SALA / MAOMBI
Hili ni
tendo ambalo watu wanaoamini humwendea Mungu wakimwabudu, wakifanya toba,
wakimshukuru na kumwomba mambo mbali mbali. Sala / Maombi ni mawasiliano ya
moja kwa moja kati ya mtu anayeamini na Mungu. Unamweleza Mungu kile kilichomo
ndani yako (hatuombi kwa kukariri bali
tunasema kile kilichomo ndani yetu); yanaweza kuwa ni sala / maombi binafsi
au maombezi kwa ajili ya wengine.
Tunaposoma
Biblia katika Injili ya Luka 11:1, mwanafunzi wa Yesu anamwambia Bwana wake
kwamba:
“…Bwana, tufundishe sisi kusali…”
– Luka 11:1
Kuna jambo
la kuzingatia hapa: Kabla ya kuingia katika maombi, ni muhimu sana kutambua kwanini
tunaomba, ni nani tunapaswa kumwomba, na kwanini tumwombe yeye; baada ya
kufahamu hivyo, hapo ndipo tuingie katika maombi.
1. Tunaomba
kwa sababu sisi ni dhaifu, hatujitoshelezi pasipo msaada wa kiroho. Tunahitaji dira,
mwongozo na usimamizi ili tuweze kutenda vema. Pia tunasali kwa ajili ya
kurudisha shukrani kwa Yeye atutimiziaye haja zetu.
2.
Tunapaswa kumwomba Mungu ambaye ndiye muweza wa yote. Sala / Maombi yetu yote
yanamwelekea Mungu. Yeye anaweza
kutujibu kwa namna mbalimbali: mf. kupitia watu, viumbe wa kiroho, na hata
kupitia mazingira; hivyo sisi hatutazami
ni kwa njia gani tumepokea bali tunatazama ni wapi kimetoka. Kwa hiyo
tunamwomba Yeye (Mungu) aliye chanzo cha baraka zetu.
3.
Tunamwomba Mungu kwa sababu Yeye ndiye muweza wa yote; vitu vyote vimetoka
Kwake na hata sisi ni Wake. Katika Zaburi 33 Biblia inasema,
“…Nchi imejaa fadhili za BWANA. Kwa neno la BWANA mbingu
zilifanyika, Na jeshi Lake lote kwa pumzi ya kinywa Chake.” – Zab 33:5-6
Hivyo, ni Mungu ndiye aliye chanzo cha baraka zote; sala /
maombi yetu yote tunayaelekeza kwake Yeye pekee.
Sasa basi; katika Injili ya Luka11:1 tumeona mwanafunzi wa
Yesu akimwomba awafundishe kusali; hebu tazama jinsi Yesu anavyowaambia: “…ninyi salini hivi…” (Mt 6:9), “…Msalipo semeni…” (Lk 11:2), “…Baba yetu uliye mbinguni…” (Mt 6:9; Lk
11:2). Yesu anawaambia sala zao wazielekeze / wazipeleke kwa “…Baba yetu…” (Mungu) aliye mbinguni, na
wala si mwingine. Na vile vile Yesu anazidi kutufafanulia kwamba:
“Nanyi mkiomba lo lote kwa jina Langu, hilo
nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana.” - Yn 14:13
Tunapaswa
kumwomba Mungu kupitia Yesu Kristo (kwa jina la Yesu). Hapo anayetenda ni Yesu
ndio maana amesema: “…hilo nitalifanya…”
lakini anayetukuzwa ni Mungu Baba. Hapo zingatia point hii: Hatumwombi Yesu ila
tunamwomba Mungu Baba kwa jina la Yesu (yaani
kupitia Yesu kunapokea kutoka kwa Mungu Baba).
Ndio maana katika Wakolosai 3:17 Biblia inasema:
“Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo,
fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa Yeye.” -
Kol 3:17
Kwa jina la Yesu vipofu wanaona, viwete wanatembea, wafu
wanafufuliwa, viziwi wanasikia, na wokovu tumeupata: Lakini shukrani zetu
tunazipeleka kwa Mungu Baba kwa majibu ya sala zetu anayotupatia kupitia Yesu
Kristo. Nadhani hadi hapo imeeleweka vema.
Hebu sasa tujifunze; ni kwa nini maombi yako yanaweza
yasijibiwe?
Kuna
mambo matatu yanayofanya maombi yako yasijibiwe:
1.
Dhambi (maisha ya dhambi).
2.
Kuomba vibaya.
3.
Kutokuwa na imani.
1. DHAMBI (MAISHA YA DHAMBI).
Dhambi ndiyo inawatafuna wengi sana kuliko hivyo vingine viwili nilivyovitaja hapo juu.
Biblia inasema kwamba:
“Kila atendaye dhambi, afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi.” – 1 Yn 3:4
Tukisoma
2 Kor 6:14 Biblia inasema hakuna urafiki kati ya haki na uasi. Ikiwa kama Mungu
anatuambia sisi tusifungamane na waovu kwa namna isiyo sawa sawa; je, si zaidi
ya hivyo kwa Mungu? Huwezi kupokea majibu ya maombi yako bila kufanya toba. Kabla
ya kuingia kwenye maombi ni lazima kwanza wewe ujitakase (fanya toba ya kweli);
na ili Mungu akusamehe nawe pia unapaswa kuwasamehe waliokukosea. Biblia
inasema,
“Basi, kwa kuwa
mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu
wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa
na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na
ninyi.” – Kol 3:12-13
“tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma,
mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.” – Efe 4:32
“Jilindeni; kama ndugu yako akikosa,
mwonye; akitubu msamehe. Na kama akikukosa mara saba katika siku moja, na
kurudi kwako mara saba, akisema, Nimetubu, msamehe.” – Lk 17:3,4
“Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali,
aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu. Nanyi, kila msimamapo na
kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni
awasamehe na ninyi makosa yenu. Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu
aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.” – Mk 11:24-26
Kuna
umuhimu mkubwa sana kusamehe na kufanya toba ndipo uingie katika maombi; Ndio
maana katika Waebrania 12:14, Biblia inasema:
“Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu
wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao.”
