanafunzi Wake ili wampokee Roho Mtakatifu? Je! Yesu alisemaje? Yesu alisema:
"...Pokeeni Roho Mtakatifu." ~ YOHANA 20:22.
Ni hivyo tu; na kweli wote
walimpokea Roho Mtakatifu (MATENDO
2:4).
Je! Mtume Petro aliweka mikono juu ya Kornelio na juu ya watu wa nyumbani mwake ili wampokee Roho Mtakatifu? Je! Mtume Petro aliwaombea watu hao ili Roho Mtakatifu awashukie?
HAPANA. Bali Biblia inasema kwamba:
"Petro alipokuwa akisema maneno hayo Roho Mtakatifu akawashukia wote waliolisikia lile neno." ~ MATENDO 10:44.
Yeye Mtume Petro
alikuwa bize akihubiri, watu wale walipoamini na kuweka tayari mioyo yao kwa
ajili ya kumpokea Yesu, ndipo Roho Mtakatifu akashuka na kuweka makao Yake
ndani yao. Roho Mtakatifu huweka makao Yake mahali ambapo ndani yake kuna CHAPA YA YESU. Kamwe hakuna mchungaji wala mtumishi ye yote yule wa Mungu awezaye
kukuombea ujazwe Roho Mtakatifu endapo kama wewe HAUJAMKIRI YESU AWE BWANA NA
MWOKOZI WA MAISHA YAKO. Roho Mtakatifu haamrishwi na mtu kwamba INGIA KWA HUYO au YULE. Yeye Mwenyewe anaingia pale palipotakaswa kwa damu ya Yesu.
Hauwezi kumlazimisha bali Yeye anaingia pale ambapo ni patakatifu tu. Kubatizwa
au kutobatizwa si hoja Kwake, bali Yeye huutazama kwanza moyo wako kama Yesu
ameshaweka makao Yake ndani yako, ndipo na Yeye Roho Mtakatifu huja na kuingia
ndani yako. Wapo watu waliompokea Roho Mtakatifu kabla ya kubatizwa, na pia
wapo watu waliompokea Roho Mtakatifu baada ya kubatizwa.
Kitu ambacho kinakuwa kizingiti kwa watu
wasijazwe Roho Mtakatifu ni KUTOKUAMINI pamoja na DHAMBI kwa ujumla.
Je! Utajuaje kwamba umejazwa Roho
Mtakatifu?
Utajua kwamba umejazwa Roho Mtakatifu
kwa sababu maisha yako yatabadirika kimwili na kiroho pia.
KWANZA:
Utaona ipo nguvu ndani yako ambayo
inakuamrisha ujitenge na dhambi. Kila kilicho dhambi utakatazwa usikifanye;
utasikia sauti au nguvu kutoka ndani yako inayokushuhudia kwamba hicho si
halali kwako kufanya.
PILI:
Utapata nguvu na hamu ya kujifunza neno
la Mungu. Yawezekana hapo awali ulikuwa hauwezi kuomba kwa muda mrefu, au
yawezekana ulikuwa haupendi kusikiliza mahubiri, au yawezekana ulikuwa haupendi
uhudhulia ibada, au yawezekana ulikuwa haupendi kusoma na kujifunza neno la
Mungu; lakini pindi tu Roho Mtakatifu awekapo makao ndani yako utajikuta
automatically unampenda Mungu na kupenda kujifunza neno Lake.
TATU:
Utapata nguvu na ujasiri wa kulihubiri
neno la Mungu. Katika kuhubiri ni lazima unawafundisha watu wawe wanafunzi wa
Yesu; utakutana na changamoto nyingi lakini Roho Mtakatifu atakuwa
anakufundisha namna ya kujibu, pia atakupa maarifa ya namna ya kuufikisha
ujumbe wa Mungu mahali husika. Utajikuta hofu, woga, pamoja na aibu zinatoweka
kabisa. Hauwezi kufanya kazi ya Mungu bila kuwa na Roho Mtakatifu; Ndio maana
Yesu aliwaambia wanafunzi wake kwamba:
“…nawaleteta juu yenu ahadi ya Baba Yangu; lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu.” – LUKA 24:49.
Hapo Yesu
anasema: “...KAENI humu mjini, hata MVIKWE UWEZO utokao juu.” Roho Mtakatifu ndiye atupaye UWEZO /
NGUVU ya kuitenda kazi ya Mungu.
NNE:
Utaweza kushinda
vita vyote dhidi ya Shetani na jeshi lake. Bwana Yesu ametupatia AMRI ya
kuharibu kila kazi ya Shetani wala hakuna lo lote litakalotudhuru (Luka 10:19). Tunaziharibu kazi hizo za Shetani kwa kutumia NGUVU na
UWEZO wa Roho Mtakatifu anayekaa ndani yetu.
Hivyo ndivyo
namna ya kujua kwamba wewe unaye Roho Mtakatifu ndani yako. Nakutakia amani na
Baraka tele.
Kila mwanafunzi wa Yesu ni lazima awe na
Roho Mtakatifu ~ (WARUMI 8:9).
Pokea Roho Mtakatifu katika jina la Yesu
Kristo. Amina.
2 MAONI:
Mungu awabariki
Mungu aku jazie
Post a Comment