Monday, September 16, 2013

Uchaguzi wako na uhamuzi wako ndio matokeo ya jinsi ambavyo wewe ulivyo.

Je! Wajua ? ? ?

"MTU ANAKUWA MASIKINI KWA SABABU YEYE MWENYEWE AMECHAGUA AU AMEKUBALI YEYE MWENYEWE KUWA HIVYO." Uchaguzi wako na uhamuzi wako ndio matokeo ya jinsi ambavyo wewe ulivyo.

Bibilia Takatifu inasema kwamba:
"Mtu mvivu hapiki mawindo yake; Bali mwenye bidii anazo mali za thamani." ~ MITHALI 12:27.
Siku zote watu wengi huwa masikini kwa sababu ya UVIVU walio nao. Upo uvivu wa namna tofauti, mfano: Uvivu wa kufikiri; na, Uvivu wa kufanya kazi. Watu wengi ni wavivu wa kufikiri namna ya kufanyia ufumbuzi changamoto mbali mbali wanazokutana nazo maishani; wamekuwa ni wepesi wa kukata tamaa. Wao wanataka kwanza warahisishiwe mambo ndipo wapate wepesi. Hawapendi kabisa kushughulisha akili zao; watu wa namna hiyo hawafanikiwi kwa sababu ya uvivu walio nao.

Tukija kwenye kundi la wavivu wa kufanya kazi; hapa napo wapo watu wengi sana. Watu hawa wamekaa wakisubiri kula kutoka katika kazi za wenzao; hawalimi lakini wao ni wa kwanza kuvuna hata ambavyo havijakomaa; hawapiki lakini wao ni wa kwanza kuuliza kama vimeiva jikoni; wanakataa kuajiriwa lakini wao ndio wa kwanza kuuliza kama mshahara umetoka; hawatafuti chakula lakini wao ndio wa kwanza kulalamika kuwa chakula hakitoshi mezani; na hawataki kujishughulisha lakini wao ndio wa kwanza kulalamika maisha ni magumu. Wanashinda vijiweni na wengine utawaona kutwa amekaa kwenye makochi sebureni akinyanyanyana remote control ya tv na watoto; wanajivunia mali za ndugu zao. Watu hao ni wapumbavu wanaokesha wakiomba ndugu zao wafe ili wao wapate mirathi. Na endapo wakiambiwa wajitegemee utasikia wakisema fulani ana roho mbaya, apendi kukaa na ndugu.
Biblia Takatifu inasema kwamba:
"Ataabishaye nyumba yake mwenyewe ataurithi upepo; Mpumbavu atakuwa mtumwa wa mtu mwenye moyo wa akili." ~ MITHALI 11:29
Kama na wewe ni miongoni mwao basi fahamu kuwa wewe ni MPUMBAVU na urithi wako unaokustahiri ni UPEPO. Kwa maana nyepesi ni kwamba wewe utakufa ukiwa hauna mali. Kwa nini ushinde sebureni kuwataabisha watoto kwa kunyanganyana nao remote ya tv? Kwa nini ushinde nyumbani kuwasumbua mawifi zako na mashemeji zako badala ya wewe kwenda kufanya kazi? Biblia inasema kwamba wewe ni mpumbavu na utakuwa mtumwa wa mtu mwenye moyo wa akili. Huo umasikini wako ulio nao ni matokeo kabisa ya uchanguzi ambao wewe mwenyewe umeuchagua. Mungu ajakuumba ili uishi kwa huzuni hapa duniani; wewe mwenyewe unaweza ukawa kichocheo cha furaha yako au huzuni yako uliyo nayo. Hebu badirika ufahamu wako sasa. Mtumainie Mungu huku ukiwa unafanya kazi.
Unajua kuna mambo ambayo watu huyakosea pasipo kujua; Zipo baraka za aina mbili ambazo Mungu anatupatia watu wake, ambazo ni: Baraka za mwilini, pamoja na baraka za rohoni. Baraka za rohoni huja kwa njia ya maombi; wakati baraka za mwilini huja kwa njia ya kufanya kazi huku ukimtumainia Mungu katika mambo yako yote. Umasikini ulionao unatokana na shida iliyomo ndani ya ufahamu wako. Usimsingizie shetani kabisa katika hilo. Uvivu wako ndio matokeo ya jinsi ulivyo. Biblia Takatifu inasema kwamba:
"Je! Wamwona mtu mwenye bidii katika kazi zake? Huyo atasimama mbele ya wafalme; Hatasimama mbele ya watu wasio na cheo." ~ MITHALI 22:29.
Hapo Biblia Takatifu inasema "...Wamwona mtu mwenye BIDII katika KAZI zake?..." Bidii hiyo inatakiwa iwepo katika KAZI sio katika KUOMBA OMBA. Hebu tazama hata mataifa yanayofanikiwa hapa duniani ni yale ambayo yameweka BIDII katika kufanya KAZI. Endapo akili yako ukiielekeza katika kuomba omba kamwe hautafanikiwa; kwa sababu Mungu anasema "..HERI KUTOA KULIKO KUPOKEA..." au kwa maana nyepesi ni kwamba "AMEBARIKIWA YEYE ANAYETOA KULIKO YULE ANAYEPOKEA." Usipende kuwa omba omba, bali fanya kazi zako kwa bidii huku ukimtumainia Mungu katika mambo yako yote.
Japokuwa hapa duniani tunapita, lakini Mungu anataka tufanikiwe miili yetu kama jinsi roho zetu zifanikiwavyo. Usiwe mvivu, fanya kazi nawe utaona baraka za Mungu zikimiminika maishani mwako. Pia kuwa mwaminifu kwa sababu Mungu huwapenda watu waaminifu; wawezeshe kwa kuwaonyesha njia wanaohitaji msaada wa kuinuliwa (usiwe mchoyo / saidia wengine). Mwisho kabisa napenda kusema kwamba fanya mambo yako kwa maarifa bila pupa, kwa maana imeandikwa:
"Kila aliye na busara hutenda kazi kwa maarifa; Bali wapumbavu hueneza upumbavu." ~ MITHALI 13:16.
Epukana na mambo yasiyofaa. Usiutangaze ubaya bali utangaze wema wa Mungu. Mungu anakupenda na hataki uishi maisha ya tabu hapa duniani. Usiwe mvivu; fanya kazi kwa bidii huku ukimtumainia Mungu na ukiwa mwaminifu Kwake ndipo utaona milango ya baraka ikikufungukia maishani mwako. Endapo ukiona umepata vipingamizi katika kazi hii, basi achana nayo na ufanye kazi nyingine yenye maslahi zaidi kwako. Usikate tamaa; mtumaini Yesu naye atakuwezesha katika mambo yako yote.
Biblia inasema kwamba:
"Mwenye haki hula akaishibisha nafsi yake; Bali tumbo la mtu mbaya litaona njaa." ~ MITHALI 13:16, 25.
Umasikini ulionao unatokana na shida iliyomo katoka ufahamu wako (akili zako), au umasikini unatokana na uvivu wako. Usimlaumu mtu kwa sababu wewe mwenyewe ndivyo umechaguwa kuwa hivyo. Ukitaka kuamini maneno haya; basi chukua hatua sasa nawe utathibitisha hiki nisemacho.

Wewe uliye fanyia kazi ujumbe huu; nakutakia baraka tele katika jina la Yesu Kristo. Amina.

0 MAONI:

Post a Comment

TUMA KWA RAFIKI :

Twitter FacebookMore

 
Kuhusu Huduma Hii | Masharti Ya Utumiaji Wa Tovuti Hii | Wasiliana Nasi | Tangaza Kupitia Tovuti Hii