Friday, March 21, 2014

Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo...!

"Moyo wa mwenye ufahamu hutafuta maarifa..." - Mithali 15:14.
Ujaze moyo wako kwa UFAHAMU; kwa maana Biblia Takatifu inasema: "Ufahamu ni chemchemi ya uzima kwake aliye nao..." (Mithali 16:22). Moyo wako ujaapo UFAHAMU ndipo utamtukuza Mungu kwa kila tendo na kila neno litokalo katika kinywa chako. Ndio maana Biblia inasema kwamba:
"Moyo wake mwenye hekima hufundisha kinywa chake; Huzidisha elimu ya midomo yake." - Mithali 16:23.
Moyo ndio ufundishao KINYWA cha mtu mwenye HEKIMA. Moyo ndio uongoza MIDOMO ya mtu mwenye HEKIMA; Tena Biblia inasema kwamba: "Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima." (Mithali 4:23).
Je! Nini maana ya MOYO kulingana na Maandiko hayo?
Tunapo zungumzia neno "MOYO" kwa Mujibu wa Biblia Takatifu; upo wakati neno "MOYO" limetumika kumaanisha "ROHO" (mf. Zab 51:10,17; Eze 36:26) ambao ndio undani wa mtu, au uzima wa mtu; Lakini pia kuna wakati neno "MOYO" limetumika kumaanisha "NAFSI au AKILI" ya mtu, ambayo ndiyo NIA ya mtu katika kutenda jambo fulani; na pia kuna wakati neno "MOYO" limetumika kumaanisha "MOYO" wenyewe (kiungo cha mwili).
Sasa basi; katika maandiko hayo tuliyoyasoma hapo awali (Mithali 4:23; 15:14; 16:22,23) neno "moyo" limetumika kumaanisha "NAFSI" au "AKILI" ya mtu. Je! Nini maana ya NAFSI?
Neno nafsi maana yake ni kituo cha maamuzi katika mwili wa binadamu, kinachofanya maamuzi kati ya roho na mwili wa mtu. Nafsi / akili ya mwanadamu ndiyo inayoongoza kile mtu afanyacho; nafsi / akili ya mtu ikijaa mambo yakumchukiza Mungu, ndipo mtu huyo utenda machukizo mbele za Mungu. Je! Wewe akili yako imejaa nini ndani yake?
Akili / nafsi ya mtu ndiyo inabeba NIA ya kila ufanyalo! Biblia inasema kwamba:

"Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu." - Warumi 12:2.
Hapo tunaona Biblia inasema: "...mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu..." Huko kufanywa UPYA katika NIA ni kufanya akili zetu kupokea mambo yampendezayo Mungu ili ufahamu wetu upate kujaa kila jema la kumpendeza Mungu. Akili yako ijaapo neno la Mungu ndipo kinywa na matendo yako yote yatampendeza Mungu. Mambo hayo yajazayo akili ya mtu, ndiyo hayo mtu huyo atayafanya. Haiwezekani kuyajua MAPENZI ya Mungu ikiwa NIA / AKILI / NAFSI yako imeharibika; nafsi / nia / akili ya mtu huweza kujengwa au kuharibiwa kwa kile UNACHOONA / UNACHOTAZAMA, UNACHOGUSA, pamoja na kile UNACHOSIKIA!!! Uwe makini sana katika UONACHO, UGUSACHO, na USIKIACHO.
Je! Ni neno lipi liwezalo kuzigeuza nia zetu? Biblia Takatifu inatuambia kwamba:
"Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu." - (Wakolosai 3:16).
Biblia Takatifu inatuambia: "Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu..." Si kwamba LISIMAME, bali LIKAE kwa wingi ndani yetu. Neno la Bwana Yesu LIKIKAA kwa WINGI NDANI yako ndipo ufahamu wako utajaa uzima na kila jema la kumtukuza Mungu. Nasisitiza tena; Hapa sisemi LISIMAME NDANI YAKO, bali ninasema NENO LA KRISTO LIKAE NDANI YAKO; wala si kukaa tu, bali LIKAE KWA WINGI ndani yako. Upo utofauti kati ya KUSIMAMA, na KUKAA. 
Sasa hebu ruhusu neno la Bwana Yesu Kristo LIKAE NDANI YAKO, ndipo akili / nafsi / nia yako itajaa hekima na chemchemi ya uzima ndani yako.

"Linda AKILI / NIA / NAFSI yako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima."
Akili yako ikiharibika, mwili na roho yako nazo zitaharibikiwa na kupotea!
Nakutakia baraka tele katika jina la Yesu Kristo.


1 MAONI:

Hope in Christ Orphans Center Mbeya Tanzania said...

Somo zuri

Post a Comment

TUMA KWA RAFIKI :

Twitter FacebookMore

 
Kuhusu Huduma Hii | Masharti Ya Utumiaji Wa Tovuti Hii | Wasiliana Nasi | Tangaza Kupitia Tovuti Hii