Je, Ufufuko wa Yesu ndio sikukuu ya Pasaka?
Je, Pasaka na “Easter” ni kitu kimoja?
Maswali hayo huwatatiza watu wengi sana, hivyo basi leo nimependa
tujifunze ili tuondokane na utata huo; barikiwa sana na somo hili:
PASAKA
Sikukuu ya Pasaka ilikuwa mpango wa Mungu kwa Waisraeli ili
washerehekee kuokolewa kwao kutoka utumwani Misri kwa njia ya miujiza
(Kut 12:14,24).
Jina la sikukuu lilikumbusha tendo la malaika wa
Mungu “kupita juu” ya nyumba za Waisraeli alipowauwa wazaliwa wa kwanza
wa Wamisri (Kut 12:27). Lakini Mungu alihifadhi nyumba za Waisraeli
wasipatwe na hukumu ile alipoona damu ya mnyama wa sadaka iliyopakwa
kuzunguka mlango mkubwa wa mbele wa nyumba zao. Damu hiyo ilikuwa ishara
kwamba uzima usiokuwa na hatia ulitolewa badala ya mtu aliekuwa chini
ya hukumu (Kut 12:5,7,12-13,21-23).
Mwezi wa Pasaka uliwekwa kuwa
mwezi wa kwanza wa mwaka wa kalenda ya Kiyahudi (Abibu / Nisani ambao
ni mwezi March kwenda April katika kalenda ya Gregory).
Baada ya
Pasaka, sikukuu ya siku saba ya Mkate Usiotiwa Chachu iliunganishwa na
sherehe ya Pasaka; mambo hayo miwili hasa yalihesabiwa kama sikukuu moja
(Kum 16:1-8; Mk 14:1). Baada ya kuondoa chachu kutoka nyumba zao kabla
ya Pasaka, watu walitunza nyumba zao zisiwe na chachu yo yote kwa juma
lingine baada ya Pasaka (Kut 12:14-20). Jambo hili liliwakumbusha
kwamba, baada ya kuokolewa kwa njia ya Pasaka, walikimbia kutoka Misri
kwa haraka, wakipika mikate isiyochachwa hapo waliposafiri (Kut
12:33-34,39).
Waisraeli walipofika Kanaani, walipaswa kuadhimisha
sikukuu ya Pasaka katika mahali maalumu pa ibada tu. Mwanzoni mahali
hapo palikuwa Hema la Kukutania, na baadaye palikuwa helalu (Kum 16:5-6;
Yos 5:10-12; 2Nya 8:12-13; 30:1; 35:1; Lk 2:41; Yn 2:13; 11:55).
Wanaume wote wa Israeli waliokuwa watu wazima walipaswa kuhudhuria
sherehe ya Pasaka (Kut 23:14,17), na hata wageni waliweza kusherehekea,
mradi tu walipata tohara na hivyo walikuwa sehemu ya watu wa Agano (Kut
12:43-49).
PASAKA KATIKA AGANO JIPYA
Wakati wa Bwana
Yesu, sikukuu ya Pasaka ilikuwa kanuni maalumu pamoja na sherehe kadhaa
zilizokuwa zimeongezeka. Ingawa watu walichinja mwana-kondoo hekaluni
walikula karamu yake binafsi pamoja na marafiki na jamaa (Lk 22:8-13).
Kati ya nyongeza zile za karamu kulikuwa na kikombe cha divai ambacho ni
kwa ajili yake mkuu wa nyumba alisema sala ya shukrani (au ya baraka, 1
Kor 10:16), ambacho pia alikizungusha kwa wote walioshiriki, kabla ya
kula mkate usiochachwa na baada yake pia (Mk 14:22-24; Lk 22:15-20).
Kuimba pia kulikuwa sehemu ya sherehe, washiriki wakiimba nyimbo
mbalimbali za Zaburi zilizojulikana kwa “Zaburi za Hallel” (yaani za
Haleluya - za kumsifu BWANA, ambazo ni Zaburi 113-118). Kwa kawaida
waliimba Zaburi mbili za kwanza kabla ya kula mwana-kondoo na Zaburi
nyingine baadaye (Mk 14:26).
Katika Pasaka ya mwisho ya Bwana
Yesu, Yeye na wanafunzi Wake walikula karamu siku moja kabla ya wakati
wake hasa, na labda pasipo mwana-kondoo (Lk 22:15; Yn 13:1). Inawezekana
walifanya hivyo kwa kuwa Yesu alikwisha jua kwamba Yeye mwenyewe wakati
huo alikuwa mwana-kondoo wa Pasaka; siku ya kesho yake angetoa maisha
Yake wakati ule ule ambao wanyama wangechinjwa kwa maandalizi ya karamu
iliyofuata usiku huo (Yn 18:28; 19:14,31,42).
Kifo cha Yesu
msalabani kilikuwa tendo kuu la ukombozi ambalo Pasaka ya Waisraeli
ilikuwa mfano wake mdogo tu (linganisha Kut 12:5 na 1 Pet 1:18-19, pia
Kut 12:46 na Yn 19:36, pia Kut 12:21,27 na 1 Kor 5:7). Baada ya kufa
kwake Yesu, Pasaka ya Wayahudi haikuwa na maana tena; iliondolewa na
mahali pake sherehe mpya ya ukumbusho iliwekwa, yaani Chakula cha Bwana
(Mt 26:17-30; 1 Kor 10:16; 11:23-26).
