JIONESHE KUWA MWANAMUME (1 Wafalme 2:1)
Bwana Yesu Kristo apewe sifa. Ninamshukuru Mungu kwa neema Yake kuu amenipatia kibali cha kulihudumia kanisa Lake hata sasa. Leo ninao ujumbe wenye baraka kwako uliobeba kichwa kinachoitwa: JIONESHE KUWA
MWANAMUME. Huu ni mwanzoni mwa mwaka 2018, watu wengi wanatazamia baraka nyingi ziambatane nao; hivyo
basi, Roho wa Mungu amenipa ujumbe huu kwa ajili yako: “JIONESHE KUWA MWANAMUME”.
Hebu tufungue Biblia zetu tusome 1 Wafalme 2:1-2, Biblia Takatifu
inasema:
“Basi siku ya kufa kwake Daudi ikakaribia, akamwusia
Sulemani mwanawe, akasema, Mimi naenda njia ya ulimwengu wote (yaani, naenda
kufa); basi uwe hodari, ujioneshe kuwa mwanamume…” ~ 1 Wafalme 2:1-2
Mfalme Daudi anamwambia Sulemani mwanawe: “…ujioneshe kuwa mwanamume…”
(“…show thyself a man…” - KJV)
Je, nini basi maana ya “…kuwa mwanamume…”? Mwanamue ni
mtu asiye ogopa, mtu jasiri mwenye kufanya mambo magumu na shujaa. Kuwa
mwanamume sio kijinsia bali ni kuwa jasiri na hodari. Mfalme Daudi alitambua
dhahili shujaa ndiye anayetawala wala si mtu mlegevu; hapo alimtaka Sulemani
mwanawe awe mtu hodari na jasiri ili aweze kuhimili misukosuko ya utawala
unaomkabili. Mfalme Daudi sio tu alimtaka Sulemani mwanawe awe hodari, bali pia
AJIONESHE YEYE NI HODARI; yaani watu wamwone na wamtambue yeye ni hodari. Hivyo
ndivyo Mungu anavyotaka sisi tuwe hadi ulimwengu utambue uwepo wetu (Luka
10:19).
Watu wengi huwa wanatamani sana kuinuliwa, lakini je
umejiandaa kuzikabili changamoto zinazoambatana na baraka hizo? Mara zote unapobarikiwa
na kuinuliwa kwa viwango vya juu kunaambatana na kundi la maadui linalokupinga
kimwili na kiroho; mf. kuna majambazi, pepo wachafu, wachawi, wasengenyaji na
wengine watakuchukia tu kwa sababu wewe umeinuliwa juu kuliko wao. Ndio maana
neno la kwanza tumeona Sulemani ameambiwa “…uwe hodari…” (1 Fal 2:2; 1 Nya
28:10, 20) Mtu hodani ni yule mwenye uwezo wa kufanya jambo lililowashinda
wengine, mtu mahiri na stadi; anayewaongoza watu kwenda pale wanapopaswa kwenda
wala si pale wanapotaka kwenda.
Ukitaka kuvifikia viwango vya juu vya Baraka ni lazima
uchague kufanya mambo magumu kwa wengine, usichague mambo mepesi mepesi; bali
yafanye mambo magumu kwa umahiri na ustadi mkubwa. Uwe hodari katika kila
ufanyalo; iwe katika biashara yako, masomo yako, familia yako, ndoa yako, kazi
zako na katika kila utendalo.
Sasa hivi tumeshaingia katika mwaka mpya ambao wengi
wanatazamia kuinuliwa zaidi ya mwaka uliopita; Lakini tambua kuwa mwaka mpya ni
badiliko la kalenda tu, bali kutamalaki hakupo kwa watu walegevu wala wavivu,
ila ni kwa watu walio hodari. Lazima ujioneshe kuwa mwanamume.
Biblia inasema:
“Atendaye mambo kwa mkono mlegevu huwa
maskini; Bali mkono wake aliye na bidii hutajirisha.” – Mithali 10:4
Utofauti kati ya fukara na tajiri upo katika namna
yake ya kufikiri na jinsi anavyotenda mambo; ni hivyo tu. Utajiri / kufanikiwa
ni uchaguzi wako, hata ufukara / kushindwa pia ni uchaguzi wako pia. Huwezi
kukwea ngazi ya kamba iliyoning’inia huku ukiwa umeweka mikono mfukoni mwa
suluali yako! Ni lazima ushikilie vizuri ndipo utaweza kuikwea.
