Thursday, February 26, 2015

UNALINDWA NA NGUVU ZA MUNGU KWA NJIA YA IMANI; HAUNA SABABU YA KUMWOGOPA SHETANI WALA KAZI ZAKE ZOTE!

Biblia Takatifu inasema kwamba:

"Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu; tupate na urithi usioharibika, usio na uchafu, usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu. Nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani hata mpate wokovu ulio tayari kufunuliwa wakati wa mwisho." - 1 Petro 1:3-5

Wakati umefika Mkristo kuyatambua mamlaka uliyopewa na Mungu Baba. Biblia inasema: Mungu Baba (JEHOVA / YAHWEH) ametuzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye UZIMA kupitia ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Hapa zingatia sana: Tumaini hilo la UZIMA tunalipata kupitia UFUFUKO wa Yesu Kristo; hatulipati tu kupitia Yesu, bali tunalipata kupitia UFUFUKO wa Yesu Kristo. Lazima uelewe kuwa UFUFUKO wa Yesu Kristo ndio umekamilisha uzima wetu.

Hapa siongelei habari za udini, maana kuna watu wa dini ambao Yesu wao bado amekufa / yupo kaburini!
Hapa siongelei habari za Yesu wa kwenye Qur'an; Injili ni kulitangaza neno la Mungu bila unafiki wala kufichana: Issa bin Maryamu bado amekufa! Lakini Yesu Kristo Mwana wa YAHWEH yupo hai. Issa bin Maryamu alikuja kumtangaza ALLAH, lakini Yesu Kristo alikuja kutimiza mapenzi ya Baba Yake wa mbinguni anayeitwa YEHOVA. Wakristo mwe na akili; huo upuuzi wa kukubali Issa bin Maryamu unawafanya kuwaondolea mamlaka mliyowekewa na Mungu Baba ndani yenu.

Biblia inasema: KUFUFUKA kwa Yesu kunatupatia TUMAINI LA UZIMA. Sisi ni uzao mteule wa Mungu; sisi ni milki ya Mungu; YEHOVA ametuzaa mara ya pili na kutufanya sisi kuwa milki Yake. Hakuna pepo mchafu wala mchawi mwenye mamlaka juu yako ikiwa wewe umemkabidhi Yesu awe Bwana na Mwokozi wa maisha yako. WEWE UNALINDWA NA NGUVU ZA MUNGU KWA NJIA YA IMANI.

Hatulindwi na nguvu za Mungu kwa kuvaa rozari, wala hirizi! Huo ni utapeli tu wa kidini. Neno IMANI ni kutenda pasipo kutumia vielelezo. Nguvu za Mungu hazimo katika maji, wala vitambaa, wala sanamu, wala mafuta; bali nguvu hizo zimo ndani yetu kwa sababu sisi ni hekalu la Mungu, Roho Mtakatifu ameweka makao Yake ndani yetu, nasi tunashinda zaidi ya kushinda.

Mkristo anayejitambua haogopi wachawi wala hila za Shetani. Mkristo anayejitambua hutumia mamlaka ya jina la Yesu kwa kuharibu kila kazi za Shetani. Sisi tunaye Mungu ndani yetu; tunapokutana na upinzani wa Shetani huo huwa sio muda wa kuomba bali ni muda ya kukemea katika jina la Yesu Kristo. Mtu aliyeokoka anatambua yeye ni nani katika ulimwengu huu. SISI TUNALINDWA NA NGUVU ZA MUNGU KWA NJIA YA IMANI.

Neema hiyo ipo kwa wale tu waliomkabidhi Yesu awe Bwana na Mwokozi wa maisha yao. Kama wewe bado haujamkabidhi Yesu maisha yako; basi sali sala hii fupi:

"Mungu Baba, asante kwa wokovu ulionipatia kupitia Yesu Kristo. Ninakiri pasipo msaada wako mimi nimeangamia; sasa ninayakabidhi maisha yangu Kwako, nitakase dhambi zangu kwa damu ya Yesu Kristo; tawala maisha yangu tangu sasa, niongoze katika mapenzi Yako, nifanye niwe jinsi Wewe utakavyo niwe kwa ajili ya utukufu Wako. Ninaomba Roho Wako Mtakatifu aniongoze tangu sasa hata milele. Asante kwa kunifanya kiumbe kipya katika jina la Yesu Kristo. Amen"

Amini tayari umekuwa kiumbe kipya, amini tayari umesamehewe dhambi; lakini umebakiwa na kitu kimoja tu! Ambatana na watu (Kanisa) wanaohubiri Injili ya kweli (wokovu) ili uweze kukua katika imani.

Nakutakia baraka tele katika jina la Yesu Kristo. Amen.

0 MAONI:

Post a Comment

TUMA KWA RAFIKI :

Twitter FacebookMore

 
Kuhusu Huduma Hii | Masharti Ya Utumiaji Wa Tovuti Hii | Wasiliana Nasi | Tangaza Kupitia Tovuti Hii