– Ebr 12:14
Utakatifu
unatangulia ndipo utapokea haja ya moyo wako. Hata uwe na imani kubwa namna
gani, usipojitakasa hayo maombi yako ni sawa na kuupaka rangi upepo. Fanya
toba; jinyeyekeze mbele za Mungu kwa toba ya kweli. Usijihesabie haki maana
inawezekana umemkosea Mungu bila kujua. Kutenda dhambi sio lazima kuzini tu!
Sin means to miss the mark! (kutofanya kwa kiwango ulichopaswa kutenda), na huo
ndio uasi kwa maana haujatenda kama jinsi unavyopaswa kutenda.
2. KUOMBA VIBAYA.
Hapa
kuna shida kubwa sana; watu hawa naona wapo katika makundi mawili:
i.
Wanaoomba kwa tamaa zao na anasa (sio kwa utukufu wa Mungu). Biblia inasema
kwamba:
“Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili
mvitumie kwa tamaa zenu.” - Yakobo 4:3
ii.
Wasiojua nani wamwombe (wanaomba ovyo ovyo tu).
Hapo
awali tumejifunza Yesu anasema tumuombe "Baba" katika jina Lake Yesu,
hilo atafanya (Yohana 14:13); kwa maana nyepesi ni kwamba usipomwomba Mungu
Baba kwa jina la Yesu hilo halifanyi, unakuwa unapoteza muda tu, na hata
ukijibiwa unapokea kutoka kwa Shetani. Kuna watu wamefundishwa vibaya; utona
wapo watu wanamwomba Mungu kupitia Maria, Yosefu n.k. hayo mapokeo yakijinga
inabidi watu wajiepushe nayo. Tunapaswa kumwomba Mungu Baba kwa jina la Yesu,
sio namna nyingine yoyote ile.
3. KUTOKUWA NA IMANI.
Unapoomba
amini tayari umepokea hata kama unaona katika ulimwengu wa mwili hali bado
haijabadilika. Biblia inasema,
“…imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya
mambo yasiyoonekana.” – Ebr 11:1
Kuamini
hakusubiri matokeo mwilini; bali katika roho tayari umepokea alafu matokeo ya
mwilini yatafuata. Bwana Yesu anasema,
“…Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea,
nayo yatakuwa yenu.” – Mk 11:24
Napenda
kuhitimisha somo hili kwa mfano ufuatao, Biblia inasema kwamba:
“Hata asubuhi yake walipotoka Bethania aliona njaa. Akaona
kwa mbali mtini wenye majani, akaenda ili labda aone kitu juu yake; na
alipoufikilia hakuona kitu ila majani; maana si wakati wa tini. Akajibu,
akauambia, Tangu leo hata milele mtu asile matunda kwako. Wanafunzi wake
wakasikia…
Na asubuhi walipokuwa wakipita, waliuona ule mtini umenyauka
toka shinani. Petro akakumbuka habari yake, akamwambia, Rabi, tazama, mtini
ulioulaani umenyauka. Yesu akajibu, akamwambia, Mwaminini Mungu. Amin, nawaambia,
Ye yote atakayeuambia mlima huu, Ng'oka ukatupwe baharini, wala asione shaka
moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake. Kwa sababu
hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo
yatakuwa yenu.” - Mk 11:12-14,20-24
Kuna
mambo ya muhimu sana kujifunza katika habari hiyo: 1. Yesu aliona njaa. 2.
Wakati huo haukuwa msimu wa tini lakini Yesu alitaka apate tini kutoka kwenye
huo mtini. Mambo hayo mawili ni mfano halisia wa maisha yetu: Wapo watu wenye
njaa (shida / uhitaji), na katika maisha yao wapo katika wakati ambao dunia
dunia nzima inasema hali ni ngumu, uchumi ni mgumu, ugonjwa huo hauna tiba;
wanajaribu namna mbalimbali ya kujinasua lakini hawaoni matokeo. Hali hiyo ni
sawa na jinsi Yesu alivyokuwa na njaa lakini alitaka ale tini wakati ambao sio
msimu wa matunda hayo. Sijui kama hapo umenielewa vema.
Yesu
aliulaani mtini kisha akaondoka zake, siku ya pili yake waliporudi walikuta ule
mtini umekauka. Kuna jambo la kujifunza hapa: mti ule ulikauka pale punde tu
alipotamka japokuwa kwa macho ya nyama ulionesha bado haujakauka! Matokeo
huanzia katika ulimwengu wa roho alafu ndipo jibu linadhihirika katika
ulimwengu wa mwili. Hivyo ndivyo tunapaswa kuwa na imani. Mtu wa haki ukitamka
tu tayari papo hapo imetimia, usipoteze muda kusubiri matokeo katika ulimwengu
wa mwili.
Bila
shaka somo hili limefanyika baraka kwako. Nakutakia baraka tele, Mungu Mwenyezi
akubariki katika jina la Yesu Kristo. Amen.
Somo
hili limeandaliwa nami Masanja Sabbi (+255756147354). Mungu akubariki sana.
0 MAONI:
Post a Comment