Hata mafanikio ya mtu hayaji kizembe, ni lazima
uchague kufanya mambo magumu, makubwa yanayowashinda wavivu. Uwe na ndoto
kubwa, heshimu malengo yako, uwe jasiri, thubutu kutenda bila woga, fanya kile
chenye faida, tunza wakati, epuka marafiki wabaya, uwe na nidhamu ya pesa, weka
akiba katika vitu vinavyoongezeka thamani na umtangulize Mungu katika kila
ufanyalo. Wakati sahihi wa kufanikiwa ni sasa; anza na hicho ulichonacho: kama
ni wazo basi washirikishe watu sahihi, na kama ni mtaji kidogo anza nao uo huo
huku ukiwa na mipango ya kufika juu zaidi.
Vile vile tambua kwamba, hauwezi kufanikiwa kwa akili
zako mwenyewe tu; ndio maana mfalme Daudi anaendelea kumwambia Sulemani
mwanawe, kwamba:
“…uyashike mausia ya BWANA, Mungu wako, uende katika
njia Zake, uzishike sheria Zake, na amri Zake, na hukumu Zake, na shuhuda Zake
…upate kufanikiwa katika kila ufanyalo, na kila utazamako.” 1 Wafalme 2:3-4
Mweke
Mungu mbele ya kila jambo; Ndio maana sisi tunaambiwa: “Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo,
fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa Yeye. “ – (Wakolosai
3:17). Ukimtumainia Mungu katika yote, hapo ndipo kila utazamako
(unachokihitaji) kinakuwa chako. Katika kuomba kwako usiombe kwa tamaa zako,
bali kwa ajili ya utukufu wa Mungu (Yakobo 4:3). Lazima Mungu awe na sehemu
katika mipango yako, na zingatia kumtolea Mungu sadaka ya shukurani katika
mapato yako; si kwa kulazimishwa, bali kwa moyo mkunjufu wa shukurani sawa sawa
na jinsi Mungu alivyokubariki. Endapo kama umemuwekea Mungu nadhiri, hakikisha
unakuwa mwaminifu katika kuitimiza kwa uhaminifu wote (Hesabu 30:2; Kumb 23:21).
Uwe
hodari katika kila lililo jema wala si katika uovu (Zaburi 64:5), ndio maana
Biblia inasema:
“…Heri
mtu yule amchaye BWANA, Apendezwaye sana na maagizo Yake. Wazao wake watakuwa
hodari duniani; Kizazi cha wenye adili kitabarikiwa.” – Zaburi 112:1-2
Hapo zingatia
neno hili: “Kizazi cha
wenye adili kitabarikiwa.” Hicho ni kizazi kinachomtii Mungu ndicho
kinachobarikiwa. Baraka za mcha Mungu hodari zitaambatana naye pamoja na
kizazi chake. Sisi Wakristo, tayari Mungu ametubariki wala hakuna laana yoyote
ile inayotuandama (1 Petro 2:9). Japokuwa tayari Mungu amekubariki, kama jinsi
tunavyosoma katika Kumb 28:2-6
“…baraka hizi zote zitakujilia na kukupata
usikiapo sauti ya BWANA, Mungu wako. Utabarikiwa mjini, utabarikiwa na
mashambani. Utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, na uzao wa
wanyama wako wa mifugo, maongeo ya ng'ombe wako, na wadogo wa kondoo zako.
Litabarikiwa kapu lako, na chombo chako cha kukandia unga. Utabarikiwa
uingiapo, utabarikiwa na utokapo.”
– Kumb 28:2-6
Lakini
baraka hizi utazipata pale USIPOKATA TAMAA. Hakuna mafanikio mepesi, ni lazima
kuwa hodari kweli kweli; lazima ujioneshe kuwa mwanamume kweli kweli. Hebu
tusome habari hii itakusaidia kukufungua ufahamu wako; katika Mwanzo 26:17-22
Biblia inasema:
“Basi Isaka akatoka huko akapiga kambi katika Bonde la
Gerari, akakaa huko. Isaka akarudi akavichimbua vile visima vya maji
walivyovichimba siku za Abrahamu babaye, maana wale Wafilisti walikuwa
wamevifukia baada ya kufa kwake Abrahamu. Naye akaviita majina kufuata majina
alivyoviita babaye. Pia watumishi wa Isaka wakachimba katika lile bonde, nao
wakapata kisima cha maji yanayobubujika.
