Monday, September 16, 2013

Uchaguzi wako na uhamuzi wako ndio matokeo ya jinsi ambavyo wewe ulivyo.

Je! Wajua ? ? ?

"MTU ANAKUWA MASIKINI KWA SABABU YEYE MWENYEWE AMECHAGUA AU AMEKUBALI YEYE MWENYEWE KUWA HIVYO." Uchaguzi wako na uhamuzi wako ndio matokeo ya jinsi ambavyo wewe ulivyo.

Bibilia Takatifu inasema kwamba:
"Mtu mvivu hapiki mawindo yake; Bali mwenye bidii anazo mali za thamani." ~ MITHALI 12:27.
Siku zote watu wengi huwa masikini kwa sababu ya UVIVU walio nao. Upo uvivu wa namna tofauti, mfano: Uvivu wa kufikiri; na, Uvivu wa kufanya kazi. Watu wengi ni wavivu wa kufikiri namna ya kufanyia ufumbuzi changamoto mbali mbali wanazokutana nazo maishani; wamekuwa ni wepesi wa kukata tamaa. Wao wanataka kwanza warahisishiwe mambo ndipo wapate wepesi. Hawapendi kabisa kushughulisha akili zao; watu wa namna hiyo hawafanikiwi kwa sababu ya uvivu walio nao.

