Thursday, January 11, 2018

JIONESHE KUWA MWANAMUME


 JIONESHE KUWA MWANAMUME (1 Wafalme 2:1)

Bwana Yesu Kristo apewe sifa. Ninamshukuru Mungu kwa neema Yake kuu amenipatia kibali cha kulihudumia kanisa Lake hata sasa. Leo ninao ujumbe wenye baraka kwako uliobeba kichwa kinachoitwa: JIONESHE KUWA MWANAMUME. Huu ni mwanzoni mwa mwaka 2018, watu wengi wanatazamia baraka nyingi ziambatane nao; hivyo basi, Roho wa Mungu amenipa ujumbe huu kwa ajili yako: “JIONESHE KUWA MWANAMUME”.
Hebu tufungue Biblia zetu tusome 1 Wafalme 2:1-2, Biblia Takatifu inasema:

Basi siku ya kufa kwake Daudi ikakaribia, akamwusia Sulemani mwanawe, akasema, Mimi naenda njia ya ulimwengu wote (yaani, naenda kufa); basi uwe hodari, ujioneshe kuwa mwanamume…” ~ 1 Wafalme 2:1-2

Mfalme Daudi anamwambia Sulemani mwanawe: “…ujioneshe kuwa mwanamume…” (“…show thyself a man…” - KJV)

Je, nini basi maana ya “…kuwa mwanamume…”? Mwanamue ni mtu asiye ogopa, mtu jasiri mwenye kufanya mambo magumu na shujaa. Kuwa mwanamume sio kijinsia bali ni kuwa jasiri na hodari. Mfalme Daudi alitambua dhahili shujaa ndiye anayetawala wala si mtu mlegevu; hapo alimtaka Sulemani mwanawe awe mtu hodari na jasiri ili aweze kuhimili misukosuko ya utawala unaomkabili. Mfalme Daudi sio tu alimtaka Sulemani mwanawe awe hodari, bali pia AJIONESHE YEYE NI HODARI; yaani watu wamwone na wamtambue yeye ni hodari. Hivyo ndivyo Mungu anavyotaka sisi tuwe hadi ulimwengu utambue uwepo wetu (Luka 10:19).

Watu wengi huwa wanatamani sana kuinuliwa, lakini je umejiandaa kuzikabili changamoto zinazoambatana na baraka hizo? Mara zote unapobarikiwa na kuinuliwa kwa viwango vya juu kunaambatana na kundi la maadui linalokupinga kimwili na kiroho; mf. kuna majambazi, pepo wachafu, wachawi, wasengenyaji na wengine watakuchukia tu kwa sababu wewe umeinuliwa juu kuliko wao. Ndio maana neno la kwanza tumeona Sulemani ameambiwa “…uwe hodari…” (1 Fal 2:2; 1 Nya 28:10, 20) Mtu hodani ni yule mwenye uwezo wa kufanya jambo lililowashinda wengine, mtu mahiri na stadi; anayewaongoza watu kwenda pale wanapopaswa kwenda wala si pale wanapotaka kwenda.

Ukitaka kuvifikia viwango vya juu vya Baraka ni lazima uchague kufanya mambo magumu kwa wengine, usichague mambo mepesi mepesi; bali yafanye mambo magumu kwa umahiri na ustadi mkubwa. Uwe hodari katika kila ufanyalo; iwe katika biashara yako, masomo yako, familia yako, ndoa yako, kazi zako na katika kila utendalo.

Sasa hivi tumeshaingia katika mwaka mpya ambao wengi wanatazamia kuinuliwa zaidi ya mwaka uliopita; Lakini tambua kuwa mwaka mpya ni badiliko la kalenda tu, bali kutamalaki hakupo kwa watu walegevu wala wavivu, ila ni kwa watu walio hodari. Lazima ujioneshe kuwa mwanamume.
Biblia inasema:

Atendaye mambo kwa mkono mlegevu huwa maskini; Bali mkono wake aliye na bidii hutajirisha.– Mithali 10:4

Utofauti kati ya fukara na tajiri upo katika namna yake ya kufikiri na jinsi anavyotenda mambo; ni hivyo tu. Utajiri / kufanikiwa ni uchaguzi wako, hata ufukara / kushindwa pia ni uchaguzi wako pia. Huwezi kukwea ngazi ya kamba iliyoning’inia huku ukiwa umeweka mikono mfukoni mwa suluali yako! Ni lazima ushikilie vizuri ndipo utaweza kuikwea.

