KAMPENI YA UZIMA WA MILELE:
"KUTII NENO LA MUNGU NA UTAKATIFU KWANZA."
Ukristo sio dhehebu; bali Ukristo ni mahusiano bora na Mungu.
Watu wengi hudhani Ukristo ni dhehebu ambalo limeanzishwa ili kuleta ustaarabu fulani katika jamii. Wakristo wengi wanaishi maisha ya kuigiza kisa tu ni wafuasi wa kanisa fulani! Wengine wanayaacha maagizo ya Mungu na kuyaheshimu mapokeo potofu ya dhehebu fulani eti kisa tu na wao wanajiita wakristo! Wengi wanaishi maisha ya maigizo, wanatenda dhambi kwa siri huku wakijiita "wapendwa"! Ndugu yangu na rafiki yangu; hapo unajidanganya wewe mwenyewe. Hakuna dhambi unayoweza kumficha Mungu. Leo ninasema na roho yako! Yachunguze matendo yako, chunguza siri za nafsini mwako; umemtenda Mungu dhambi. Umekuwa mnafiki, umekuwa na majungu japo unajiita mkristo, umekuwa mwizi japo unaitwa mpendwa, umekuwa mwongo umezaa hata nje ya ndoa yako kwa siri ukidhani Mungu hakuoni, umekuwa mshirikina na umejaa hila nafsini mwako. Unatenda ukidhani hakuna akuonaye; kumbe hapo wajidanganya wewe mwenyewe.
Biblia Takatifu inatuambia kwamba:
"Pumzi ya mwanadamu ni taa ya BWANA; Hupeleleza yote yaliyomo ndani yake." ~ Mithali 20:27.
Hakuna jambo uwezalo kumficha Mungu. Yeye anayajua mawazo yako hata kabla hujatenda jambo. Mungu anajua kuwa leo umekusudia kufanya uzinzi japo kuwa unamficha mchungaji wako! Anajua kuwa leo umetoka kufanya uzinzi japo kuwa unasema "Bwana Yesu asifiwe"!
Ichunguze nafsi yako, tubu sasa kwa maana neema bado ingalipo kwako. Wokovu sio wa maigizo, bali wokovu ni maisha halisi. Najua umeanguka mara nyingi dhambini lakini leo unayo nafasi ya kurekebisha maisha yako; Tubu sasa, la sivyo jehanam ipo kwa ajili yako na inakungoja.
Narudia tena kwa msisitizo: Ukristo sio dhehebu; bali Ukristo ni mahusiano bora na Mungu. Ukristo unaonekana katika kunena kwako, kuvaa kwako, upendo wako kwa Mungu na kwa majirani zako. Huwezi kusema Mungu hatazami uvaaji bali anatazama tu roho yako! Hapo hakika haupo salama; hicho ni kiburi tu cha uzima kinachokusumbua. Biblia inasema kuwa sisi ni barua isomwayo na watu wote (2 Kor 3:2), je ni tabia ipi uioneshayo kwa watu wasiomjua Mungu? Huko ni kuutukana wokovu wako, na hakika utatoa hesabu ya matendo yako yote. Haijarishi kuwa wewe unajiita au unaitwa mtume au nabii, haijarishi wewe ni mwinjilisti au mchungaji, haijarishi kwamba wewe ni mwimbaji au ni mwalimu, na hata kama wewe ni muumini wa kawaida tu; lakini nakuambia usipotubu leo, hakika kesho yako itakuwa ni ya majuto; itakuwa ni kilio na kusaga meno milele yote.
Biblia inapotuambia tujitenge na uovu wa kila namna (Zaburi 107:42); ni kwa sababu dhambi iingiapo unaweza ukaiona kama ni kitu kidogo tu, lakini usipoitubu na kuikemea utajikuta umejenga mazoea ya kuiona ni kitu cha kawaida tu; na hapo ndipo uovu unaumbika ndani yako. Hata kama ukikemewa utakuwa na kiburi kwa maana hiyo roho ya kuizoelea dhambi inakuandama. Dhambi sio kitu cha kuzoelea hata kidogo, dhambi imekusudia kukutenga tena na Mungu; uwe makini sana mpendwa. Leo ninaongea nawe kwa upole, ninaonge na roho yako. Rekebisha matendo yako kwa maana neema bado ingalipo kwako.
Biblia Takatifu inasema:
"Wanyofu wa moyo wataona na kufurahi, Na uovu wa kila namna utajifumba kinywa.
Aliye na hekima na ayaangalie hayo; Na wazitafakari fadhili za Bwana." ~ Zaburi 107:42-43
Mtu MNYOFU ndiye atakayeufurahia uzima wa milele; lakini mwovu atakataliwa mbali kabisa na Mungu. Kila jambo linayo kanuni yake, hata uzima wa milele pia unayo kanuni yake. Biblia Takatifu inatuambia kwamba:
"Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;
mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo." ~ Waebrania 12:14-15
Tafuta kwa bidii amani kwa watu wote pamoja na huo UTAKATIFU. Tunapoelekea katika mwaka 2015, hebu kampeni yetu iwe ni "KUTII NENO LA MUNGU NA UTAKATIFU KWANZA" Tuyakemee na kujiepusha na mafundisho potofu.Tuzingatie hili:
"KUTII NENO LA MUNGU NA UTAKATIFU KWANZA"
Ukristo sio dhehebu; bali Ukristo ni mahusiano bora na Mungu. Nawatakia nyote baraka tele katika jina la Yesu Kristo, amen.
0 MAONI:
Post a Comment