Tuesday, April 18, 2017

UFUFUKO WA YESU


Je, Ufufuko wa Yesu ndio sikukuu ya Pasaka?
Je, Pasaka na “Easter” ni kitu kimoja?


Maswali hayo huwatatiza watu wengi sana, hivyo basi leo nimependa tujifunze ili tuondokane na utata huo; barikiwa sana na somo hili:

PASAKA
Sikukuu ya Pasaka ilikuwa mpango wa Mungu kwa Waisraeli ili washerehekee kuokolewa kwao kutoka utumwani Misri kwa njia ya miujiza (Kut 12:14,24).

Jina la sikukuu lilikumbusha tendo la malaika wa Mungu “kupita juu” ya nyumba za Waisraeli alipowauwa wazaliwa wa kwanza wa Wamisri (Kut 12:27). Lakini Mungu alihifadhi nyumba za Waisraeli wasipatwe na hukumu ile alipoona damu ya mnyama wa sadaka iliyopakwa kuzunguka mlango mkubwa wa mbele wa nyumba zao. Damu hiyo ilikuwa ishara kwamba uzima usiokuwa na hatia ulitolewa badala ya mtu aliekuwa chini ya hukumu (Kut 12:5,7,12-13,21-23).

Mwezi wa Pasaka uliwekwa kuwa mwezi wa kwanza wa mwaka wa kalenda ya Kiyahudi (Abibu / Nisani ambao ni mwezi March kwenda April katika kalenda ya Gregory).

Baada ya Pasaka, sikukuu ya siku saba ya Mkate Usiotiwa Chachu iliunganishwa na sherehe ya Pasaka; mambo hayo miwili hasa yalihesabiwa kama sikukuu moja (Kum 16:1-8; Mk 14:1). Baada ya kuondoa chachu kutoka nyumba zao kabla ya Pasaka, watu walitunza nyumba zao zisiwe na chachu yo yote kwa juma lingine baada ya Pasaka (Kut 12:14-20). Jambo hili liliwakumbusha kwamba, baada ya kuokolewa kwa njia ya Pasaka, walikimbia kutoka Misri kwa haraka, wakipika mikate isiyochachwa hapo waliposafiri (Kut 12:33-34,39).

Waisraeli walipofika Kanaani, walipaswa kuadhimisha sikukuu ya Pasaka katika mahali maalumu pa ibada tu. Mwanzoni mahali hapo palikuwa Hema la Kukutania, na baadaye palikuwa helalu (Kum 16:5-6; Yos 5:10-12; 2Nya 8:12-13; 30:1; 35:1; Lk 2:41; Yn 2:13; 11:55). Wanaume wote wa Israeli waliokuwa watu wazima walipaswa kuhudhuria sherehe ya Pasaka (Kut 23:14,17), na hata wageni waliweza kusherehekea, mradi tu walipata tohara na hivyo walikuwa sehemu ya watu wa Agano (Kut 12:43-49).

PASAKA KATIKA AGANO JIPYA
Wakati wa Bwana Yesu, sikukuu ya Pasaka ilikuwa kanuni maalumu pamoja na sherehe kadhaa zilizokuwa zimeongezeka. Ingawa watu walichinja mwana-kondoo hekaluni walikula karamu yake binafsi pamoja na marafiki na jamaa (Lk 22:8-13). Kati ya nyongeza zile za karamu kulikuwa na kikombe cha divai ambacho ni kwa ajili yake mkuu wa nyumba alisema sala ya shukrani (au ya baraka, 1 Kor 10:16), ambacho pia alikizungusha kwa wote walioshiriki, kabla ya kula mkate usiochachwa na baada yake pia (Mk 14:22-24; Lk 22:15-20).
Kuimba pia kulikuwa sehemu ya sherehe, washiriki wakiimba nyimbo mbalimbali za Zaburi zilizojulikana kwa “Zaburi za Hallel” (yaani za Haleluya - za kumsifu BWANA, ambazo ni Zaburi 113-118). Kwa kawaida waliimba Zaburi mbili za kwanza kabla ya kula mwana-kondoo na Zaburi nyingine baadaye (Mk 14:26).

Katika Pasaka ya mwisho ya Bwana Yesu, Yeye na wanafunzi Wake walikula karamu siku moja kabla ya wakati wake hasa, na labda pasipo mwana-kondoo (Lk 22:15; Yn 13:1). Inawezekana walifanya hivyo kwa kuwa Yesu alikwisha jua kwamba Yeye mwenyewe wakati huo alikuwa mwana-kondoo wa Pasaka; siku ya kesho yake angetoa maisha Yake wakati ule ule ambao wanyama wangechinjwa kwa maandalizi ya karamu iliyofuata usiku huo (Yn 18:28; 19:14,31,42).

Kifo cha Yesu msalabani kilikuwa tendo kuu la ukombozi ambalo Pasaka ya Waisraeli ilikuwa mfano wake mdogo tu (linganisha Kut 12:5 na 1 Pet 1:18-19, pia Kut 12:46 na Yn 19:36, pia Kut 12:21,27 na 1 Kor 5:7). Baada ya kufa kwake Yesu, Pasaka ya Wayahudi haikuwa na maana tena; iliondolewa na mahali pake sherehe mpya ya ukumbusho iliwekwa, yaani Chakula cha Bwana (Mt 26:17-30; 1 Kor 10:16; 11:23-26).
Hata hivyo, Agano Jipya linataja mahitaji ya Pasaka katika mafundisho ya Kikristo; kwa maana jinsi sikukuu ya Pasaka ilivyokuwa na maana kwamba Waisraeli walipaswa kutoa "chachu" katika nyumba zao, vivyo hivyo sadaka ya Yesu Kristo ina maana kwamba Wakristo wanapaswa kuondoa "dhambi" katika maisha yao (1 Kor 5:7-8).