Hata mafanikio ya mtu hayaji kizembe, ni lazima uchague kufanya mambo magumu, makubwa yanayowashinda wavivu. Uwe na ndoto kubwa, heshimu malengo yako, uwe jasiri, thubutu kutenda bila woga, fanya kile chenye faida, tunza wakati, epuka marafiki wabaya, uwe na nidhamu ya pesa, weka akiba katika vitu vinavyoongezeka thamani na umtangulize Mungu katika kila ufanyalo. Wakati sahihi wa kufanikiwa ni sasa; anza na hicho ulichonacho: kama ni wazo basi washirikishe watu sahihi, na kama ni mtaji kidogo anza nao uo huo huku ukiwa na mipango ya kufika juu zaidi.

Vile vile tambua kwamba, hauwezi kufanikiwa kwa akili zako mwenyewe tu; ndio maana mfalme Daudi anaendelea kumwambia Sulemani mwanawe, kwamba:

“…uyashike mausia ya BWANA, Mungu wako, uende katika njia Zake, uzishike sheria Zake, na amri Zake, na hukumu Zake, na shuhuda Zake …upate kufanikiwa katika kila ufanyalo, na kila utazamako.” 1 Wafalme 2:3-4

Mweke Mungu mbele ya kila jambo; Ndio maana sisi tunaambiwa: “Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa Yeye. “ – (Wakolosai 3:17). Ukimtumainia Mungu katika yote, hapo ndipo kila utazamako (unachokihitaji) kinakuwa chako. Katika kuomba kwako usiombe kwa tamaa zako, bali kwa ajili ya utukufu wa Mungu (Yakobo 4:3). Lazima Mungu awe na sehemu katika mipango yako, na zingatia kumtolea Mungu sadaka ya shukurani katika mapato yako; si kwa kulazimishwa, bali kwa moyo mkunjufu wa shukurani sawa sawa na jinsi Mungu alivyokubariki. Endapo kama umemuwekea Mungu nadhiri, hakikisha unakuwa mwaminifu katika kuitimiza kwa uhaminifu wote (Hesabu 30:2; Kumb 23:21).
Uwe hodari katika kila lililo jema wala si katika uovu (Zaburi 64:5), ndio maana Biblia inasema:

“…Heri mtu yule amchaye BWANA, Apendezwaye sana na maagizo Yake. Wazao wake watakuwa hodari duniani; Kizazi cha wenye adili kitabarikiwa.” – Zaburi 112:1-2

Hapo zingatia neno hili: “Kizazi cha wenye adili kitabarikiwa.” Hicho ni kizazi kinachomtii Mungu ndicho kinachobarikiwa. Baraka za mcha Mungu hodari zitaambatana naye pamoja na kizazi chake. Sisi Wakristo, tayari Mungu ametubariki wala hakuna laana yoyote ile inayotuandama (1 Petro 2:9). Japokuwa tayari Mungu amekubariki, kama jinsi tunavyosoma katika Kumb 28:2-6

…baraka hizi zote zitakujilia na kukupata usikiapo sauti ya BWANA, Mungu wako. Utabarikiwa mjini, utabarikiwa na mashambani. Utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, na uzao wa wanyama wako wa mifugo, maongeo ya ng'ombe wako, na wadogo wa kondoo zako. Litabarikiwa kapu lako, na chombo chako cha kukandia unga. Utabarikiwa uingiapo, utabarikiwa na utokapo. – Kumb 28:2-6

Lakini baraka hizi utazipata pale USIPOKATA TAMAA. Hakuna mafanikio mepesi, ni lazima kuwa hodari kweli kweli; lazima ujioneshe kuwa mwanamume kweli kweli. Hebu tusome habari hii itakusaidia kukufungua ufahamu wako; katika Mwanzo 26:17-22 Biblia inasema:

Basi Isaka akatoka huko akapiga kambi katika Bonde la Gerari, akakaa huko. Isaka akarudi akavichimbua vile visima vya maji walivyovichimba siku za Abrahamu babaye, maana wale Wafilisti walikuwa wamevifukia baada ya kufa kwake Abrahamu. Naye akaviita majina kufuata majina alivyoviita babaye. Pia watumishi wa Isaka wakachimba katika lile bonde, nao wakapata kisima cha maji yanayobubujika.
Bali wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka, wakisema, “Maji haya ni yetu.” Ndipo akakiita jina la kile kisima Eseki, kwa sababu waligombana naye. Nao wakachimba kisima kingine, wakagombania na hicho tena. Basi akakiita jina lake Sitna. Akaondoka huko na akachimba kisima kingine, wala hicho hawakukigombania. Basi akakiita jina lake Rehobothi, kwa maana alisema, “Kwa kuwa sasa BWANA ametufanyia nafasi, nasi tutazidi katika nchi.” – Mwanzo 26:17-22

Hapo tumejifunza Isaka hakupoteza muda kung’ang’ania kushindana na adui zake, bali yeye alitazama fursa kwingine na kuitumia. Siku zote ukitaka kufika viwango vya juu vya baraka, usipoteze muda kushindana na mtu mpumbavu, bali tazama fursa zilizopo mbele yako alafu piga hatua kuzifuata. Usifanye jambo lisilo na faida kwako, usiupoteze bure wakati wako. Usiishie kulaumu tu, bali tazama fursa zilipo na ujichanganye huko. Baraka za Mungu zinaambata na mtu yule aliyechukua hatua kuzifuata; wala sio kwa kusali tu, wala kwa kufunga na kuomba tu: bali kwa matendo pia. Huwezi kuzifikia baraka zako kwa kuishia kusema “amina” kanisani wala kwa kupewa mafuta ya upako; bali unapaswa utambue tayari Mungu amekwisha kubariki ila kilichobaki ni wewe kuzifuata hizo baraka zako. Hapo ni sawa na mzazi aliyekuwekea chakula ndani, ila wewe umebakiza jukumu lako la kuinuka na kukila pindi unapokihitaji. Tazama wapi fursa zilipo, nawe nenda huko kazifuate ndipo utaifikia baraka yako.

Jambo la mwisho la kuzingatia ninalopenda kukwambia; Tenda mambo kwa busara bila kumdharau mtu awaye yote. Biblia Takatifu inatuambia kwamba:

 “Tazama, Mungu ni hodari, wala hamdharau mtu ye yote; Ana uweza katika nguvu za fahamu.” – Ayubu 36:5

Mungu Mwenyewe ni hodari (yaani, anatenda mambo yanayowashinda wengine) lakini hamdharau mtu ye yote. Hizi mali na utajiri tunaoupata vyote vinatoka Kwake, ni kwa neema Zake tu; hatukuja na kitu duniani na wala hatutaondoka na kitu duniani; hivyo basi tuwahehimu na kuwapenda watu wote, na hata kuwaombea watu walio adui zetu (Luka 6:35; Warumi 12:20).
Tukisoma katika Mithali 17:2 tunaona Biblia inasema:

“Mtumwa atendaye kwa busara atamtawala mwana atendaye mambo ya aibu; Tena atapata sehemu ya urithi kati ya ndugu.” – Mithali 17:2

Zingatia point hii: hapo (Mithali 17:2) imetumia neno "Mtumwa...", kwa kumaanisha "mtu mwovu" (yule asiyemtii wala kumwabudu Mungu wa kweli) akitenda mambo kwa busara ndipo atamtawala "...mwana..."  atendaye mambo ya aibu (mtu wa Mungu aliyekengeuka au afanyaye mambo kivivu).  Kwa hiyo; hapo neno "mtumwa" linamwakilisha "mtu mwovu", na neno "mwana" linamwakilisha "mtu wa Mungu". Hapa ndipo utaweza kuwaona baadhi watu waovu wanafanikiwa na kustawi maishani kuliko wacha Mungu walio wavivu; ndiyo maana hapo Biblia inamalizia kwa kusema kuhusu huyo mtumwa: "..Tena atapata sehemu ya urithi kati ya ndugu.” – (Mithali 17:2) Yaani atamiliki ile sehemu uliyopaswa wewe kuipokea.

