Sunday, January 28, 2018

BWANA, TUFUNDISHE SISI KUSALI (Luka 11:1)


SALA / MAOMBI
Hili ni tendo ambalo watu wanaoamini humwendea Mungu wakimwabudu, wakifanya toba, wakimshukuru na kumwomba mambo mbali mbali. Sala / Maombi ni mawasiliano ya moja kwa moja kati ya mtu anayeamini na Mungu. Unamweleza Mungu kile kilichomo ndani yako (hatuombi kwa kukariri bali tunasema kile kilichomo ndani yetu); yanaweza kuwa ni sala / maombi binafsi au maombezi kwa ajili ya wengine.

Tunaposoma Biblia katika Injili ya Luka 11:1, mwanafunzi wa Yesu anamwambia Bwana wake kwamba:

“…Bwana, tufundishe sisi kusali…” – Luka 11:1

Kuna jambo la kuzingatia hapa: Kabla ya kuingia katika maombi, ni muhimu sana kutambua kwanini tunaomba, ni nani tunapaswa kumwomba, na kwanini tumwombe yeye; baada ya kufahamu hivyo, hapo ndipo tuingie katika maombi.

1. Tunaomba kwa sababu sisi ni dhaifu, hatujitoshelezi pasipo msaada wa kiroho. Tunahitaji dira, mwongozo na usimamizi ili tuweze kutenda vema. Pia tunasali kwa ajili ya kurudisha shukrani kwa Yeye atutimiziaye haja zetu.

2. Tunapaswa kumwomba Mungu ambaye ndiye muweza wa yote. Sala / Maombi yetu yote yanamwelekea Mungu.  Yeye anaweza kutujibu kwa namna mbalimbali: mf. kupitia watu, viumbe wa kiroho, na hata kupitia mazingira;  hivyo sisi hatutazami ni kwa njia gani tumepokea bali tunatazama ni wapi kimetoka. Kwa hiyo tunamwomba Yeye (Mungu) aliye chanzo cha baraka zetu.

3. Tunamwomba Mungu kwa sababu Yeye ndiye muweza wa yote; vitu vyote vimetoka Kwake na hata sisi ni Wake. Katika Zaburi 33 Biblia inasema,

“…Nchi imejaa fadhili za BWANA. Kwa neno la BWANA mbingu zilifanyika, Na jeshi Lake lote kwa pumzi ya kinywa Chake. – Zab 33:5-6

Hivyo, ni Mungu ndiye aliye chanzo cha baraka zote; sala / maombi yetu yote tunayaelekeza kwake Yeye pekee.

Sasa basi; katika Injili ya Luka11:1 tumeona mwanafunzi wa Yesu akimwomba awafundishe kusali; hebu tazama jinsi Yesu anavyowaambia: “…ninyi salini hivi…” (Mt 6:9), “…Msalipo semeni…” (Lk 11:2), “…Baba yetu uliye mbinguni…” (Mt 6:9; Lk 11:2). Yesu anawaambia sala zao wazielekeze / wazipeleke kwa “…Baba yetu…” (Mungu) aliye mbinguni, na wala si mwingine. Na vile vile Yesu anazidi kutufafanulia kwamba:

“Nanyi mkiomba lo lote kwa jina Langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana.” - Yn 14:13

Tunapaswa kumwomba Mungu kupitia Yesu Kristo (kwa jina la Yesu). Hapo anayetenda ni Yesu ndio maana amesema: “…hilo nitalifanya…” lakini anayetukuzwa ni Mungu Baba. Hapo zingatia point hii: Hatumwombi Yesu ila tunamwomba Mungu Baba kwa jina la Yesu (yaani kupitia Yesu kunapokea kutoka kwa Mungu Baba).
Ndio maana katika Wakolosai 3:17 Biblia inasema:

“Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa Yeye.” - Kol 3:17

Kwa jina la Yesu vipofu wanaona, viwete wanatembea, wafu wanafufuliwa, viziwi wanasikia, na wokovu tumeupata: Lakini shukrani zetu tunazipeleka kwa Mungu Baba kwa majibu ya sala zetu anayotupatia kupitia Yesu Kristo. Nadhani hadi hapo imeeleweka vema.
Hebu sasa tujifunze; ni kwa nini maombi yako yanaweza yasijibiwe?

