"Mtu awaye yote asiudharau ujana wako, bali uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi... ufanye bidii katika kusoma na kuonya na kufundisha." ~ 1 Timotheo 4:12-13.Ewe Mtumishi wa Yesu Kristo unaambiwa kwamba: "...ufanye bidii katika KUSOMA na KUONYA na KUFUNDISHA."
Jitahidi kila siku unatenga nafasi ya KUSOMA neno la Mungu; kwa sababu hauwezi kulifundisha neno kwa ufasaha bila ya KUSOMA. Na pia unaposoma ni lazima utafakari; je! Ni kitu gani hicho usomacho? Kusoma maana yake ni KUJIFUNZA. Si kila kitu kinakufaa wewe kujifunza. Hakikisha unajifunza mema ili uweze kuzaa mema. Kila kiingiacho akilini mwako kwa wingi ndicho hicho kinacho jaza moyo wako, na ndicho kiutiao najisi mwili wako au kiletacho baraka kwako. Zingatia sana kile uonacho, usikiacho, na ujifunzacho kiwe chema. Kujifunza ndio chanzo cha maarifa; kuwa makini na hicho ujifunzacho.
Katika KUONYA; Hauwezi kuonya bila ya kuwa na uhakika wa onyo ulitoalo. Ukisoma / ukijifunza neno la Mungu hakika utayajua mapenzi Yake. Hapa tunagundua kuwa hata kuonya vema kunatokana na KUJIFUNZA mema. Tumia mamlaka sahihi, kwa wakati sahihi, na mahali sahihi.
Pia katika KUFUNDISHA; napo hauwezi kuwa mwalimu mzuri kama wewe ulikuwa mwanafunzi MBAYA. Lazima uzingatie; je! Unajifunza nini? Pia je! Unafundisha nini?
Ewe Mtumishi wa Yesu Kristo unaambiwa kwamba: "...ufanye bidii katika KUSOMA na KUONYA na KUFUNDISHA."
UJUMBE HUU NI WAKO.
Nakutakia huduma njema katika jina la Yesu Kristo. Amen.
0 MAONI:
Post a Comment