Je, EASTER ndiyo PASAKA?
Neno “Easter” halipo katika Biblia yo yote ile (ya Kiebrania – Agano la Kale, wala ya Kiyunani – Agano Jipya). Katika maandiko yote ndani ya Biblia Takatifu hakuna sherehe ya “Easter” kwa watu wa Mungu. Tafasiri ya neno “Easter” tunaziona kwenye kamusi mbalimbali zikifafanua kuwa; ni sherehe za Kikristo kuadhimisha ufufuko wa Yesu.
Hebu tutazame nukuu zifuatazo:

"Easter
· n. the festival of the Christian Church celebrating the resurrection of Christ, held (in the Western Church) on the first Sunday after the first full moon following the northern spring equinox.
– ORIGIN OE Uastre, of Gmc origin and rel. to east; perh. from Éastre, the name of a goddess assoc. with spring." –
Oxford Dictionary 10th Edition;

"Easter, annual festival commemorating the Resurrection of Jesus Christ, and the principal feast of the Christian year... a Christian festival, embodies many pre-Christian traditions. The origin of its name is unknown. Scholars, however, accepting the derivation proposed by the 8th-century English scholar St Bede, believe it probably comes from “Ēostre”, the Anglo-Saxon name of a Teutonic goddess of spring and fertility, to whom was dedicated a month corresponding to April. Her festival was celebrated on the day of the vernal equinox; traditions associated with the festival survive in the Easter rabbit, a symbol of fertility, and in coloured Easter eggs, originally painted with bright colours to represent the sunlight of spring, and used in Easter-egg-rolling contests or given as gifts." -
Microsoft ® Encarta ® Encyclopedia 2005.

Neno “Easter” asili yake ni neno “Ēostre” ambalo ni jina la mungu “mke” wa mavuno na uzazi aliyekuwa akiabudiwa (amewekewa wakfu) majira ya kuchipua mimea hususani kipindi cha mwezi April, ambayo pia ndiyo mwezi Nisani kwa Wayahudi ambao waliadhimisha Pasaka.

Sherehe ya “Eostre / Easter” iliambatana na mambo ya kimila; walitoa sadaka ya sungura kama alama ya uzazi, na mayai yaliyopakwa rangi ya mng’ao ili kuwakilisha “jua” ambayo yalitumika katika mashindano ya kupondana mayai, au kutolewa tu kama zawadi.
Sherehe hizo zilitokana na dini ya kale ya Kigiriki, walikuwa na desturi ya kuadhimisha kurudi kwa Persephone binti wa Demeter / Ēostre “mungu wa mavuno” kutoka kuzimu kuja duniani kwenye mwanga wa mchana (return of Persephone, daughter of Demeter, goddess of the earth, from the underworld to the light of day); kurudi kwake “Persephone” kwa Wagiriki wa kale walitafasiri ni ufufuo wa maisha katika kuchipua mimea kipindi cha mwezi April baada ya kuharibiwa na majira ya baridi kali huko kwao. Watu hao waliamani kuwa “mungu” wao mwenye nguvu zote alikwenda kulala wakati wa msimu wa baridi, nao wakafanya sherehe na kucheza muziki katika majira ya kuchipua kwa mimea wakiamini “mungu” wao ameamka toka usingizini, amerudi toka kuzimu.

Lakini, katika Biblia ya lugha ya Kiingereza neno Pasaka limeandikwa: “Passover” likimaanisha “PITA-JUU” kama jinsi tulivyojifunza katika Kut 12:27, malaika wa Mungu alipoziacha nyumba za wana wa Israel kwa kupita juu na kuwaangamiza wazaliwa wa kwanza wa Wamisri.

Sherehe hizo za “Easter” zimeingia kwenye baadhi ya dini za Kikristo kutokana na mapokeo kutoka dini ya kipagani ya Wagiriki wa kale.

Tukirejea katika Biblia; hakuna sherehe za “Easter”, wala Pasaka sio “Easter”. Sherehe hizo za kipagani “Easter” ziliadhimishwa katika majira sambamba na sherehe za Pasaka ya Kiyahudi (mwezi Nisani / April) ambayo pia ndiyo majira Yesu alisulibiwa, kufa na kufufuka.

Mapokeo hayo ya “Easter” ndiyo yameingizwa hata leo katika sherehe za kidini ingawa kiukweli huo ni upagani uliofunikwa mwamvuli wa Ukristo.

Easter sio Ufufuko wa Yesu, wala Easter sio Pasaka ya Kiyahudi.

Ninaamini ujumbe huu umewafungua fahamu watu wengi; nami nakuombea uzidi kubarikiwa katika jina la Yesu Kristo, Amen.

0 MAONI:

Post a Comment

TUMA KWA RAFIKI :

Twitter FacebookMore

 
Kuhusu Huduma Hii | Masharti Ya Utumiaji Wa Tovuti Hii | Wasiliana Nasi | Tangaza Kupitia Tovuti Hii