Kuna mambo matatu yanayofanya maombi yako yasijibiwe:

1. Dhambi (maisha ya dhambi).
2. Kuomba vibaya.
3. Kutokuwa na imani.

1. DHAMBI (MAISHA YA DHAMBI).
Dhambi ndiyo inawatafuna wengi sana kuliko hivyo vingine viwili nilivyovitaja hapo juu. Biblia inasema kwamba:

“Kila atendaye dhambi, afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi.” – 1 Yn 3:4

Tukisoma 2 Kor 6:14 Biblia inasema hakuna urafiki kati ya haki na uasi. Ikiwa kama Mungu anatuambia sisi tusifungamane na waovu kwa namna isiyo sawa sawa; je, si zaidi ya hivyo kwa Mungu? Huwezi kupokea majibu ya maombi yako bila kufanya toba. Kabla ya kuingia kwenye maombi ni lazima kwanza wewe ujitakase (fanya toba ya kweli); na ili Mungu akusamehe nawe pia unapaswa kuwasamehe waliokukosea. Biblia inasema,

Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi.” – Kol 3:12-13

tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.” – Efe 4:32

“Jilindeni; kama ndugu yako akikosa, mwonye; akitubu msamehe. Na kama akikukosa mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba, akisema, Nimetubu, msamehe.” – Lk 17:3,4

“Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu. Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu. Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.” – Mk 11:24-26

Kuna umuhimu mkubwa sana kusamehe na kufanya toba ndipo uingie katika maombi; Ndio maana katika Waebrania 12:14, Biblia inasema:

“Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao.” – Ebr 12:14

Utakatifu unatangulia ndipo utapokea haja ya moyo wako. Hata uwe na imani kubwa namna gani, usipojitakasa hayo maombi yako ni sawa na kuupaka rangi upepo. Fanya toba; jinyeyekeze mbele za Mungu kwa toba ya kweli. Usijihesabie haki maana inawezekana umemkosea Mungu bila kujua. Kutenda dhambi sio lazima kuzini tu! Sin means to miss the mark! (kutofanya kwa kiwango ulichopaswa kutenda), na huo ndio uasi kwa maana haujatenda kama jinsi unavyopaswa kutenda.

2. KUOMBA VIBAYA.
Hapa kuna shida kubwa sana; watu hawa naona wapo katika makundi mawili:

i. Wanaoomba kwa tamaa zao na anasa (sio kwa utukufu wa Mungu). Biblia inasema kwamba:

Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu.”  - Yakobo 4:3

ii. Wasiojua nani wamwombe (wanaomba ovyo ovyo tu).
Hapo awali tumejifunza Yesu anasema tumuombe "Baba" katika jina Lake Yesu, hilo atafanya (Yohana 14:13); kwa maana nyepesi ni kwamba usipomwomba Mungu Baba kwa jina la Yesu hilo halifanyi, unakuwa unapoteza muda tu, na hata ukijibiwa unapokea kutoka kwa Shetani. Kuna watu wamefundishwa vibaya; utona wapo watu wanamwomba Mungu kupitia Maria, Yosefu n.k. hayo mapokeo yakijinga inabidi watu wajiepushe nayo. Tunapaswa kumwomba Mungu Baba kwa jina la Yesu, sio namna nyingine yoyote ile.

3. KUTOKUWA NA IMANI.
Unapoomba amini tayari umepokea hata kama unaona katika ulimwengu wa mwili hali bado haijabadilika. Biblia inasema,

“…imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana.” – Ebr 11:1

Kuamini hakusubiri matokeo mwilini; bali katika roho tayari umepokea alafu matokeo ya mwilini yatafuata. Bwana Yesu anasema,

“…Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.” – Mk 11:24

Napenda kuhitimisha somo hili kwa mfano ufuatao, Biblia inasema kwamba:

“Hata asubuhi yake walipotoka Bethania aliona njaa. Akaona kwa mbali mtini wenye majani, akaenda ili labda aone kitu juu yake; na alipoufikilia hakuona kitu ila majani; maana si wakati wa tini. Akajibu, akauambia, Tangu leo hata milele mtu asile matunda kwako. Wanafunzi wake wakasikia…
Na asubuhi walipokuwa wakipita, waliuona ule mtini umenyauka toka shinani. Petro akakumbuka habari yake, akamwambia, Rabi, tazama, mtini ulioulaani umenyauka. Yesu akajibu, akamwambia, Mwaminini Mungu. Amin, nawaambia, Ye yote atakayeuambia mlima huu, Ng'oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake. Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.”  - Mk 11:12-14,20-24

Kuna mambo ya muhimu sana kujifunza katika habari hiyo: 1. Yesu aliona njaa. 2. Wakati huo haukuwa msimu wa tini lakini Yesu alitaka apate tini kutoka kwenye huo mtini. Mambo hayo mawili ni mfano halisia wa maisha yetu: Wapo watu wenye njaa (shida / uhitaji), na katika maisha yao wapo katika wakati ambao dunia dunia nzima inasema hali ni ngumu, uchumi ni mgumu, ugonjwa huo hauna tiba; wanajaribu namna mbalimbali ya kujinasua lakini hawaoni matokeo. Hali hiyo ni sawa na jinsi Yesu alivyokuwa na njaa lakini alitaka ale tini wakati ambao sio msimu wa matunda hayo. Sijui kama hapo umenielewa vema.
Yesu aliulaani mtini kisha akaondoka zake, siku ya pili yake waliporudi walikuta ule mtini umekauka. Kuna jambo la kujifunza hapa: mti ule ulikauka pale punde tu alipotamka japokuwa kwa macho ya nyama ulionesha bado haujakauka! Matokeo huanzia katika ulimwengu wa roho alafu ndipo jibu linadhihirika katika ulimwengu wa mwili. Hivyo ndivyo tunapaswa kuwa na imani. Mtu wa haki ukitamka tu tayari papo hapo imetimia, usipoteze muda kusubiri matokeo katika ulimwengu wa mwili.

Bila shaka somo hili limefanyika baraka kwako. Nakutakia baraka tele, Mungu Mwenyezi akubariki katika jina la Yesu Kristo. Amen.
Somo hili limeandaliwa nami Masanja Sabbi (+255756147354). Mungu akubariki sana.

Thursday, January 11, 2018

JIONESHE KUWA MWANAMUME


 JIONESHE KUWA MWANAMUME (1 Wafalme 2:1)

Bwana Yesu Kristo apewe sifa. Ninamshukuru Mungu kwa neema Yake kuu amenipatia kibali cha kulihudumia kanisa Lake hata sasa. Leo ninao ujumbe wenye baraka kwako uliobeba kichwa kinachoitwa: JIONESHE KUWA MWANAMUME. Huu ni mwanzoni mwa mwaka 2018, watu wengi wanatazamia baraka nyingi ziambatane nao; hivyo basi, Roho wa Mungu amenipa ujumbe huu kwa ajili yako: “JIONESHE KUWA MWANAMUME”.
Hebu tufungue Biblia zetu tusome 1 Wafalme 2:1-2, Biblia Takatifu inasema:

Basi siku ya kufa kwake Daudi ikakaribia, akamwusia Sulemani mwanawe, akasema, Mimi naenda njia ya ulimwengu wote (yaani, naenda kufa); basi uwe hodari, ujioneshe kuwa mwanamume…” ~ 1 Wafalme 2:1-2

Mfalme Daudi anamwambia Sulemani mwanawe: “…ujioneshe kuwa mwanamume…” (“…show thyself a man…” - KJV)

Je, nini basi maana ya “…kuwa mwanamume…”? Mwanamue ni mtu asiye ogopa, mtu jasiri mwenye kufanya mambo magumu na shujaa. Kuwa mwanamume sio kijinsia bali ni kuwa jasiri na hodari. Mfalme Daudi alitambua dhahili shujaa ndiye anayetawala wala si mtu mlegevu; hapo alimtaka Sulemani mwanawe awe mtu hodari na jasiri ili aweze kuhimili misukosuko ya utawala unaomkabili. Mfalme Daudi sio tu alimtaka Sulemani mwanawe awe hodari, bali pia AJIONESHE YEYE NI HODARI; yaani watu wamwone na wamtambue yeye ni hodari. Hivyo ndivyo Mungu anavyotaka sisi tuwe hadi ulimwengu utambue uwepo wetu (Luka 10:19).