Hata hivyo, Agano Jipya
linataja mahitaji ya Pasaka katika mafundisho ya Kikristo; kwa maana
jinsi sikukuu ya Pasaka ilivyokuwa na maana kwamba Waisraeli walipaswa
kutoa "chachu" katika nyumba zao, vivyo hivyo sadaka ya Yesu Kristo ina
maana kwamba Wakristo wanapaswa kuondoa "dhambi" katika maisha yao (1
Kor 5:7-8).
Je, EASTER ndiyo PASAKA?
Neno “Easter” halipo
katika Biblia yo yote ile (ya Kiebrania – Agano la Kale, wala ya
Kiyunani – Agano Jipya). Katika maandiko yote ndani ya Biblia Takatifu
hakuna sherehe ya “Easter” kwa watu wa Mungu. Tafasiri ya neno “Easter”
tunaziona kwenye kamusi mbalimbali zikifafanua kuwa; ni sherehe za
Kikristo kuadhimisha ufufuko wa Yesu.
Hebu tutazame nukuu zifuatazo:
"Easter
· n. the festival of the Christian Church celebrating the resurrection of Christ, held (in the Western Church) on the first Sunday after the first full moon following the northern spring equinox.
– ORIGIN OE Uastre, of Gmc origin and rel. to east; perh. from Éastre, the name of a goddess assoc. with spring." –
Oxford Dictionary 10th Edition;
"Easter, annual festival commemorating the Resurrection of Jesus
Christ, and the principal feast of the Christian year... a Christian festival, embodies many pre-Christian traditions. The origin of its name is unknown. Scholars, however, accepting the derivation proposed by the 8th-century English scholar St Bede, believe it probably comes from “Ēostre”, the Anglo-Saxon name of a Teutonic goddess of spring and fertility, to whom was dedicated a month corresponding to April. Her festival was celebrated on the day of the vernal equinox; traditions associated with the festival survive in the Easter rabbit, a symbol of fertility, and in coloured Easter eggs, originally painted with bright colours to represent the sunlight of spring, and used in Easter-egg-rolling contests or given as gifts." - Microsoft ®
Encarta ® Encyclopedia 2005.
Neno “Easter” asili yake ni neno “Ēostre”
ambalo ni jina la mungu “mke” wa mavuno na uzazi aliyekuwa akiabudiwa
(amewekewa wakfu) majira ya kuchipua mimea hususani kipindi cha mwezi
April, ambayo pia ndiyo mwezi Nisani kwa Wayahudi ambao waliadhimisha
Pasaka.
Sherehe ya “Eostre / Easter” iliambatana na mambo ya
kimila; walitoa sadaka ya sungura kama alama ya uzazi, na mayai
yaliyopakwa rangi ya mng’ao ili kuwakilisha “jua” ambayo yalitumika
katika mashindano ya kupondana mayai, au kutolewa tu kama zawadi.
Sherehe hizo zilitokana na dini ya kale ya Kigiriki, walikuwa na
desturi ya kuadhimisha kurudi kwa Persephone binti wa Demeter / Ēostre
“mungu wa mavuno” kutoka kuzimu kuja duniani kwenye mwanga wa mchana
(return of Persephone, daughter of Demeter, goddess of the earth, from
the underworld to the light of day); kurudi kwake “Persephone” kwa
Wagiriki wa kale walitafasiri ni ufufuo wa maisha katika kuchipua mimea
kipindi cha mwezi April baada ya kuharibiwa na majira ya baridi kali
huko kwao. Watu hao waliamani kuwa “mungu” wao mwenye nguvu zote
alikwenda kulala wakati wa msimu wa baridi, nao wakafanya sherehe na
kucheza muziki katika majira ya kuchipua kwa mimea wakiamini “mungu” wao
ameamka toka usingizini, amerudi toka kuzimu.
Lakini, katika Biblia ya lugha ya
Kiingereza neno Pasaka limeandikwa: “Passover” likimaanisha “PITA-JUU”
kama jinsi tulivyojifunza katika Kut 12:27, malaika wa Mungu alipoziacha
nyumba za wana wa Israel kwa kupita juu na kuwaangamiza wazaliwa wa
kwanza wa Wamisri.
Sherehe hizo za
“Easter” zimeingia kwenye baadhi ya dini za Kikristo kutokana na mapokeo
kutoka dini ya kipagani ya Wagiriki wa kale.
Tukirejea katika
Biblia; hakuna sherehe za “Easter”, wala Pasaka sio “Easter”. Sherehe
hizo za kipagani “Easter” ziliadhimishwa katika majira sambamba na
sherehe za Pasaka ya Kiyahudi (mwezi Nisani / April) ambayo pia ndiyo
majira Yesu alisulibiwa, kufa na kufufuka.
Mapokeo hayo ya
“Easter” ndiyo yameingizwa hata leo katika sherehe za kidini ingawa
kiukweli huo ni upagani uliofunikwa mwamvuli wa Ukristo.
Easter sio Ufufuko wa Yesu, wala Easter sio Pasaka ya Kiyahudi.
Ninaamini ujumbe huu umewafungua fahamu watu wengi; nami nakuombea uzidi kubarikiwa katika jina la Yesu Kristo, Amen.