Bali wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa
Isaka, wakisema, “Maji haya ni yetu.” Ndipo akakiita jina la kile kisima Eseki,
kwa sababu waligombana naye. Nao wakachimba kisima kingine, wakagombania na hicho
tena. Basi akakiita jina lake Sitna. Akaondoka huko na akachimba kisima kingine, wala hicho
hawakukigombania. Basi akakiita jina lake Rehobothi, kwa maana alisema, “Kwa
kuwa sasa BWANA ametufanyia nafasi, nasi tutazidi katika nchi.” – Mwanzo
26:17-22
Hapo
tumejifunza Isaka hakupoteza muda kung’ang’ania kushindana na adui zake, bali
yeye alitazama fursa kwingine na kuitumia. Siku zote ukitaka kufika viwango vya
juu vya baraka, usipoteze muda kushindana na mtu mpumbavu, bali tazama fursa
zilizopo mbele yako alafu piga hatua kuzifuata. Usifanye jambo lisilo na faida
kwako, usiupoteze bure wakati wako. Usiishie kulaumu tu, bali tazama fursa
zilipo na ujichanganye huko. Baraka za Mungu zinaambata na mtu yule aliyechukua
hatua kuzifuata; wala sio kwa kusali tu, wala kwa kufunga na kuomba tu: bali
kwa matendo pia. Huwezi kuzifikia baraka zako kwa kuishia kusema “amina”
kanisani wala kwa kupewa mafuta ya upako; bali unapaswa utambue tayari Mungu
amekwisha kubariki ila kilichobaki ni wewe kuzifuata hizo baraka zako. Hapo ni
sawa na mzazi aliyekuwekea chakula ndani, ila wewe umebakiza jukumu lako la
kuinuka na kukila pindi unapokihitaji. Tazama wapi fursa zilipo, nawe nenda
huko kazifuate ndipo utaifikia baraka yako.
Jambo
la mwisho la kuzingatia ninalopenda kukwambia; Tenda mambo kwa busara bila
kumdharau mtu awaye yote. Biblia Takatifu inatuambia kwamba:
“Tazama,
Mungu ni hodari, wala hamdharau mtu ye yote; Ana uweza katika nguvu za fahamu.”
– Ayubu 36:5
Mungu Mwenyewe ni hodari (yaani,
anatenda mambo yanayowashinda wengine) lakini hamdharau mtu ye yote. Hizi mali
na utajiri tunaoupata vyote vinatoka Kwake, ni kwa neema Zake tu; hatukuja na
kitu duniani na wala hatutaondoka na kitu duniani; hivyo basi tuwahehimu na
kuwapenda watu wote, na hata kuwaombea watu walio adui zetu (Luka 6:35; Warumi
12:20).
Tukisoma katika Mithali 17:2
tunaona Biblia inasema:
“Mtumwa atendaye kwa busara
atamtawala mwana atendaye mambo ya aibu; Tena atapata sehemu ya urithi kati ya
ndugu.” – Mithali 17:2
Zingatia point hii: hapo (Mithali 17:2) imetumia neno "Mtumwa...", kwa kumaanisha "mtu mwovu" (yule asiyemtii wala kumwabudu Mungu wa kweli) akitenda mambo kwa busara ndipo atamtawala "...mwana..." atendaye mambo ya aibu (mtu wa Mungu aliyekengeuka au afanyaye mambo kivivu). Kwa hiyo; hapo neno "mtumwa" linamwakilisha "mtu mwovu", na neno "mwana" linamwakilisha "mtu wa Mungu". Hapa ndipo utaweza kuwaona baadhi watu waovu wanafanikiwa na kustawi maishani kuliko wacha Mungu walio wavivu; ndiyo maana hapo Biblia inamalizia kwa kusema kuhusu huyo mtumwa: "..Tena atapata sehemu ya urithi kati ya ndugu.” – (Mithali 17:2) Yaani atamiliki ile sehemu uliyopaswa wewe kuipokea.
Mafanikio au kushindwa vyote vipo katika uchaguzi wako; ikiwa unahitaji kufanikiwa, basi tenda mambo yote kwa busara, hekima
na uwe hodari. Hakuna mafanikio yanayokuja kizembe; ni lazima ujioneshe kuwa
mwanamume (sio kijinsia, ila katika “attitude” yako – namna yako ya kufikiri na
kutenda kama mwana wa mfalme).
Jina langu naitwa Masanja Sabbi
(masanjasabbi@gmail.com), nakutakia kheri na baraka tele katika kila utendalo. Malaika wa
Mungu akutangulie na kukufanikisha katika jina la Yesu Kristo. Amen.
0 MAONI:
Post a Comment