Watu wengi huwa wanatamani sana kuinuliwa, lakini je umejiandaa kuzikabili changamoto zinazoambatana na baraka hizo? Mara zote unapobarikiwa na kuinuliwa kwa viwango vya juu kunaambatana na kundi la maadui linalokupinga kimwili na kiroho; mf. kuna majambazi, pepo wachafu, wachawi, wasengenyaji na wengine watakuchukia tu kwa sababu wewe umeinuliwa juu kuliko wao. Ndio maana neno la kwanza tumeona Sulemani ameambiwa “…uwe hodari…” (1 Fal 2:2; 1 Nya 28:10, 20) Mtu hodani ni yule mwenye uwezo wa kufanya jambo lililowashinda wengine, mtu mahiri na stadi; anayewaongoza watu kwenda pale wanapopaswa kwenda wala si pale wanapotaka kwenda.

Ukitaka kuvifikia viwango vya juu vya Baraka ni lazima uchague kufanya mambo magumu kwa wengine, usichague mambo mepesi mepesi; bali yafanye mambo magumu kwa umahiri na ustadi mkubwa. Uwe hodari katika kila ufanyalo; iwe katika biashara yako, masomo yako, familia yako, ndoa yako, kazi zako na katika kila utendalo.

Sasa hivi tumeshaingia katika mwaka mpya ambao wengi wanatazamia kuinuliwa zaidi ya mwaka uliopita; Lakini tambua kuwa mwaka mpya ni badiliko la kalenda tu, bali kutamalaki hakupo kwa watu walegevu wala wavivu, ila ni kwa watu walio hodari. Lazima ujioneshe kuwa mwanamume.
Biblia inasema:

Atendaye mambo kwa mkono mlegevu huwa maskini; Bali mkono wake aliye na bidii hutajirisha.– Mithali 10:4

Utofauti kati ya fukara na tajiri upo katika namna yake ya kufikiri na jinsi anavyotenda mambo; ni hivyo tu. Utajiri / kufanikiwa ni uchaguzi wako, hata ufukara / kushindwa pia ni uchaguzi wako pia. Huwezi kukwea ngazi ya kamba iliyoning’inia huku ukiwa umeweka mikono mfukoni mwa suluali yako! Ni lazima ushikilie vizuri ndipo utaweza kuikwea.

Hata mafanikio ya mtu hayaji kizembe, ni lazima uchague kufanya mambo magumu, makubwa yanayowashinda wavivu. Uwe na ndoto kubwa, heshimu malengo yako, uwe jasiri, thubutu kutenda bila woga, fanya kile chenye faida, tunza wakati, epuka marafiki wabaya, uwe na nidhamu ya pesa, weka akiba katika vitu vinavyoongezeka thamani na umtangulize Mungu katika kila ufanyalo. Wakati sahihi wa kufanikiwa ni sasa; anza na hicho ulichonacho: kama ni wazo basi washirikishe watu sahihi, na kama ni mtaji kidogo anza nao uo huo huku ukiwa na mipango ya kufika juu zaidi.

Vile vile tambua kwamba, hauwezi kufanikiwa kwa akili zako mwenyewe tu; ndio maana mfalme Daudi anaendelea kumwambia Sulemani mwanawe, kwamba:

“…uyashike mausia ya BWANA, Mungu wako, uende katika njia Zake, uzishike sheria Zake, na amri Zake, na hukumu Zake, na shuhuda Zake …upate kufanikiwa katika kila ufanyalo, na kila utazamako.” 1 Wafalme 2:3-4