Tukija kwenye kundi la wavivu wa kufanya kazi; hapa napo wapo watu wengi sana. Watu hawa wamekaa wakisubiri kula kutoka katika kazi za wenzao; hawalimi lakini wao ni wa kwanza kuvuna hata ambavyo havijakomaa; hawapiki lakini wao ni wa kwanza kuuliza kama vimeiva jikoni; wanakataa kuajiriwa lakini wao ndio wa kwanza kuuliza kama mshahara umetoka; hawatafuti chakula lakini wao ndio wa kwanza kulalamika kuwa chakula hakitoshi mezani; na hawataki kujishughulisha lakini wao ndio wa kwanza kulalamika maisha ni magumu. Wanashinda vijiweni na wengine utawaona kutwa amekaa kwenye makochi sebureni akinyanyanyana remote control ya tv na watoto; wanajivunia mali za ndugu zao. Watu hao ni wapumbavu wanaokesha wakiomba ndugu zao wafe ili wao wapate mirathi. Na endapo wakiambiwa wajitegemee utasikia wakisema fulani ana roho mbaya, apendi kukaa na ndugu.
Biblia Takatifu inasema kwamba:
"Ataabishaye nyumba yake mwenyewe ataurithi upepo; Mpumbavu atakuwa mtumwa wa mtu mwenye moyo wa akili." ~ MITHALI 11:29
Kama na wewe ni miongoni mwao basi fahamu kuwa wewe ni MPUMBAVU na urithi wako unaokustahiri ni UPEPO. Kwa maana nyepesi ni kwamba wewe utakufa ukiwa hauna mali. Kwa nini ushinde sebureni kuwataabisha watoto kwa kunyanganyana nao remote ya tv? Kwa nini ushinde nyumbani kuwasumbua mawifi zako na mashemeji zako badala ya wewe kwenda kufanya kazi? Biblia inasema kwamba wewe ni mpumbavu na utakuwa mtumwa wa mtu mwenye moyo wa akili. Huo umasikini wako ulio nao ni matokeo kabisa ya uchanguzi ambao wewe mwenyewe umeuchagua. Mungu ajakuumba ili uishi kwa huzuni hapa duniani; wewe mwenyewe unaweza ukawa kichocheo cha furaha yako au huzuni yako uliyo nayo. Hebu badirika ufahamu wako sasa. Mtumainie Mungu huku ukiwa unafanya kazi.
Unajua kuna mambo ambayo watu huyakosea pasipo kujua; Zipo baraka za aina mbili ambazo Mungu anatupatia watu wake, ambazo ni: Baraka za mwilini, pamoja na baraka za rohoni. Baraka za rohoni huja kwa njia ya maombi; wakati baraka za mwilini huja kwa njia ya kufanya kazi huku ukimtumainia Mungu katika mambo yako yote. Umasikini ulionao unatokana na shida iliyomo ndani ya ufahamu wako. Usimsingizie shetani kabisa katika hilo. Uvivu wako ndio matokeo ya jinsi ulivyo. Biblia Takatifu inasema kwamba:
"Je! Wamwona mtu mwenye bidii katika kazi zake? Huyo atasimama mbele ya wafalme; Hatasimama mbele ya watu wasio na cheo." ~ MITHALI 22:29.
Hapo Biblia Takatifu inasema "...Wamwona mtu mwenye BIDII katika KAZI zake?..." Bidii hiyo inatakiwa iwepo katika KAZI sio katika KUOMBA OMBA. Hebu tazama hata mataifa yanayofanikiwa hapa duniani ni yale ambayo yameweka BIDII katika kufanya KAZI. Endapo akili yako ukiielekeza katika kuomba omba kamwe hautafanikiwa; kwa sababu Mungu anasema "..HERI KUTOA KULIKO KUPOKEA..." au kwa maana nyepesi ni kwamba "AMEBARIKIWA YEYE ANAYETOA KULIKO YULE ANAYEPOKEA." Usipende kuwa omba omba, bali fanya kazi zako kwa bidii huku ukimtumainia Mungu katika mambo yako yote.
Japokuwa hapa duniani tunapita, lakini Mungu anataka tufanikiwe miili yetu kama jinsi roho zetu zifanikiwavyo. Usiwe mvivu, fanya kazi nawe utaona baraka za Mungu zikimiminika maishani mwako. Pia kuwa mwaminifu kwa sababu Mungu huwapenda watu waaminifu; wawezeshe kwa kuwaonyesha njia wanaohitaji msaada wa kuinuliwa (usiwe mchoyo / saidia wengine). Mwisho kabisa napenda kusema kwamba fanya mambo yako kwa maarifa bila pupa, kwa maana imeandikwa:
"Kila aliye na busara hutenda kazi kwa maarifa; Bali wapumbavu hueneza upumbavu." ~ MITHALI 13:16.
Epukana na mambo yasiyofaa. Usiutangaze ubaya bali utangaze wema wa Mungu. Mungu anakupenda na hataki uishi maisha ya tabu hapa duniani. Usiwe mvivu; fanya kazi kwa bidii huku ukimtumainia Mungu na ukiwa mwaminifu Kwake ndipo utaona milango ya baraka ikikufungukia maishani mwako. Endapo ukiona umepata vipingamizi katika kazi hii, basi achana nayo na ufanye kazi nyingine yenye maslahi zaidi kwako. Usikate tamaa; mtumaini Yesu naye atakuwezesha katika mambo yako yote.
Biblia inasema kwamba:
"Mwenye haki hula akaishibisha nafsi yake; Bali tumbo la mtu mbaya litaona njaa." ~ MITHALI 13:16, 25.
Umasikini ulionao unatokana na shida iliyomo katoka ufahamu wako (akili zako), au umasikini unatokana na uvivu wako. Usimlaumu mtu kwa sababu wewe mwenyewe ndivyo umechaguwa kuwa hivyo. Ukitaka kuamini maneno haya; basi chukua hatua sasa nawe utathibitisha hiki nisemacho.

Wewe uliye fanyia kazi ujumbe huu; nakutakia baraka tele katika jina la Yesu Kristo. Amina.

Wednesday, July 31, 2013

WEWE NI NURU YA ULIMWENGU.