Mafanikio au kushindwa vyote vipo katika uchaguzi wako; ikiwa unahitaji kufanikiwa, basi tenda mambo yote kwa busara, hekima na uwe hodari. Hakuna mafanikio yanayokuja kizembe; ni lazima ujioneshe kuwa mwanamume (sio kijinsia, ila katika “attitude” yako – namna yako ya kufikiri na kutenda kama mwana wa mfalme).


Jina langu naitwa Masanja Sabbi (masanjasabbi@gmail.com), nakutakia kheri na baraka tele katika kila utendalo. Malaika wa Mungu akutangulie na kukufanikisha katika jina la Yesu Kristo. Amen.

Wednesday, April 19, 2017

THAWABU YANGU NI NINI?


NAWAKUMBUSHA TU WATUMISHI WA MUNGU

"Basi thawabu yangu ni nini? Ni hii, ya kuwa nihubiripo, nitaitoa Injili bila gharama..." - 1 Kor 9:18

Inawezekana andiko hili huwa unalipita au haujawahi kulisoma; lakini leo napenda kukukumbusha mtu wa Mungu, kabla ya kuingia kwenye huduma, ni vema ukazingatia andiko hili.

Mbarikiwe sana watu wa Mungu.

Tuesday, April 18, 2017

UFUFUKO WA YESU


Je, Ufufuko wa Yesu ndio sikukuu ya Pasaka?
Je, Pasaka na “Easter” ni kitu kimoja?


Maswali hayo huwatatiza watu wengi sana, hivyo basi leo nimependa tujifunze ili tuondokane na utata huo; barikiwa sana na somo hili:

PASAKA
Sikukuu ya Pasaka ilikuwa mpango wa Mungu kwa Waisraeli ili washerehekee kuokolewa kwao kutoka utumwani Misri kwa njia ya miujiza (Kut 12:14,24).

Jina la sikukuu lilikumbusha tendo la malaika wa Mungu “kupita juu” ya nyumba za Waisraeli alipowauwa wazaliwa wa kwanza wa Wamisri (Kut 12:27). Lakini Mungu alihifadhi nyumba za Waisraeli wasipatwe na hukumu ile alipoona damu ya mnyama wa sadaka iliyopakwa kuzunguka mlango mkubwa wa mbele wa nyumba zao. Damu hiyo ilikuwa ishara kwamba uzima usiokuwa na hatia ulitolewa badala ya mtu aliekuwa chini ya hukumu (Kut 12:5,7,12-13,21-23).

Mwezi wa Pasaka uliwekwa kuwa mwezi wa kwanza wa mwaka wa kalenda ya Kiyahudi (Abibu / Nisani ambao ni mwezi March kwenda April katika kalenda ya Gregory).

Baada ya Pasaka, sikukuu ya siku saba ya Mkate Usiotiwa Chachu iliunganishwa na sherehe ya Pasaka; mambo hayo miwili hasa yalihesabiwa kama sikukuu moja (Kum 16:1-8; Mk 14:1). Baada ya kuondoa chachu kutoka nyumba zao kabla ya Pasaka, watu walitunza nyumba zao zisiwe na chachu yo yote kwa juma lingine baada ya Pasaka (Kut 12:14-20). Jambo hili liliwakumbusha kwamba, baada ya kuokolewa kwa njia ya Pasaka, walikimbia kutoka Misri kwa haraka, wakipika mikate isiyochachwa hapo waliposafiri (Kut 12:33-34,39).