Mweke Mungu mbele ya kila jambo; Ndio maana sisi tunaambiwa: “Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa Yeye. “ – (Wakolosai 3:17). Ukimtumainia Mungu katika yote, hapo ndipo kila utazamako (unachokihitaji) kinakuwa chako. Katika kuomba kwako usiombe kwa tamaa zako, bali kwa ajili ya utukufu wa Mungu (Yakobo 4:3). Lazima Mungu awe na sehemu katika mipango yako, na zingatia kumtolea Mungu sadaka ya shukurani katika mapato yako; si kwa kulazimishwa, bali kwa moyo mkunjufu wa shukurani sawa sawa na jinsi Mungu alivyokubariki. Endapo kama umemuwekea Mungu nadhiri, hakikisha unakuwa mwaminifu katika kuitimiza kwa uhaminifu wote (Hesabu 30:2; Kumb 23:21).
Uwe hodari katika kila lililo jema wala si katika uovu (Zaburi 64:5), ndio maana Biblia inasema:

“…Heri mtu yule amchaye BWANA, Apendezwaye sana na maagizo Yake. Wazao wake watakuwa hodari duniani; Kizazi cha wenye adili kitabarikiwa.” – Zaburi 112:1-2

Hapo zingatia neno hili: “Kizazi cha wenye adili kitabarikiwa.” Hicho ni kizazi kinachomtii Mungu ndicho kinachobarikiwa. Baraka za mcha Mungu hodari zitaambatana naye pamoja na kizazi chake. Sisi Wakristo, tayari Mungu ametubariki wala hakuna laana yoyote ile inayotuandama (1 Petro 2:9). Japokuwa tayari Mungu amekubariki, kama jinsi tunavyosoma katika Kumb 28:2-6

…baraka hizi zote zitakujilia na kukupata usikiapo sauti ya BWANA, Mungu wako. Utabarikiwa mjini, utabarikiwa na mashambani. Utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, na uzao wa wanyama wako wa mifugo, maongeo ya ng'ombe wako, na wadogo wa kondoo zako. Litabarikiwa kapu lako, na chombo chako cha kukandia unga. Utabarikiwa uingiapo, utabarikiwa na utokapo. – Kumb 28:2-6

Lakini baraka hizi utazipata pale USIPOKATA TAMAA. Hakuna mafanikio mepesi, ni lazima kuwa hodari kweli kweli; lazima ujioneshe kuwa mwanamume kweli kweli. Hebu tusome habari hii itakusaidia kukufungua ufahamu wako; katika Mwanzo 26:17-22 Biblia inasema:

Basi Isaka akatoka huko akapiga kambi katika Bonde la Gerari, akakaa huko. Isaka akarudi akavichimbua vile visima vya maji walivyovichimba siku za Abrahamu babaye, maana wale Wafilisti walikuwa wamevifukia baada ya kufa kwake Abrahamu. Naye akaviita majina kufuata majina alivyoviita babaye. Pia watumishi wa Isaka wakachimba katika lile bonde, nao wakapata kisima cha maji yanayobubujika.
Bali wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka, wakisema, “Maji haya ni yetu.” Ndipo akakiita jina la kile kisima Eseki, kwa sababu waligombana naye. Nao wakachimba kisima kingine, wakagombania na hicho tena. Basi akakiita jina lake Sitna. Akaondoka huko na akachimba kisima kingine, wala hicho hawakukigombania. Basi akakiita jina lake Rehobothi, kwa maana alisema, “Kwa kuwa sasa BWANA ametufanyia nafasi, nasi tutazidi katika nchi.” – Mwanzo 26:17-22

Hapo tumejifunza Isaka hakupoteza muda kung’ang’ania kushindana na adui zake, bali yeye alitazama fursa kwingine na kuitumia. Siku zote ukitaka kufika viwango vya juu vya baraka, usipoteze muda kushindana na mtu mpumbavu, bali tazama fursa zilizopo mbele yako alafu piga hatua kuzifuata. Usifanye jambo lisilo na faida kwako, usiupoteze bure wakati wako. Usiishie kulaumu tu, bali tazama fursa zilipo na ujichanganye huko. Baraka za Mungu zinaambata na mtu yule aliyechukua hatua kuzifuata; wala sio kwa kusali tu, wala kwa kufunga na kuomba tu: bali kwa matendo pia. Huwezi kuzifikia baraka zako kwa kuishia kusema “amina” kanisani wala kwa kupewa mafuta ya upako; bali unapaswa utambue tayari Mungu amekwisha kubariki ila kilichobaki ni wewe kuzifuata hizo baraka zako. Hapo ni sawa na mzazi aliyekuwekea chakula ndani, ila wewe umebakiza jukumu lako la kuinuka na kukila pindi unapokihitaji. Tazama wapi fursa zilipo, nawe nenda huko kazifuate ndipo utaifikia baraka yako.