Ewe Mkristo; wewe ni NURU YA ULIMWENGU (Mathayo 5:14). Hivyo basi; ili uweze kuuangazia ulimwengu unapaswa kufanya hivi:
"Yatendeni mambo yote pasipo manung'uniko wala mashindano, mpate kuwa wana wa Mungu wasio na lawama, wala udanganyifu, wasio na ila kati ya kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka; ambao kati ya hao mnaonekana kuwa kama mianga katika ulimwengu." ~ WAFILIPI 2:14-15.
Ni kweli kwamba sisi tumo ndani ya kizazi kilichopotoka na chenye ukaidi; hatumo humu kwa mkosi bali ni kwa kusudi la Mungu ili sisi tuuangazie ulimwengu wapate kumjua Mungu kupitia sisi. Mungu anataka sisi tuufikie ulimwengu usiomjua Yeye ili tuubadilishe upate kumjua na kumpokea Yeye.

Ewe mtumishi wa Mungu, hakikisha mahali pote ulipo unauangazia ulimwengu kwa neno la Mungu na maisha matakatifu. Sisi tumeokolewa ili tuujenge mwili wa Kristo. Mtangaze Yesu kila mahali ulipo, hiyo ndiyo kazi tuliyoamriwa tuifanye. Kuhubiri ni amri wala si ihari; Yesu anasema kwamba;
"...nimewapa AMRI ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru." ~ LUKA 10:19
Kila Mkristo analazimika KUHARIBU KILA KAZI YA SHETANI, endapo kama usipofanya hivyo unakuwa umekaidi kutii AMRI hiyo. USIOGOPE kwa sababu Yesu ametuambia:
"...hakuna kitu kitakachowadhuru." ~ LUKA 10:19
Nawatakieni huduma njema na yenye baraka tele iliyojawa na nguvu na uweza wa Roho Mtakatifu. Ukimwamini Yesu na ukimwacha Yeye akuongoze; hakika yote yawezekana katika jina la Yesu.

Wednesday, July 24, 2013

UJUMBE HUU NI WAKO..!

UJUMBE HUU NI WAKO:
"Mtu awaye yote asiudharau ujana wako, bali uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi... ufanye bidii katika kusoma na kuonya na kufundisha." ~ 1 Timotheo 4:12-13.
Ewe Mtumishi wa Yesu Kristo unaambiwa kwamba: "...ufanye bidii katika KUSOMA na KUONYA na KUFUNDISHA."

Jitahidi kila siku unatenga nafasi ya KUSOMA neno la Mungu; kwa sababu hauwezi kulifundisha neno kwa ufasaha bila ya KUSOMA. Na pia unaposoma ni lazima utafakari; je! Ni kitu gani hicho usomacho? Kusoma maana yake ni KUJIFUNZA. Si kila kitu kinakufaa wewe kujifunza. Hakikisha unajifunza mema ili uweze kuzaa mema. Kila kiingiacho akilini mwako kwa wingi ndicho hicho kinacho jaza moyo wako, na ndicho kiutiao najisi mwili wako au kiletacho baraka kwako. Zingatia sana kile uonacho, usikiacho, na ujifunzacho kiwe chema. Kujifunza ndio chanzo cha maarifa; kuwa makini na hicho ujifunzacho.

Katika KUONYA; Hauwezi kuonya bila ya kuwa na uhakika wa onyo ulitoalo. Ukisoma / ukijifunza neno la Mungu hakika utayajua mapenzi Yake. Hapa tunagundua kuwa hata kuonya vema kunatokana na KUJIFUNZA mema. Tumia mamlaka sahihi, kwa wakati sahihi, na mahali sahihi.

Pia katika KUFUNDISHA; napo hauwezi kuwa mwalimu mzuri kama wewe ulikuwa mwanafunzi MBAYA. Lazima uzingatie; je! Unajifunza nini? Pia je! Unafundisha nini?

Ewe Mtumishi wa Yesu Kristo unaambiwa kwamba: "...ufanye bidii katika KUSOMA na KUONYA na KUFUNDISHA."

UJUMBE HUU NI WAKO.

Nakutakia huduma njema katika jina la Yesu Kristo. Amen.

TUMA KWA RAFIKI :

Twitter FacebookMore

 
Kuhusu Huduma Hii | Masharti Ya Utumiaji Wa Tovuti Hii | Wasiliana Nasi | Tangaza Kupitia Tovuti Hii