Waisraeli walipofika Kanaani, walipaswa kuadhimisha sikukuu ya Pasaka katika mahali maalumu pa ibada tu. Mwanzoni mahali hapo palikuwa Hema la Kukutania, na baadaye palikuwa helalu (Kum 16:5-6; Yos 5:10-12; 2Nya 8:12-13; 30:1; 35:1; Lk 2:41; Yn 2:13; 11:55). Wanaume wote wa Israeli waliokuwa watu wazima walipaswa kuhudhuria sherehe ya Pasaka (Kut 23:14,17), na hata wageni waliweza kusherehekea, mradi tu walipata tohara na hivyo walikuwa sehemu ya watu wa Agano (Kut 12:43-49).

PASAKA KATIKA AGANO JIPYA
Wakati wa Bwana Yesu, sikukuu ya Pasaka ilikuwa kanuni maalumu pamoja na sherehe kadhaa zilizokuwa zimeongezeka. Ingawa watu walichinja mwana-kondoo hekaluni walikula karamu yake binafsi pamoja na marafiki na jamaa (Lk 22:8-13). Kati ya nyongeza zile za karamu kulikuwa na kikombe cha divai ambacho ni kwa ajili yake mkuu wa nyumba alisema sala ya shukrani (au ya baraka, 1 Kor 10:16), ambacho pia alikizungusha kwa wote walioshiriki, kabla ya kula mkate usiochachwa na baada yake pia (Mk 14:22-24; Lk 22:15-20).
Kuimba pia kulikuwa sehemu ya sherehe, washiriki wakiimba nyimbo mbalimbali za Zaburi zilizojulikana kwa “Zaburi za Hallel” (yaani za Haleluya - za kumsifu BWANA, ambazo ni Zaburi 113-118). Kwa kawaida waliimba Zaburi mbili za kwanza kabla ya kula mwana-kondoo na Zaburi nyingine baadaye (Mk 14:26).

Katika Pasaka ya mwisho ya Bwana Yesu, Yeye na wanafunzi Wake walikula karamu siku moja kabla ya wakati wake hasa, na labda pasipo mwana-kondoo (Lk 22:15; Yn 13:1). Inawezekana walifanya hivyo kwa kuwa Yesu alikwisha jua kwamba Yeye mwenyewe wakati huo alikuwa mwana-kondoo wa Pasaka; siku ya kesho yake angetoa maisha Yake wakati ule ule ambao wanyama wangechinjwa kwa maandalizi ya karamu iliyofuata usiku huo (Yn 18:28; 19:14,31,42).

Kifo cha Yesu msalabani kilikuwa tendo kuu la ukombozi ambalo Pasaka ya Waisraeli ilikuwa mfano wake mdogo tu (linganisha Kut 12:5 na 1 Pet 1:18-19, pia Kut 12:46 na Yn 19:36, pia Kut 12:21,27 na 1 Kor 5:7). Baada ya kufa kwake Yesu, Pasaka ya Wayahudi haikuwa na maana tena; iliondolewa na mahali pake sherehe mpya ya ukumbusho iliwekwa, yaani Chakula cha Bwana (Mt 26:17-30; 1 Kor 10:16; 11:23-26).
Hata hivyo, Agano Jipya linataja mahitaji ya Pasaka katika mafundisho ya Kikristo; kwa maana jinsi sikukuu ya Pasaka ilivyokuwa na maana kwamba Waisraeli walipaswa kutoa "chachu" katika nyumba zao, vivyo hivyo sadaka ya Yesu Kristo ina maana kwamba Wakristo wanapaswa kuondoa "dhambi" katika maisha yao (1 Kor 5:7-8).

Je, EASTER ndiyo PASAKA?
Neno “Easter” halipo katika Biblia yo yote ile (ya Kiebrania – Agano la Kale, wala ya Kiyunani – Agano Jipya). Katika maandiko yote ndani ya Biblia Takatifu hakuna sherehe ya “Easter” kwa watu wa Mungu. Tafasiri ya neno “Easter” tunaziona kwenye kamusi mbalimbali zikifafanua kuwa; ni sherehe za Kikristo kuadhimisha ufufuko wa Yesu.
Hebu tutazame nukuu zifuatazo:

"Easter
· n. the festival of the Christian Church celebrating the resurrection of Christ, held (in the Western Church) on the first Sunday after the first full moon following the northern spring equinox.
– ORIGIN OE Uastre, of Gmc origin and rel. to east; perh. from Éastre, the name of a goddess assoc. with spring." –
Oxford Dictionary 10th Edition;