Jambo la mwisho la kuzingatia ninalopenda kukwambia; Tenda mambo kwa busara bila kumdharau mtu awaye yote. Biblia Takatifu inatuambia kwamba:

 “Tazama, Mungu ni hodari, wala hamdharau mtu ye yote; Ana uweza katika nguvu za fahamu.” – Ayubu 36:5

Mungu Mwenyewe ni hodari (yaani, anatenda mambo yanayowashinda wengine) lakini hamdharau mtu ye yote. Hizi mali na utajiri tunaoupata vyote vinatoka Kwake, ni kwa neema Zake tu; hatukuja na kitu duniani na wala hatutaondoka na kitu duniani; hivyo basi tuwahehimu na kuwapenda watu wote, na hata kuwaombea watu walio adui zetu (Luka 6:35; Warumi 12:20).
Tukisoma katika Mithali 17:2 tunaona Biblia inasema:

“Mtumwa atendaye kwa busara atamtawala mwana atendaye mambo ya aibu; Tena atapata sehemu ya urithi kati ya ndugu.” – Mithali 17:2

Zingatia point hii: hapo (Mithali 17:2) imetumia neno "Mtumwa...", kwa kumaanisha "mtu mwovu" (yule asiyemtii wala kumwabudu Mungu wa kweli) akitenda mambo kwa busara ndipo atamtawala "...mwana..."  atendaye mambo ya aibu (mtu wa Mungu aliyekengeuka au afanyaye mambo kivivu).  Kwa hiyo; hapo neno "mtumwa" linamwakilisha "mtu mwovu", na neno "mwana" linamwakilisha "mtu wa Mungu". Hapa ndipo utaweza kuwaona baadhi watu waovu wanafanikiwa na kustawi maishani kuliko wacha Mungu walio wavivu; ndiyo maana hapo Biblia inamalizia kwa kusema kuhusu huyo mtumwa: "..Tena atapata sehemu ya urithi kati ya ndugu.” – (Mithali 17:2) Yaani atamiliki ile sehemu uliyopaswa wewe kuipokea.

Mafanikio au kushindwa vyote vipo katika uchaguzi wako; ikiwa unahitaji kufanikiwa, basi tenda mambo yote kwa busara, hekima na uwe hodari. Hakuna mafanikio yanayokuja kizembe; ni lazima ujioneshe kuwa mwanamume (sio kijinsia, ila katika “attitude” yako – namna yako ya kufikiri na kutenda kama mwana wa mfalme).


Jina langu naitwa Masanja Sabbi (masanjasabbi@gmail.com), nakutakia kheri na baraka tele katika kila utendalo. Malaika wa Mungu akutangulie na kukufanikisha katika jina la Yesu Kristo. Amen.

Wednesday, April 19, 2017

THAWABU YANGU NI NINI?


NAWAKUMBUSHA TU WATUMISHI WA MUNGU

"Basi thawabu yangu ni nini? Ni hii, ya kuwa nihubiripo, nitaitoa Injili bila gharama..." - 1 Kor 9:18

Inawezekana andiko hili huwa unalipita au haujawahi kulisoma; lakini leo napenda kukukumbusha mtu wa Mungu, kabla ya kuingia kwenye huduma, ni vema ukazingatia andiko hili.

Mbarikiwe sana watu wa Mungu.

TUMA KWA RAFIKI :

Twitter FacebookMore

 
Kuhusu Huduma Hii | Masharti Ya Utumiaji Wa Tovuti Hii | Wasiliana Nasi | Tangaza Kupitia Tovuti Hii