"Easter, annual festival commemorating the Resurrection of Jesus Christ, and the principal feast of the Christian year... a Christian festival, embodies many pre-Christian traditions. The origin of its name is unknown. Scholars, however, accepting the derivation proposed by the 8th-century English scholar St Bede, believe it probably comes from “Ēostre”, the Anglo-Saxon name of a Teutonic goddess of spring and fertility, to whom was dedicated a month corresponding to April. Her festival was celebrated on the day of the vernal equinox; traditions associated with the festival survive in the Easter rabbit, a symbol of fertility, and in coloured Easter eggs, originally painted with bright colours to represent the sunlight of spring, and used in Easter-egg-rolling contests or given as gifts." -
Microsoft ® Encarta ® Encyclopedia 2005.

Neno “Easter” asili yake ni neno “Ēostre” ambalo ni jina la mungu “mke” wa mavuno na uzazi aliyekuwa akiabudiwa (amewekewa wakfu) majira ya kuchipua mimea hususani kipindi cha mwezi April, ambayo pia ndiyo mwezi Nisani kwa Wayahudi ambao waliadhimisha Pasaka.

Sherehe ya “Eostre / Easter” iliambatana na mambo ya kimila; walitoa sadaka ya sungura kama alama ya uzazi, na mayai yaliyopakwa rangi ya mng’ao ili kuwakilisha “jua” ambayo yalitumika katika mashindano ya kupondana mayai, au kutolewa tu kama zawadi.
Sherehe hizo zilitokana na dini ya kale ya Kigiriki, walikuwa na desturi ya kuadhimisha kurudi kwa Persephone binti wa Demeter / Ēostre “mungu wa mavuno” kutoka kuzimu kuja duniani kwenye mwanga wa mchana (return of Persephone, daughter of Demeter, goddess of the earth, from the underworld to the light of day); kurudi kwake “Persephone” kwa Wagiriki wa kale walitafasiri ni ufufuo wa maisha katika kuchipua mimea kipindi cha mwezi April baada ya kuharibiwa na majira ya baridi kali huko kwao. Watu hao waliamani kuwa “mungu” wao mwenye nguvu zote alikwenda kulala wakati wa msimu wa baridi, nao wakafanya sherehe na kucheza muziki katika majira ya kuchipua kwa mimea wakiamini “mungu” wao ameamka toka usingizini, amerudi toka kuzimu.

Lakini, katika Biblia ya lugha ya Kiingereza neno Pasaka limeandikwa: “Passover” likimaanisha “PITA-JUU” kama jinsi tulivyojifunza katika Kut 12:27, malaika wa Mungu alipoziacha nyumba za wana wa Israel kwa kupita juu na kuwaangamiza wazaliwa wa kwanza wa Wamisri.

Sherehe hizo za “Easter” zimeingia kwenye baadhi ya dini za Kikristo kutokana na mapokeo kutoka dini ya kipagani ya Wagiriki wa kale.

Tukirejea katika Biblia; hakuna sherehe za “Easter”, wala Pasaka sio “Easter”. Sherehe hizo za kipagani “Easter” ziliadhimishwa katika majira sambamba na sherehe za Pasaka ya Kiyahudi (mwezi Nisani / April) ambayo pia ndiyo majira Yesu alisulibiwa, kufa na kufufuka.

Mapokeo hayo ya “Easter” ndiyo yameingizwa hata leo katika sherehe za kidini ingawa kiukweli huo ni upagani uliofunikwa mwamvuli wa Ukristo.

Easter sio Ufufuko wa Yesu, wala Easter sio Pasaka ya Kiyahudi.

Ninaamini ujumbe huu umewafungua fahamu watu wengi; nami nakuombea uzidi kubarikiwa katika jina la Yesu Kristo, Amen.

TUMA KWA RAFIKI :

Twitter FacebookMore

 
Kuhusu Huduma Hii | Masharti Ya Utumiaji Wa Tovuti Hii | Wasiliana Nasi | Tangaza Kupitia Tovuti Hii